Paul Makonda Aomba Siku 100 Kutimiza Ahadi zake




Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ameahidi kuwa ndani ya siku mia moja za uongozi wake Mkoani Arusha atakuwa amekamilisha ahadi zake zote alizoziahidi tangu alipoteuliwa Machi 30, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Mkuu wa Mkoa Paul Christian Makonda ametoa kauli hiyo leo Mei 16 wakati alipokuwa akikabidhiwa pikipiki 20 kwaajili ya kuimarisha Ulinzi na usalama Mkoani Arusha, pikipiki ambazo zimetolewa na Benki ya Biashara ya CRDB ikiwa ni sehemu ya programu yake ya kurudisha kwenye Jamii.

Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema miongoni mwa ahadi zake ilikuwa ni pamoja na kuliimarisha Jeshi la Polisi kwa kuwapatia Nyenzo za ufanyaji wa kazi katika kuimarisha Ulinzi na usalama Mkoani Arusha ambapo aiahidi kuwatafutia pikipiki 50, Baiskeli za Umeme 100 na magari 20 kutoka kwa wadau mbalimbali wa Maendeleo.

Mhe. Makonda amesema anatambua kuwa Usalama ni kivutio namba moja katika kuvutia utalii Mkoani Arusha na hivyo ameishukuru Benki ya CRDB kwa kumuunga mkono Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maagizo yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ya kuhakikisha anakuza utalii kwenye mkoa wa Arusha.

Mhe. Mkuu wa mkoa pia amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara mbalimbali kuendelea kuwekeza Mkoani Arusha na anasema kufikia Mwezi Julai tarehe 30 Biashara ndani ya Mkoa wa Arusha zitakuwa zinafanyika kwa saa 24 kwani Usalama na Ulinzi wa mkoa utakuwa umeimarika kwa kiwango cha juu kabisa.

Katika hatua nyingine Mhe. Mkuu wa Mkoa amemuomba Mkurugenzi Mtendaji Benki ya CRDB, Bw. Abdulmajid Nsekela kuandaa Mpango maalumu wa usaidizi wa mikopo kwa wawekezaji wa ndani, ili kuwezesha Ujenzi wa Malazi ya kutosha Mkoani Arusha katika jitihada za kuondoa ufinyu wa nyumba za kulala wageni na watalii wanaofika mkoani Arusha kutalii na kwenye mikutano na warsha mbalimbali.

Mhe. Mkuu wa Mkoa pia amevishukuru vyombo vya ulinzi na usalama Mkoani Arusha kwa kuendelea kupunguza uhalifu kwa kasi kubwa akihaidi kuendelea kushirikiana nao katika kuwawezesha vitendea kazi na dhana mbalimbali ili kuondosha vikwazo katika majukumu yao.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad