Mwenyekiti Kamati ya Harusi Abeba Mke wa mtu

Mwenyekiti Kamati ya Harusi Abeba Mke wa mtu


Ilianza kama kuzoeana kwa kawaida kati ya mke wa mkazi mmoja wa Nairobi na aliyekuwa kiongozi wa kamati ya harusi yao miaka 15 iliyopita, kiliishia kuwa sababu ya ndoa kuvunjika.


Hatutatumia majina halisi ya watatu hao kwa sababu hili ni suala nyeti sana. Dishon ambaye ni mkazi wa Nairobi, anasema licha ya kupokonywa Rhoda ambaye alikuwa barafu ya moyo wake “ninahisi kuwa mwepesi na kuondolewa mzigo mzito”.


Baba huyo wa watoto wanne aliambia Taifa Leo wakati wa mahojiano kwamba, hakuwahi kufikiria mkewe angemwacha hata kwa sekunde mbili kutokana na bidii aliyokuwa akitia kufatutia familia.


Anasema baada ya kuishi kwa muda wa miaka minne na mkewe, alianza kushangazwa na baadhi ya kauli zake, kumtaka afanye baadhi ya mambo na majukumu kama mwenyekiti wa mipango ya harusi yao.


“Mwanzoni sikuwa na shida yoyote kuambiwa vile, lakini siku kadri siku zilivyosonga ndivyo nilianza kuona mke wangu alikuwa na vijimambo,” akasimulia.


Kauli hizo zilifanya aanze kuchunguza simu ya mkewe. Kila wakati aliposhika simu ya mkewe, alipata alikuwa akifanya mazungumzo ya muda mrefu na mwenyekiti wa kamati ya harusi, akishangaa ni yapi waliyozungumzia.


“Kila siku nilipata mawasiliano kati ya mke wangu na mwenyekiti wa kamati ya harusi yakiwa ni ya muda wa kati ya dakika 45na saa moja. Yeye nikimuuliza alikuwa akiniambia ni majadiliano ya kibiasahara,” akakumbuka.


Lakini Waswahili wanasema yaliyopita si ndwele na kwamba ukupigao ndio ukufunzao. Anajuta kumweka karibu rafiki yake ambaye alifanya mapinduzi ya serikali yake ya mapenzi.


Anajilaumu kwa kumkaribisha rafiki huyo ndani ya familia yake, akisema tangu kumpata mke mwingine, ameweka mipaka kuhakikisha ndoa inadumu.


Anakiri awali, aliruhusu rafikiye kuja nyumbani kwao na kulala kila alipotaka. “Kila jambo huwa ni funzo. Nilioa mke mwingine lakini siwezi kuruhusu rafiki yangu aje kulala kwangu. Mwenyekiti wa kamati ya harusi katika ndoa yangu iliyovunjika alikuwa na uhuru wa kuja kwangu kulala,” anaeleza.


Anadai mwenyekiti wa kamati wakati mwingi alikuwa akifika kwake na kukataa kwenda nyumbani kumsumbua mke wake.


“Kwa hivyo nilimpa mafasi ya kuja kwangu kualala kwenye kiti, hata zaidi ya mara tatu kwa wiki,” akasema.


Mwaka 2017, viongozi wa kanisa na familia ya Dishon waliitwa kwenye kikao ili kusuluhisha mgogoro wa ndoa uliokuwa ukitokota baina ya watatu hao.


Hapo kikaoni anasema aliaibika kwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya harusi hata alifichua kuwa kazi aliyofanya Dishon, ni yeye alimtafutia.


Familia yake ilionekana kuengemea upande wa mwenyekiti huyo ambaye pia alifahamika kufadhili harusi yao kwa zaidi ya Sh200,000.


“Wengi walibaki vinywa wazi kufahamu kuwa hata kazi niliyokuwa nikifanya na kupokea mshahara wa Sh150,000 kwa mwezi, ni mwenyekiti huyo aliyekuwa amenitafutia,” akasema.


“Kikao ni kaka zangu wawili waliitisha. Nikiwa pale, mwenyekiti alisema kama alitaka kumchukua mke wake, hata hangetoa kufanikisha harusi yetu,” akaongeza.


Anasema kikao cha kutengeneza mambo kiligeuka cha maswali ya aibu na yakumvunja moyo, ikiwa ni ishara kuwa hana lake.


Lakini Paulo* ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa mipango ya harusi na kugeuka mume wa Bibi harusi, aliambia Taifa Leo kuwa ugomvi baina ya wawili hao ndio ulimfanya kumtafutia mwanamke huyo nyumba.  Anasema kilio cha kila wakati na kukosa suluhu kwa wawili hao, vilichangia mpasuko zaidi.


“Hata kama nilikuwa naongea na mke wake, sikuwa na nia mbaya. Mazungumzo yetu yalikuwa kuhusu malalamishi ya ndoa yao kama zile nyingine,” akasema Paulo. Paulo anafichua mama yake alimshauri kumtafutia mwanamke huyo nyumba kisha amlipie kodi ya miezi mitatu kabla awe sawa.


“Mke wa rafiki yangu alikuwa anapitia magumu nikawa sina budi,” akakiri. Rhoda ambaye ni mchache wa maneno anasema uamuzi wake wa kuondoka kwenye ndoa yake ni kutokana na kutaka kufuata ndoto zake tu.


“Nilihitaji kuwa huru kuweza kufanya mambo yangu bila kukaziwa maisha. Asante,” akasema Rhoda.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad