Paul Makonda "Wameanza Kupiga Simu Kwa Viongozi Wangu Kunishtaki"




Mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda ametoa wito kwa wale wote wenye mawazo na ushauri utakaosaidia kuboresha zoezi analolifanya la kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa namna moja au nyingine wamfikishie ushauri huo yeye mwenyewe badala ya kupiga simu za 'uchonganishi' kwa wakuu wake wa kazi na kuanza kupenyeza mambo ambayo kiuhalisia hayana mashiko

Akizungumza na mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye viunga vya ofisi ya Mkuu wa mkoa huo jijini Arusha ikiwa ni muendelezo wa kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia majawabu leo, Ijumaa Mei 10.2024 Makonda amesema kwa namna yoyote ile kiongozi yeyote ambaye amewahi kuwadhulumu au kuwanyanyasa wananchi kamwe hatofurahi kuona au kusikia yeye (Makonda) akiwaita wananchi hao kwa ajili ya kuwasikiliza kwa kuwa anafahamu kuwa maovu yake yatawekwa hadharani

Amesema katika kupambana aibu hiyo isimtokee mtu huyo ni lazima atahangaika kuwasiliana na viongozi wake (Makonda) wa kitaifa akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamedi Mchengerwa, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko na wengineo ili kumchongea ionekane jambo analolifanya ni kinyume na sheria

"Atajidai anapiga simu kwa viongozi wangu kama vile anataka kuongea jambo la maana, wewe kama una jambo la maana mtafute Makonda mwenyewe aboreshe ili wananchi wapate haki zaidi, mimi najulikana nipo hapa (Arusha) nitafute uniambie kwamba Makonda hapa ungeongeza hiki, hiki ungepunguza ili wananchi wengi wapate haki, tunapokea hayo mawazo vizuri lakini kupigapiga simu kwa viongozi wangu wakubwa huko, kukatakata 'viclip' kupeleka kwamba sasa hapa unajuwa atatengeneza mgogoro kati ya Mahakama na serikali, soma sheria ya mwaka 2011 imenipa nafasi (Mkuu wa mkoa) ya kusikiliza na yale nitakayoyabaini nitamwambia Jaji mfawidhi kwamba hapa kuna moja, mbili, tatu" -Makonda

Makonda amesema ni lazima viongozi na watumishi wa umma wawasikilize wananchi wanaowahudumia ili kutambua changamoto zao kisha kuzifanyia kazi kulingana na mahitaji ya wananchi husika

Amesema anataka kuona mkoa wa Arusha unaibuka kinara kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika baadaye mwaka huu (2024)

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad