Jessica Mshama ametoa taarifa kupitia ukurasa wake wa Instagram akikanusha taarifa iliyotolewa na tovuti ya Kenya ikimuhusisha na jina Jessica Magufuli.
"Ninaomba kutumia ukurasa wangu rasmi wa Instagram kusema kwa mara nyingine juu ya taarifa zinazotolewa na media kuambatanisha picha yangu na kunitaja kama Jessica Magufuli! Naomba kwa yeyote atakayekutana na hii taarifa aipuuze".
Aliongeza kusema, "Mimi ni Jessica Mshama na sio Jessica Magufuli! Naomba radhi kwa niaba ya media zinazotoa hizi taarifa za kupotosha watu".
Taarifa hizi zimekuja baada ya habari iliyochapishwa na mtandao maarufu wa Tuko Mei 13; "Jessica Magufuli, binti wa hayati rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, alifurahishwa alipokutana na Matatu (Dala dala) nchini Kenya iliyopambwa na picha za baba yake" Na kutumia picha yake (Jessica Mshama).
Jessica Mshama ambaye ni Mjumbe wa bodi, Baraza la Sanaa la Taifa, amesisitiza kuwa hana uhusiano wowote na familia ya Magufuli na anaomba vyombo vya habari kuheshimu ukweli huo.