Mfanyabiashara Awakaanga Watumishi ARUSHA, Takukuru Yaanza Kuwashughulikia

 

Mfanyabiashara Awakaanga Watumishi ARUSHA, TAKUKURU yaanza kuwashughulikia

Tuhuma za kughushi nyaraka, uchepushaji wa makusanyo ya Serikali na ubadhirifu wa fedha za umma, zimekiweka shakani kibarua watendaji wa Jiji la Arusha wakiongozwa na Juma Hamsini.


Mashaka hayo, yanatokana na amri ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kwa Katibu Tawala wa mkoa huo, Missaile Mussa awasimamishe kazi watumishi hao kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yao, unaofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).


Mzizi wa tuhuma hizo ni hoja iliyoibuliwa jana Jumamosi Mei 18, 2024 na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato), Wilbard Chambulo akiwatuhumu watumishi hao katika Jiji la Arusha kuchepusha fedha za Serikali.


Miongoni mwa tuhuma zilizoibuliwa naye ni utengenezaji wa nyaraka bandia na kuchepusha baadhi ya makusanyo ya kodi, jambo lililomlazimu Makonda kuagiza uchunguzi wa Takukuru.


Tuhuma kama hizo ziliwahi kuibuliwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo dhidi ya Mkurugenzi wa wakati huo, Dk John Pima mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na yeye alisimamishwa kazi na kushtakiwa.


Pima na wenzake wawili Februari 16, 2023 walishinda rufaa waliyokata kupinga adhabu ya kifungo cha miaka 20 waliyokuwa wamehukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.


Hata hivyo, Machi 20, 2024 Pima na wenzake watatu walifutiwa kesi na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) na kuwafungulia kesi nyingine mbili za uhujumu uchumi ambazo bado zinaendelea.


Hayo yalijiri jijini Arusha juzi, katika kikao cha Makonda na wadau wa utalii, kilicholenga kusikiliza na kutatua changamoto za sekta hiyo katika mkoa huo.


Ilivyokuwa


Katika kikao hicho, Chambulo alionyesha nyaraka alizodai zinathibitisha matendo maovu ya watendaji wa jiji hilo.


Katika ukarasa wa kwanza wa fomu aliyopewa na halmashauri hiyo, alisema imeandikwa jina la kampuni yake, lakini namba za biashara na utambulisho si zake.


Pamoja na mazingira hayo, alisema watumishi hao walimpa namba ya malipo kwa ajili ya kulipia ushuru wa biashara uliopaswa kuwa Sh19 milioni ambao ni asilimia 0.3 ya pato ghafi.


Alieleza kushangazwa na fomu aliyopewa na halmashauri yenye taarifa tofauti na fomu halisi aliyoijaza na kuikabidhi kwao.


“Hii nyaraka siyo ya kwangu nyaraka niliyojaza ni hii hapa na mhuri wangu nimepiga, huyu alipata wapi jina linaitwa The Tanganyika Wilderness Camps, ukifungua hapa kwenye nyaraka ya halmashauri hii hapa (anaonyesha).


Ukiangalia vizuri namba ya mlipaji hii siyo hata namba ya kwetu, hata tarakimu za simu imepungua namba moja, kwa hiyo imebandikwa, yangu hii hapa (akionyesha ukurasa wa kwanza wa fomu hizo),” alisema.


Mbele ya kikao hicho, Chambulo alieleza hata utambulisho wa biashara unaoonekana katika fomu hiyo umejazwa tofauti na kampuni yake, jambo aliloshuku kwamba pengine kodi haziendi kunakostahili.


“Hii inatuogopesha kwani tunasikia kule Mbeya wanaiba, huku ukisikia wanaiba na sisi wafanyabiashara tusikubali mtu ale hela,” alieleza.


Mkurugenzi


Awali, akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Jiji hilo, Hamsini alielezea utekelezaji wa maelekezo aliyopewa na Makonda katika kikao cha kwanza cha Aprili 13, mwaka huu.


Katika kikao hicho cha awali, Chambulo aliibua tuhuma za kutozwa ushuru wa huduma kiasi cha Sh24 milioni, lakini risiti aliyopewa iliandikwa amelipa Sh3.6 milioni.


Hata hivyo, baada ya tuhuma hizo za Chambulo, Hamsini alifanya mkutano na vyombo vya habari na akisema madai ya mfanyabiashara huyo ni uongo mtupu.


Makonda


Baada ya kusikiliza maelezo ya mfanyabiashara huyo, Makonda aliagiza Takukuru kuanza uchunguzi dhidi ya watendaji wa halmashauri hiyo na wote wanaotajwa kuhusika na tuhuma hizo kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi huo.


Katika kuwasimamisha kazi, alimwagiza Katibu tawala wa mkoa huo, kulitekeleza hilo.


“Ni utovu wa nidhamu uliopitiliza kutoka kwenye kikao cha kiongozi wako amekupa maelekezo kaunde timu ya kitaalamu mpitie hoja, waite TRA, Tato na wadau wengine kaeni pitieni hoja, angalieni sheria leteni mapendekezo; lakini unakwenda kufanya press conference (mkutano na waandishi wa habari.


“Wale wote wanaohusika leo watachukuliwa na Takukuru, mfumo wote wa malipo uchunguzi utaanza leo kwa amri yangu ili tujue huyu anayepokea hela kwa ‘code number’ inayotofautiana na code namba ya kampuni husika, huyu anayepokea hela ambaye ameweka namba ya simu hata hazijakamilika halafu majina ni ya watumishi ambao wanatoka kwenda kukamata wafanyabiashara kwa mgongo wa kukusanya kodi ya Serikali, kumbe inawezekana ni mfumo unaingiza hela kwa watu wengine,” aliongeza.


Takukuru


Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mkuu wa Takukuru mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo alisema tayari uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo umeshaanza na kwa sasa wapo katika hatua ya mahojiano.


“Tumeshaanza mahojiano na tutahoji watumishi wote wa kitengo kinachohusiana na ukusanyaji wa mapato na watumishi wengine kwa kadri tutakavyohitaji taarifa, kwa sasa ni mapema mno kujua mtuhumiwa ni yupi ila tunatarajia hadi mwisho wa wiki tutajua nani mtuhumiwa na nani ni nani,” alisema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad