WAKATI Klabu ya Simba ikieleza tayari imeanza mchakato wa kumsaka kocha mpya wa kurithi mikoba ya Abdelhak Benchikha aliyeachana na timu hiyo mwishoni mwa wiki, viongozi wa klabu hiyo wameonywa na kutakiwa kujitathimini kwanza.
Benchikha na Simba walifikia makubaliano ya pande zote za kuvunja mkataba baada ya kocha huyo kuhudumu chini ya msimu mmoja.
Akizungumza na Nipashe jana kutoka Ruangwa mkoani Lindi, Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema tayari viongozi wameanza kusaka kocha mpya kutokana na vigezo walivyoviweka.
"Nipo nje ya ofisi, lakini kwa uhakika tayari viongozi wameanza mchakato wa kusaka kocha wetu mpya, taratibu zipo hatua ya awali na mambo yakienda sawa mashabiki na wanachama wetu wataambiwa kila kitu," alisema Ahmed.
Alisema viongozi wapo kwenye mchakato huo na wapo makini kuhakikisha wanapata kocha mwenye uwezo mkubwa na sifa za kuifundisha timu hiyo.
"Lazima atakuwa kocha mwenye viwango vikubwa, Simba ni timu kubwa, hivyo lazima ipate kocha anayeendana nayo... mchakato huu wa kumpata kocha mpya unafanywa kwa weledi mkubwa," alisema Ahmed.
Jana, Juma Mgunda, aliiongoza Simba kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo FC kama kocha mkuu wa muda akichukua nafasi ya Benchikha.
Wakati huo huo Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, amewataka viongozi wa Simba kufanya haraka mchakato wa kumpata kocha mpya ili ahusike na usajili wa wachezaji wa msimu ujao, badala ya kufanya usajili wenyewe na kumleta kocha baadaye kama ambavyo wamekuwa wakifanya kwa misimu ya karibuni.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Makalla, ambaye ni shabiki na mwanachama wa klabu hiyo, pia amewataka viongozi wa klabu hiyo kujitathimini kwani imekuwa ni kawaida kwa klabu hiyo makocha kuondoka au kutimuliwa baada ya timu kufanya vibaya, akisema inabidi sasa kitafutwe chanzo cha matatizo yote hayo, badala ya kuwaangushia jumba bovu walimu.
Makalla, ambaye kabla ya wadhifa huo mara ya mwisho, alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, alisema hayo baada ya Klabu ya Simba kuvunja mkataba na kocha wake, Mualgeria Benchikha ambaye aliomba kufanya hivyo kwa kile alichodai kwenda kumuuguza mkewe.
"Ushauri wangu kwa Simba, sawa kocha ameondoka, sasa wakae, wahakikishe kocha wanampata haraka, siyo ameondoka viongozi wakafanya usajili wenyewe wakati haijapata mwalimu.
"Nashauri wampate kocha haraka, halafu huyo ndiye afanye usajili, isiwe kinyume chake, eti kocha hajapatikana halafu wanasajili, anakuja tayari wameshapata wachezaji wapya, hii haitokuwa sawa, matatizo yatakuwa ni yale yale," alisema Katibu huyo.
Kiongozi huyo pia aliitaka klabu ya Simba kutatua tatizo la msingi na si kukimbilia kuvunja mikataba wa makocha kama ambavyo imekuwa ikifanyika hivyo mara kwa mara pale timu inapokuwa haifanyi vizuri.
"Mimi huwa sipepesi maneno, Simba ni lazima itatue tatizo la msingi. Tuangalie Simba tatizo ni nini? Ni wachezaji? Je, ni uongozi? Ni makocha? Na kwa nini kila mara Simba ikitokea haifanyi vizuri ni kocha ndiye anafukuzwa au anaondoka? Sisi hatutakiwi kujitafakari kwamba tunawapa makocha wachezaji wanaotakiwa? Majukumu yetu kama viongozi tumeyatimiza? Nadhani imefika wakati tunaona kama vile pale Simba mgonjwa wa malaria anapewa dawa ya kupunguza maumivu, huwezi kupona ugonjwa ulionao," alisema Makalla.