TAWA: Ukivamiwa na Mamba Mtoboe Macho...



Katika kukabiliana na Wanyamapori hususani Mamba na Kiboko, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Nchini – TAWA, Kanda Maalum ya Dar es Salaam imewapa mafunzo maalum Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Zimbwini, iliyopo Kibiti Mkoani Pwani.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Mhifadhi wa Mamlaka hiyo, Sanjo Mafuru amesema uamuazi wa kuendesha huo ni kwa ajili ya kuwaelimisha Wanafunzi wanaoishi katika jamii zinazozunguka maeneo yanayoashiria uwepo wa Wanyamapori hao.

Amesema, “ili kujihami na kujilinda na Mamba uvukapo mto au anapopita kwenye maeneo yenye mamba hakikisha una mti au fimbo yenye ncha Kali na iwapo atakuvamia mchome kwenye macho au kichwani kwa kutumia fimbo au mti huo wenye ncha Kali, iwapo huna kitu chenye ncha Kali tumia hata vidole vyako kumtoboa mamba kwenye macho yake naye atakuachia.”

Naye Afisa wa Mamlaka ya Usimamizi ya Wanyamapori TAWA, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Zawadi Malunda amewataka Wanafunzi hao kujiepusha na matembezi ya usiku, ili kujilinda na Kiboko na Mamba ambao wanaweza kuhatarisha maisha yao hasa katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha na uwepo wa mito na vijito ambavyo Wanyama hao hupendelea kuweka makazi.

Amesema, Mamba na Kiboko huwa wakali zaidi wanapokuwa wana watoto wadogo na wakati wa joto tayari kwa kupandishiwa, huku akiwataka Wanafunzi hao kujihami na makundi ya Wanyama hao wenye watoto, ikiwemo kutoa taarifa kwa TAWA ikiwa ni pamoja na kumuwahisha alijeruhiwa Hospitalini kwa matibabu.


Akitoa shukrani za mafunzo hayo, Makamu mkuu wa Shule ya Sekondari ya Zimbwini, Tabu Kanoni amesema baadhi ya Wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa wakitumia njia za kufika Shuleni kwa kuvuka mito yenye Mamba, hivyo elimu hiyo itawasaidia kuwa salama.

Naye Mwanafunzi Sekondari ya Zimbwini, Basrah Gunza ameahidi kwenda kufundisha Wanafunzi wenzao na Wazazi wao nyumbani juu ya elimu waliyoipata ili iweze kuwasaidia kuwa salama endapo watakumbana na hali hiyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad