Mtanzania, Denis Mfumbulwa (44) anayedaiwa kujipatia huduma ya kula katika Hoteli ya Serena bila kulipa, ameachiwa huru katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo jijini Dar es salaam kwa sababu hakuna ushahidi wa kuthibitisha kama kesi hiyo dhidi yake ni ya jinai.
Mfumbulwa ambaye ni Mkazi wa Goba ameachiwa leo na Hakimu Gladness Njau wakati kesi hiyo ilipoitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kusikilizwa.
Mapema Meneja wa Hoteli hiyo, Desdery Doto alifika Mahakamani hapo kutoa ushahidi ambapo alipoulizwa alidai Mshtakiwa alifika hotelini hapo na kupata huduma ya chakula na malazi bila kulipa na kisha akatoweka.
Kufuatia maelezo hayo, Hakimu Gladness Njau alimuachia huru Mshtakiwa huyo akisema “inaonekana asili ya shauri hili ni la madai na siyo jinai hivyo kama Mlalamikaji ataona inafaa afungue kesi ya madai”
Katika kesi hiyo Mshtakiwa Mfulumbwa anayeishi Goba Kulangwa anadaiwa kuwa Machi 6,2022 hadi Machi 28,2024 kwa nyakati tofauti katika Hoteli ya Serena Wilaya ya Ilala, Dar es salaam alijipatia huduma ya malazi na chakula yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 21 bila kulipa ambapo baada ya kupatiwa huduma hiyo alitoweka huku akijua kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria.
Akizungumza nje ya Mahakama Meneja Doto amesema yuko tayari kuendelea na kesi ya madai hivyo anasubiri nakala ya hukumu.