Tundu Lissu: Chadema Tunachezewa Mchezo Mchafu, Tunachafuliwa


Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.



CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimedai kuchafuliwa na mabango yenye picha za wanawake wa Baraza la Wanawake wa Chadema (BAWACHA) yaliyobandikwa kila wanapokwenda yanayotafsiri chama hicho na serikali hawana tatizo.

Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mwembetogwa, amesema mabango hayo makubwa yapo nchi nzima kwenye miji.

Lissu amesema mabango hayo yanatumika kuwachafua kwa wananchi kuonyesha CHADEMA na serikali hawana tatizo akifafanua kuwa, tatizo lipo ndio maana wana andamana.

“Mabango haya yanatumika kutuchafua kwa wananchi kuwa sisi na serikali hatuna tatizo, ama kuonyesha tumehongwa, ila ukweli mabango haya hata sijui kwa nini tulimualika ila haina shida, ukweli CHADEMA tunaandamana kwa kuwa, tunaona shida ipo kubwa, tunaandamana kudai Katiba mpya,” amesema.

John Heche, amesema CHADEMA inaomba Watanzania wote kuunga mkono maandamano hayo, kwa kuwa hivi sasa chama hicho kinaugulia maumivu kwa kukimbiwa na wenyeviti wa serikali za mitaa pamoja na wabunge na madiwani ambao kwa maelezo yake, walinunuliwa na serikali ya CCM.

Amedai kuwa, serikali ya awamu ya tano iliacha maumivu makubwa ndani ya CHADEMA kwa kuwanunua wenyeviti na madiwani wake.

Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Iringa Mjini, Frank Nyalusi, amesema wamezuiwa kutumia njia ya Kihesa na kuruhusiwa njia moja pekee ya Mlandege hadi viwanja vya Mwembetogwa.

“Maandamano haya ni mwanzo wa maandamano na mkutano mkubwa wa CHADEMA Mkoa wa Iringa ambao utafanyika katika viwanja Mwembetogwa na kuwa maandalizi ya maandamano hayo ni ya siku moja pekee, ndiyo sababu ya watu kutokuwa wengi, lakini jambo kubwa ni kufikisha ujumbe serikalini kuhusu hitaji la msingi la kudai Katiba mpya,” amesema.

Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa, amesema sababu kubwa ya kuandamana ni kudai Katiba mpya pamoja na kuiambia serikali kuhusu ugumu wa maisha kwa Watanzania.

“Kuna baadhi ya watu wanabeza maandamano ya CHADEMA kwa kuona hayawahusu, ila nao ni miongoni mwa watu wanaokosa haki kutokana na katiba mbovu na pia, wanalia ugumu wa maisha kwa kuendelea kushuhudia gharama za bidhaa zikiendelea kupaa siku hadi siku.

“Naomba kuwaambia Watanzania, maandamano haya si ya CHADEMA pekee, ni ya watanzania wote, maana Katiba mpya si ya CHADEMA ni ya taifa zima,” amesema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad