WAKATI Simba wakiendelea kuwapa mikataba mipya baadhi ya wachezaji wake, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Mzambia, Clatous Chama, amesema anahitaji kulipwa Dola za Marekani 300,000 ( zaidi ya Sh. milioni 765), ili akubali kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo.
Taarifa zilizopatikana jijini, Dar es Salaam kutoka kwa Wekundu wa Msimbazi, Chama ameweka wazi anahitaji kiasi hicho cha fedha ili aendelee kuvaa jezi za rangi nyekundu na nyeupe katika mashindano mbalimbali msimu ujao.
Chanzo hicho kilisema Mzambia huyo amewaeleza mabosi wa Simba uamuzi wake huo katika kikao walichokutana naye ambao walihitaji kumaliza mchakato wa kumwongezea mkataba nyota huyo.
Taarifa zaidi zilisema Simba imegoma kumpatia Chama dau hilo kwa sababu ya umri wake na ilimpatia ofa ambayo wanaweza kumpa kiungo huyo ambaye alirejea tena Msimbazi akitokea RS Berkane ya Morocco.
"Chama amesema anataka kulipwa Dola 300,000 ili aendelee kubakia Simba, lakini viongozi wamesema hawawezi kutoa kiasi hicho kwa mchezaji wa umri wake. Wamempa ofa yao na endapo ataridhika atasaini mkataba mwingine wa miaka miwili," kilisema chanzo chetu.
Kiliongeza kuwa kama Chama ataendelea kushikilia uamuzi wa kulipwa dau hilo alilotamka, Simba itakuwa tayari kumwacha aende kujiunga na klabu nyingine.
“Wamempa ofa yao (bila kutaja kiasi), baada ya kugoma kumpa ofa aliyoileta rasmi mezani, unajua ni zaidi ya milioni 600, na wamemwambia kama ataendelea na msimamo huo, wamemwambia hawataweza kuendelea naye,” kiliongeza chanzo chetu.
Habari zaidi zinasema Simba imedhamiria kuboresha kikosi chake na hii ni kuhakikisha wanafikia malengo ya kufanya vizuri katika mashindano yote watakayoshiriki msimu ujao.
"Tutasajili kweli, usajili hautakuwa wa kitoto, kuna wachezaji ambao tayari mazungumzo yamekamilika na wengine wanaendelea nao, nyota hao baadhi wanatoka klabu za hapa ndani na wachache ni wa kutoka nje ya Tanzania.
Kwa sasa mazungumzo yanayoendelea ni baina yao na uongozi wa Ihefu kwa ajili ya kupata huduma ya kiungo, Marouf Tchakie, ambapo wametakiwa kutoa Dola za Marekani 50,000," alisema mtoa habari wetu.
Taarifa ziliongeza pia kuna mazungumzo yanaendelea ya kumpeleka Luis Miquisson katika kikosi cha Ihefu.
Nipashe lilimtafuta Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema mchakato wa usajili wa wachezaji unaendelea kwa umakini na utulivu kwa sababu wanataka kurejesha furaha kwa wanachama na mashabiki wao.
Ahmed alisema pia bado wanaendelea kujipanga kuhakikisha wanamaliza msimu ujao katika nafasi ya pili ili kujihakikishia tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
"Kuna baadhi ya wachezaji tayari wameshaongezewa mikataba na wengine wapo katika mazungumzo, atakayeridhika na ofa yao watahakikisha wanambakiza na asiyeridhika watampa baraka zote aende atakapopata kile anachokihitaji.
Pia niseme tuko katika vita vya kusaka nafasi ya pili lakini hii haitatufanya tusianze kuangalia mahitaji yetu kwa wachezaji wapya ambao tutawasajili, fedha ipo tunaenda sokoni kuangalia mahitaji yetu kwa kufuata mapendekezo ya benchi la ufundi ili kuimarisha timu yetu kuelekea msimu mpya,” alisema Ahmed.