Wakati wananchi wa Manyara wakilalamika kulipwa fidia ndogo waliyolipwa kupisha ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema malipo hayo yamezingatia taratibu zote za ulipaji fidia za kitaifa na kimataifa.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Mei 30, 2024 Mkurugenzi wa TPDC, Musa Makame amesema hakuna taratibu zilizokiukwa na kuwataka wasioridhika na fidia hiyo kufuata taratibu za kufikisha malalamiko yao.
Taratibu hizo Makame amesema zinaanzia ngazi ya kijiji, wilaya na mkoa na kama wataona hawajaridhika ofisi zao zipo wazi huku akibainisha mpaka sasa hajafikiwa na malalamiko yoyote mezani kwake.
Malalamiko ya wananchi
Wananchi hao katika malalamiko yao wamesema wamelipwa fidia mwaka jana (2023) kwa thamani ya ardhi waliofanyiwa uthamini mwaka 2016, jambo ambalo si sawa wala haki.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Manyara, Kamili Fabiano amesema hawajaridhishwa na fidia waliyolipwa na walikubali kusaini kishingo upande.
“Kwa mfano mimi kwangu heka moja wamenilipa Sh300,000 wakati thamani ya ardhi yao hiyo hadi ulipwaji wa fidia unaanza ilikuwa ni zaidi ya Sh1 milioni haki ipo wapi hapa, tunaomba Serikali itusaidie tupate haki yetu.
“Kiasi cha fedha tulicholipwa hakitoshi hata kwenda kununua eneo mahala pengine, ukizingatia wengine ardhi iliyochukuliwa ndio tulikuwa tukitegemea kulima, sasa hatutalima tena,” amesema mwananchi huyo.
Baraka Lenga kutoka Shirika la Greenfaith Tanzania, linalojishughulisha na mabadiliko ya tabianchi, amesema ni kutokana na ukiukwaji huo wa haki za binadamu, wameshaenda kuomba kusitishwa kutekelezwa kwa mradi huo katika benki za nje ya nchi na kampuni za bima zinazoudhamini.
“Mpaka sasa tayari benki 28 na kampuni 27 za bima hazitadhamini mradi huo, zilizopo katika Bara la America na Ulaya,” amesema Lenga.
Amesema ndio maana kumekuwa na ukimya katika ujenzi wake kwa kuwa wameshaenda kuweka pini huko nje, ili kuona haki inatendeka sio tu kwenye ulipaji fidia lakini pia kuhakikisha mradi unazingatia mikataba ya kimataifa ya uhifadhi wa mazingira.
Katika hili, Makame amekiri wanaharakati hao kwenda kwenye baadhi ya benki na kueleza kuwa nyingine zimeshakuja nchini kujiridhisha kwa kuwa zisingeweza kusikiliza upande mmoja.
Mradi wa bomba la mafuta unaojengwa, unatarajiwa kuendeshwa kwa ushirikiano wa kampuni za Total ya nchini Ufaransa, CNOOC ya China na Tullow ya Uingereza, kwa ubia na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Hii ni baada ya matokeo ya utafiti uliofanywa na kampuni za kimataifa za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi za Total, TULLOW na CNOOC ambao ulibaini uwepo wa mafuta ghafi takribani mapipa bilioni 6.5.
Kutokana na ugunduzi huo imebainika uwezekano wa kuvuna mapipa kati ya bilioni 1.2 hadi 1.7 na malengo yake ni kuwezesha mafuta yatakayozalishwa nchini Uganda kusambazwa katika soko la ndani na sehemu inayobaki kuuzwa nje kwenye soko la kimataifa kupitia bomba la mafuta.
Maeneo ambayo bomba litapita ni mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.