Duru za ndani kabisa, zinasema Simba imenasa antena zake Jangwani ambako lolote linaweza kutokea kati yao na Kennedy Musonda wa Yanga.
Habari zinasema kwamba Yanga huenda ikaachana na Musonda muda wowote baada ya kumalizana na gwaride la ubingwa ili nafasi yake wanunue chuma kingine wanachodai kina takwimu za kuvutia.
Kumbuka Musonda ambaye ni raia wa Zambia, ndiye aliyefungua njia ya zile bao 5-1 dhidi ya Simba lakini wekundu hao wamekaa mkao wa kula wakisubiri maamuzi hayo tu ili wamsombe fasta.
Hesabu za kwanza kwa Yanga ni kwamba ili kuingiza jina la mshambuliaji wao mpya wanayeendelea na mchakato wake Prince Dube inatakiwa kumchomoa mtu mmoja ndani ya wachezaji wake 12 wa kigeni.
Na Yanga inaona Musonda mwenye mabao matano kwenye ligi bado hajafanya makubwa. Inapiga hesabu za kumuacha mwisho wa msimu huu ili nafasi yake itumiwe na Dube huku pia ikipanga kuingiza winga mmoja wa kigeni au kiungo mshambuliaji ambapo hapo anayechomolewa mwingine ni Mahalatse Makudubela 'Skudu'.
Simba kwenye vyanzo vyao vya usajili, wamenasa za ndaani kuhusu staa huyo na wanaona anawafaa kwenye kikosi chao kama Yanga itafanya maamuzi hayo ya kumuacha.
Msimbazi wanataka kumchukua Musonda haraka ili akaongoze safu yao ya ushambuliaji mara tu Yanga itakapompa Thank you mshambuliaji huyo anayejua kufunga kwa kichwa na mwenye uzoefu mkubwa na Ligi za Afrika.
"Tusubiri maamuzi yao ya mwisho, hapa Simba atacheza tofauti na presha iliyopo pale Yanga ambayo haimpi muda wa kutosha wa kucheza, "alisema bosi mmoja kwenye usajili wa Simba.
"Unajua Bora ya mtu ambaye mmeshamuona anayejua mazingira ya kawaida, tunafahamu tukimbakisha Chama (Clatous) tunaweza kumpata kirahisi zaidi.”
Mkataba wa Musonda na Yanga unafikia tamati mwisho wa msimu huu na Mwanaspoti linajua hakuna mazungumzo yoyote ya kina juu ya kumpa mkataba mpya na hata yeye ameshaanza kuhisi kwa mujibu wa watu wa karibu yake.
Musonda alikuwa mfungaji wa bao la kwanza la Yanga ilipoichapa Simba kwa mabao 5-1 akifunga kwa kichwa bao ambalo lilifungulia kipigo hicho kwa wekundu yaoNovemba 5,2023. Mchezaji huyo alitua Yanga miaka miwili iliyopita baada ya Mabingwa hao wa Tanzania kuipiga bao TP Mazembe ambao walikuwa wakimfukuzia.
Tetesi za usajili wa klabu kubwa za Ligi Kuu Bara zimeanza kushika kasi wakati Yanga ikiwa imesalia sikuchache kukabidhiwa rasmi kombe lao Jijini Dar es Salaam.