Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu leo Ijumaa amekabidhiwa gari lake aina ya Toyota Land Cruiser V8, VXR na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma na kuwaomba Watanzania wamsaidie kulitengeneza kisha lifanye kazi za siasa. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Lissu amekabidhiwa gari hilo lililokuwa limehifadhiwa katika Kituo cha Polisi Dodoma tangu aliposhambuliwa kwa risasi tarehe 7 Septemba 2017 nyumbani kwake Area D jijini humo.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa gari hilo lililokuwa na namba za usajili T 216 DHH, amesema ‘plate’ namba za gari hilo hajui zimechukuliwa na nani ila ameangalia kwenye mfumo akakuta kuna mtu anayemiliki Land Cruiser HardTop ya rangi nyeupe ndiye anayezitumia.
Amesema gari hiyo inayotumia namba za gari lake imeonesha inadaiwa ushuru wa kuegesha magari zaidi ya Sh 10,800 maeneo ya jiji hilo la Dodoma.
“Kwa hiyo kuna mtu huko mtaani anatumia plate namba za gari yangu, naomba afanye utaratibu hizo plate namba arejeshe,” amesema.
Aidha, pia ameomba Watanzania kuendelea kumsaidia kama walivyofanya kwenye matibabu yake, vivyo hivyo wamsaidie kulitengeneza gari hilo ili lirejee kufanya kazi.
Amesema likishafikia kiwango cha mwisho kufanya kazi, atalirejeshea mlango ambao una matundu ya risasi na kulitengenezea makumbusho maalumu ili vizazi vijavyo vitambue kuwa kuna madhila waliyowahi kupitia wapinzani.
Awali akielezea matundu ya risasi yanayoonekana kwenye mlango wa upande wa abiri wa gari hilo, Lissu amesema matundu hayo ni alama za makovu aliyonayo baada ya kupigwa risasi.
Amesema risasi tatu zilimpiga kwenye nyonga, nne chini ya nyonga hali inayomfanya kushindwa kuvaa suruali vizuri na kuonekana kama anavaa mlegezo maarufu kata K.
Amesema risasi nyingine nne zilimpiga mguuni, moja bado ipo kwenye uti wa mgongo, nyingine mikononi na tumboni.
Lissu alishambuliwa na watu wasiojulikana muda mfupi baada ya kutoka kwenye mkutano wa Bunge uliokuwa unaendelea.
Alidai kuwa alishambuliwa kwa risasi 30 lakini 16 ndizo zilimpata kwenye mwili wake ambapo alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa Dodoma, siku hiyohiyo akahamishiwa Nairobi nchini Kenya kisha tarehe 6 Januari 2018 akahamishiwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi.