Si unafahamu Yanga SC inahitaji pointi nne pekee ili kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu? Sasa basi vigogo wa timu hiyo wametumia akili nyingi ili kuwafurahisha wanachama na mashabiki wa timu hiyo kongwe hapa nchini.
Ipo hivi; leo Jumatatu Yanga itakuwa Manungu Complex, Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa raundi ya 27 wa Ligi Kuu Bara.
Mchezo huo utakaoanza saa 10:00 jioni, hesabu za Yanga ni kushinda na kufikisha pointi 71 ili ikienda Dodoma kupambana na Dodoma Jiji, itangaze ubingwa ikihitaji pointi moja tu zitakazowafanya kuwa na 72 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote.
Katika hesabu hizo, ikimalizana na Dodoma Jiji na mambo yakienda sawa na kutangaza ubingwa, mechi mbili za mwisho itakuwa mwenyeji dhidi ya Tabora United na Tanzania Prisons Mei 25 na 28 mwaka huu.
Mechi hizo mbili za mwisho kabla ya kukabidhiwa ubingwa wao, mipango waliyonayo ni kuzihamisha kutoka Dar es Salaam ilipo ngome yao na kuzipeleka Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri.
KWA NINI DODOMA?
Akili kubwa waliyoitumia Yanga wamelenga zaidi katika suala zima la kushangilia ubingwa wanaoamini katika mechi nne zilizobaki hawatafanya makosa lazima wabebe kutokana na mwenendo wao bora ulivyo kwa sasa.
“Mipango iliyopo sasa ni kuhakikisha hizi mechi mbili zinazofuata kuzicheza vizuri ili kukusanya pointi nne zitakazotupa ubingwa,” kilisema chanzo kutoka ndani ya Yanga.
“Baada ya hapo uongozi umepanga kuzihamisha mechi mbili za mwisho kutoka Dar es Salaam kuzipeleka Dodoma kwa ajili ya jambo moja kubwa la kusherehekea ubingwa.
“Si unajua mechi ya mwisho ndiyo tutakabidhiwa ubingwa? Basi uongozi umeona kama ubingwa tukikabidhiwa hapa Dar basi ule mzuka wa ‘parade’ la ubingwa hautanoga ndiyo maana sherehe zinapangwa kuanzia Dodoma na huko mashabiki na wanachama wetu watapata fursa ya kuungana nasi kabla ya kurudi Dar, si unajua sisi hatuna jambo dogo.”
Endapo Yanga itabeba ubingwa huo utakuwa ni wa tatu mfululizo na wa 30 kwa jumla tangu kuanzishwa kwa ligi hiyo na itaifanya timu hiyo kuzidi kutanua wigo wa kuwa washindi mara nyingi wakiiacha Simba kwa makombe manane kwani wanayo 22 ya Ligi Kuu.
Kuutumia Uwanja wa Jamhuri Dodoma huenda likawezekana kwa Yanga kwani mwenyeji wa uwanja huo Dodoma Jiji mechi zake mbili za mwisho itakuwa ugenini.
Dodoma Jiji itacheza dhidi ya Ihefu Uwanja wa Liti mkoani Singida kisha Mashujaa, Lake Tanganyika mkoani Kigoma, hivyo Uwanja wa Jamhuri utakuwa umebaki tu hauna mwenyewe.
KANUNI ZINAWARUHUSU
Inachofanya Yanga kikanuni inaruhusiwa kama zilivyofanya timu nyingine ikiwamo Simba na ilihamia CCM Kirumba, Mwanza na ikacheza dhidi ya Azam FC zikatoka sare ya bao 1-1. Pia iliutumia Uwanja wa Jamuhuri, Morogoro dhidi ya Tanzania Prisons na ilifungwa mabao 2-1, mechi zote hizo Simba ilikuwa mwenyeji.
Kanuni ya 9 inayozungumzia uwanja, inafafanua jambo hilo kwa upana zaidi kwa namna hii;
(1) Uwanja wowote kwa michezo ya Ligi Kuu ni lazima uthibitishwe na TFF.
Klabu itachagua na kutambulisha uwanja wake wa nyumbani na kuitaarifu TPLB katika kipindi cha Uthibitisho wa ushiriki Ligi Kuu.
(2) Katika mazingira maalum timu inaweza kucheza mchezo wake wa nyumbani katika uwanja mwingine endapo kuna sababu nzito na za msingi,
Utambulisho wa uwanja katika mazingira haya pia unawajibika kufanywa katika kipindi cha uthibitisho wa kushiriki ligi au kwa maombi maalum kwa TPLB angalau siku 7 (saba) kabla ya tarehe ya mchezo husika.
(3) Katika kutambulisha uwanja wake wa nyumbani, klabu inawajibika kuhakikisha uwanja huo unakidhi vigezo vyote na masharti kama vilivyoainishwa kwenye kanuni za leseni za klabu.
(4) Endapo timu yoyote haina uwanja wa nyumbani unaofaa kwa mchezo wa Ligi Kuu inaweza kuchagua uwanja mwingine katika mji au mkoa jirani na mkoa wa timu husika ndani ya Tanzania Bara ulio na sifa zinazokubalika na uthibitishwe au kuidhinishwa na TFF, baada ya uteuzi wa uwanja timu haitaruhusiwa kubadilisha uwanja huo kinyume na sababu za kikanuni.
(5) Kutokana na sababu za kiusalama, uwanja kutofikika, kushindwa kukidhi vigezo vya Leseni za Klabu au sababu nyingine yoyote ya msingi, TFF kwa kushauriana na timu mwenyeji inaweza kuhamishia mchezo husika katika uwanja wa mji au mkoa jirani unaokidhi haja hiyo.
(6) TFF/TPLB ina mamlaka ya mwisho ya kuhamishia mchezo katika uwanja mwingine au kubadilisha kituo cha mchezo kwa sababu inazoona zinafaa kwa mchezo na wakati husika.
(7) Timu ya Ligi Kuu inaweza kuteua viwanja vingine miongoni mwa viwanja visivyokuwa na michezo ya Ligi Kuu kwa michezo yake miwili tu ya nyumbani na kuwasilisha Uteuzi wake huo siku ishirini na moja (21) kabla ya mchezo husika inayokusudia kucheza kwenye uwanja wa uteuzi. Masharti ya uwasilishaji yatazingatia pia kanuni ya 9:3 ya Kanuni hizi. Uwanja ukishapitishwa hautabadilishwa isipokuwa kwa mazingatio ya Kanuni ya 9:6.
KAULI YA BODI YA LIGI
Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TP:B), Karim Boimanda, amezungumzia hilo akisema kama kuna mazungumzo yanayoendelea baina ya taasisi mbili kwa maana ya Yanga na Bodi ya Ligi yanakuwa siri hadi pale yatakapofikia mwafaka ndipo watatangaza rasmi.
“Siku zote mawasiliano baina ya taasisi mbili kati ya timu na Bodi yanakuwa siri kwa sababu huwezi kusema moja kwa moja kwa jamii kitu ambacho bado hakijakamilika, hivyo basi kama jambo hilo lipo tutatoa taarifa iliyonyooka,” alisema Boimanda na kuongeza.
“Ukiangalia katika mechi hizi za mwisho kuna ushindani mkubwa sana hivyo lazima tuwe macho kwa kila kitu kwa sababu mpaka sasa hakuna timu iliyoshuka daraja wala iliyochukua ubingwa.
“Pia katika ile nafasi ya pili haina mwenyewe na zingine zinapambana kumaliza nne bora, utaona hapo jinsi gani ligi ilivyo ngumu nyakati hizi za mwisho ndiyo maana tunasema tunafanya vitu kwa umakini zaidi ili tusiharibu mazuri tuliyoyaanza kwani watu wanasubiri ukosee wasahau yale yote mazuri yaliyofanyika nyuma.”
Katika hatua nyingine Boimanda alibainisha wao kama Bodi ya Ligi wamejipanga kuhakikisha mechi za raundi mbili za mwisho kuongeza nguvu kwa wasimamizi wa michezo hiyo ili kila kitu kiende kama kilivyopangwa kusiwe na malalamiko ya upande mmoja kuonewa.
“Ndiyo maana ukiangalia ratiba ya ligi zile mechi za mzunguko wa 29 na 30 tumezipanga zote zichezwe siku moja na muda mmoja.”
AZAM, SIMBA, YANGA ZAWATIBULIA BODI
Katika raundi ya 29 na 30, ratiba inaonyesha Simba na Yanga zina mechi za nyumbani na zote hizo zimekuwa zikitumia Uwanja wa Azam Complex jambo ambalo linawafanya Bodi ya Ligi kufikiria kuzipangia viwanja vingine timu hizo ili kuendana na mipango yao. Azam wao mechi moja kati ya hizo inapaswa kucheza nyumbani na ya mwisho ugenini.
“Ndani ya siku mbili au tatu kila kitu kitafahamika mechi hizo zitachezwa uwanja gani na mkoa gani ili tu tusiharibu kile tulichokipanga,” alisema Boimanda.