Waziri wa Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Nape Nnauye amesema taarifa ya awali kutoka kwa Watoa huduma wa nyaya za baharini imesema kuna hitilafu kwenye nyaya zao ambayo ndiyo iliyopelekea kukosekana kwa huduma ya intaneti na huduma za simu za Kimataifa tangu saa tano asubuhi Nchini Tanzania.
“Mnamo majira ya saa tano asubuhi, tumeshuhudia kukosekana kwa huduma za intaneti pamoja na huduma za simu za kimataifa (international Voice), tumepokea taarifa ya awali kutoka kwa Watoa huduma wa nyaya za baharini (submarine cables), Seacom na EASSy, kwamba kuna hitilafu kwenye nyaya zao zilizo baharini” ——— Nape.
“Seacom na EASSy wameripoti kuwa kuna tatizo kwenye nyaya kati ya Msumbiji na Afrika Kusini iliyosababisha kukosekana kwa huduma hiyo Nchini Tanzania” ——— ameongeza Waziri Nape.
“Jitihada za kutatua tatizo hilo zinaendelea, aidha wakati utatuzi wa tatizo hilo unaendelea, upatikanaji wa huduma za intaneti pamoja na huduma za simu za kimataifa utakuwa wa kiwango cha chini kwa kutumia njia mbadala mpaka tatizo husika litakapotatuliwa, poleni kwa usumbu wowote uliojitokeza” ——— amemalizia Waziri Nape.