Paul Makonda Asema Anaogopa Kurudi Mtaani, ni Kugumu




MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema anatambua "mtaani ni kugumu" na asingependa arejee tena katika maisha bila ajira.

Makonda ana uzoefu wa kukaa nje ya mfumo wa ajira serikalini na chama (CCM), akikaa nje ya mfumo huo kuanzia Julai 15, 2020 Rais John Magufuli alipomwondoa kwenye nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam hadi Oktoba 22, 2023 CCM ilipomteua kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya chama - Itikadi, Uenezi na Mafunzo.

Amesema anahitaji msaada wa Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi kutekeleza majukumu aliyoagizwa na Rais Samia Suluhu Hassan mkoani Arusha.

Makonda alitoa kauli hiyo jana wakati wa semina ya uwekezaji na elimu ya fedha iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa wanahisa wake na Watanzania kuelekea Mkutano Mkuu wa 29 wa Wanahisa wa benki hiyo unaofanyika leo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), jijini Arusha.

Alisema kuwa ameagizwa na Rais Samia kuhakikisha anachochea kasi ya uwekezaji katika sekta ya utalii ili kuongeza wageni wanaotembelea mkoa huo.

Makonda, aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni (kuanzia Februari 19, 2015 akiteuliwa na Rais Jakaya Kikwete hadi Machi 13, 2016 alipoteuliwa na Rais Magufuli kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alisema asipenda kuona familia yake ya watoto watatu inapata tabu.

"Mimi ninavyokufahamu wewe Mheshimiwa Rais Mwinyi, ni rafiki yangu, wewe ni rafiki wa watu wengi wema, Makonda alisema. Mimi nina maombi mawili tu. Arusha na Zanzibar hatuwezi kukwepana, watalii wanaotua Zanzibar ndiyo hao wanaokuja kutua Arusha.
Ombi langi la kwanza, nifikishie salamu zangu za upendo wa watu wa Zanzibar, waambie kila wanapopata mtaalii - iwe ni Unguja, iwe ni Pemba, waambie wasiishie pale, waje wamtembee ndugu yao ambaye yuko Arusha.

La pili, Mheshimiwa Rais, unafanya kazi kubwa sana kule Zanzibar, kila siku unafungua hoteli, na mimi nimepewa hii ajenda na Mheshimiwa Samia, watoto wangu - ninao watatu, mkubwa ana miaka mitano, wale pacha wana umri wa miaka mitatu, nilishakaa mtaani nikaona hali ya mtaani.


Rais amenipa agizo kuchochea utalii, kasema 'kahakikishe unaongeza vyumba'. Usiponishika mkono wewe kaka yangu Mheshimiwa Mwinyi, nitapata wapi wawekezaji wa kujenga hoteli katika mkoa wangu wa Arusha?

Kwa unyenyekevu mkubwa ninakuomba, wale wanaojenga hoteli Zanzibar, waambie una mdogo wako Makonda, yuko Arusha, ili wale wawekezaji kutoka huko duniani wakatua Zanzibar, basi wakija, wawe na matawi yao mkoani Arusha kuendeleza shughuli za utalii," alisema.

Katika hotuba yake ya kufungua semina hiyo, Rais Dk. Mwinyi alijibu maombi hayo ya Makonda, alisema ombi lake la kwanza tayari linafanyiwa kazi.
Alisema ni ukweli usiofichika kwamba watalii karibu wote wanaokuja Tanzania, ni ama wanaanzia Tanzania Zanzibar kish wanakwenda Arusha au wanaanzia Arusha kisha wakwenda Zanzibar.


"Kwa hiyo, hili linafanyika, Ninaweza kukuhakikishia leo ukitaka kupata ndege ya kwenda Zanzibar kutoka hapa Arusha inabidi ukate mapema sana kwa sababu wasafiri ni wengi. Ombi hili tayari linatekelezwa.

"Lakini lile la uwekezaji sasa, kwamba wawekezaji wanaojenga hoteli, na ni kweli kule Zanzibar sasa hivi tumepata neema ya uwekezaji mkubwa katika sekta ya utalii, hoteli nyingi zinajengwa, na zingine zinajengwa katika visiwa vidogo.

"Hivi karibuni tutafungua ya kwanza, Juni Mosi mwaka huu tutafungua hoteli ya kwanza iliyojengwa katika kisiwa. Ni ya aina yake kwa kweli! Sasa hawa tuko tayari kuwashawishi waje kuwekeza na upande wa pili ili mnyonyoro wetu huu wa utalii uendelee.

"Ni ama waanze kwenye safari wamalizie kwenye fukwe au waanze kwenye fukwe wamalizie kwenye safari huku. Hili ni jambo ambalo tupo pamoja Mhehimiwa Mkuu wa Mkoa (Makonda)," Rais Dk. Mwinyi aliahidi, akiomba wanahisa wa CRDB mkutano wao wa 30 mwakani ufanyike Zanzibar.

Katika salamu zake, Makonda pia alisema wanatekeleza kwa kasi mradi wa ujenzi wa kisasa wa soka mkoani Arusha ambao serikali imetoa zabuni ya Dola milioni 112 (Sh. bilioni 286).

Katika kutekeleza maagizo ya Rais Samia - kuchochea utalii mkoani Arusha, Makonda alisema wana mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa vifaa vya kulisaidia Jeshi la Polisi kuimarisha usalama; ameahidi kulipa jeshi hilo magari 20, pikipiki 50, baiskeli za umeme 100.

"Baada ya miezi mitatu minne ijayo ukija Arusha utakutana na polisi wa utalii, vijana wazuri, wenye uwezo wa kuongea lugha zote mbili; Kiingereza na Kiswahili.

“Watamkaribisha mtaalii vizuri. Ninawashukuru CRDB kwa kutuunga mkono katika kuwezesha upatikanaji vifaa hivi. Asiyetambua kule alikoshikwa mkono, hawezi kutambua anakoelekea," alisema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad