Simba iko chimbo ikiendelea kusuka kikosi chake kimya kimya baada ya kumaliza vibaya msimu wa 2023/2024 kwa kupoteza mataji sambamba na mabilioni ya pesa ikiwemo yale ya CAF.
Ulikuwa ni msimu dume kwa Wekundu wa Msimbazi hao wakimaliza katika nafasi ya tatu kwenye ligi, kuishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, kuondoshwa hatu ya 16 bora katika kombe la FA na kukosa taji la Mapinduzi.
Kiufupi Simba msimu uliomalizika haikufikia malengo kwa kiasi kikubwa kwani ukiacha Ngao ya Jamii na Kombe la Muungano ilikotwaa mataji hayo kwingine kote imekwama. Imekosa ubingwa wa ligi, imeshindwa kufika nusu fainali CAf, Imekwama FA maeneo ambayo yalikuwa ni malengo makuu kwa timu hiyo.
Hata hivyo, mashabiki, wachezaji na viongozi wa timu hiyo wameumizwa zaidi na kukosa nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya muda mrefu eneo ambalo ilikuwa imejiwekea ufalme ikishiriki mfululizo tangu msimu wa 2018/19 hadi 2023/2024.
Yanga na Azam ndizo zitashiriki michuano hiyo huku Simba ikiangukia Kombe la Shirikisho Afrika ikiungana na Costal Union iliyomaliza katika nafasi ya nne.
Ni dhahiri Simba imepoteza mabilioni mengi ya CAF kupitia Ligi ya Mabingwa na kila hatua ina pesa yake kubwa kuliko ile inayopatikana kwenye Kombe la Shirikisho.
Katika misimu sita mfululizo ambayo Simba ilishiriki Ligi ya Mabingwa, ilifika robo fainali mara nne na misimu miwili kuishia katika hatua za mwazo.
Kila hatua ilikuwa inalipwa pesa nyingi tu. Mfano msimu uliopita kufika robo fainali ilikunja zaidi ya Sh2.3 bilioni.
Pesa hiyo ni kubwa kuliko ile ambayo Simba itaipata msimu huu kama itafika robo fainali ya Kombe la Shirikisho na itavuta takriban Sh700 milioni.
Ili kufikia hizo Sh2.3 bilioni ilizokuwa ikivuna mara kwa mara inapofika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba itatakiwa kupambana na kuhakikisha inafika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na itapata Sh3.6 bilioni.
Kwa mara ya mwisho Simba kushiriki moja kwa moja kombe la Shirikisho ilikuwa msimu wa 2017/2018 na iliondolewa hatua za mwazo na Al Masri ya Misri kwa sheria ya bao la ugenini baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 Uwanja wa Mkapa na kutoa suluhu (0-0) ugenini.
Msimu wa 2021/2022 Simba ilishiriki Kombe la Shirikisho lakini hapo haikuwa moja kwa moja bali ilidondokea huko baada ya kutolewa ligi ya mabingwa katika hatua ya pili ya mtoano na Jwaneng Galaxy ya Botswana kwa sheria ya bao la ugenini na ‘Mnyama’ alishinda 2-0 ugenini lakini bila kuamini akachapwa 3-1 Uwanja wa Mkapa na matokeo ya jumla kuwa 3-3.
SHIDA IKO HAPA
Makocha wa zamani wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems ‘Uchebe’ na Mbrazil Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ambao wote kwa nyakati tofauti waliifikisha timu hiyo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kila mmoja alitoa maoni yake nini kinaifelisha Simba kwa sasa.
“Ujue Simba na Afrika kwa jumla viongozi wengi wa soka hawafanyi kazi kwa uweledi. Wanapenda kuingilia majukumu na pia ni ngumu kutoa mahitaji muhimu kwa benchi la ufundi na wachezaji kwa wakati ikiwemo usajili unaofanya. Hizo ni baadhi ya sababu zinazoiangusha Simba,” alisema Aussems ambaye kwa sasa yupo nchini Ufaransa baada ya kuachana na AFC Leopards ya Kenya.
Kwa upande wa Robertinho aliyefukuzwa msimu uliopita baada ya kufungwa 5-1 na Yanga alisema;
“Simba imekwama kutokana na kikosi ilichonacho. Wachezaji wengi walikuwa wa kawaida lakini hata pale ilipohitajika kusajili wachezaji bora zaidi timu haikufanya hivyo,” alisema Robertinho aliye nchini kwao Brazil tangu amefutwa kazi na Simba.
Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali alisema Simba imekwama kutokana na makundi yaliyokuwepo katika uongozi lakini kwa sasa imeanza kuyatatua.
“Ukiachana na yote jambo kubwa lililotuyumbisha katika kipindi cha hivi karibuni ni makundi. Baada ya uchaguzi mkuu kufanyika Simba iligawanyika na kuwepo kwa makundi mawili hadi matatu.
Lipo kundi lililokuwa upande wa Mangungu (Murtaza), lingine upande wa Kaluwa (Moses) aliyekuwa mgombea mwenza lakini pia yalikuwepo mengine,” alisema Dalali na kuongeza;
“Mpasuko huo ndio ulileta shida kwani umoja na ushirikiano kwenye timu ulikosekana lakini nashukuru hilo limeisha na tuna mpango mkakati wa kuhakikisha timu inakuwa na umoja wa hali ya juu jambo ambalo tulianza kwa kuwapatanisha kisha kwenda kwa wanachama kuanzia Zanzibar, Mbeya, Morogoro na baadae nchi nzima.”
Mchambuzi wa soka na Mwandishi wa Mwanaspoti, Oscar Oscar alisema Simba imeponzwa na kutokuwa na msingi imara wa wachezaji wazawa.
“Tatizo kubwa la Simba sio wachezaji wa nje, ni kushuka kiwango na majeraha kwa wachezaji wazawa. Pamoja na ubora wa wageni, Simba iliyotisha hivi karibuni ilikuwa na wachezaji wengi bora wazawa. Manula (Aishi), Erasto Nyoni, Kapombe (Shomary), Zimbwe Jr, Boccco (John), Jonas Mkude na Muzamiru Yassin,” alisema Oscar na kuongeza;
“Simba inahitaji wachezaji watano hadi sita wazawa kwenye kikosi cha kwanza. Msingi wa Simba bora unajengwa na wazawa bora,” alisema Oscar aliyetoa mfano wa Yanga ilivyo imara kwa sasa kutokana na kuwa na wazawa wengi walio kwenye kiwango bora akiwataja Mudathir Yahya, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca, Jonas Mkude na Clement Mzize.