Kama wewe ni mnywaji wa pombe zinazotengenezwa kwa ngano au pombe kali, soma hapa kwa makini.
Wataalamu wa afya wameeleza uwepo wa athari hasi kwa watu wenye tabia ya kunywa pombe kabla ya kula.
Wanasema hiyo huchangia huchangia mnywaji huyo kula chakula kidogo kuliko mahitaji ya mwili na wakati huo huo huwa anaharibu kuta za utumbo.
Mtaalamu wa Lishe na Meneja Mradi wa Afya ya Mama na Mtoto kutoka Shirika la World Vision, Dk Daudi Gambo ameyasema hayo alipofanya mahojiano na Mwananchi.
Amesema hata hivyo athari zake hutegemeana na aina ya pombe anayotumia mnywaji, huku akisisitiza kuwa zipo tofauti kati ya pombe kali na zile zilizotengenezwa kwa ngano.
“Pombe zenye ngano kama bia aina zote, yule mtu anakuwa amechukua kaloris nyingi kutoka kwenye kabohaidreti, kwa maana hiyo anaweza kujikuta ameshiba na ile hamu ya kula chakula ikapungua kwa sababu nguvu tayari anazo, hivyo atapunguza nafasi ya yeye kula kitu kingine,” anasema.
Dk Gambo anasema mnywaji atakuwa amechukua kaloris, hivyo vitamin, protini na madini mengine, vyote hivyo anajikuta amevikosa na wengi akishashiba anaweza asile tena.
Anasema mtu huyo sasa anakuwa hajapata virutubisho vyote vinavyopatikana kwenye makundi sita ya vyakula.
Anasema anayekunywa bia anakuwa amechukua sehemu moja na ameacha virutubisho kutoka makundi mengine na akishakunywa pombe, hamu ya chakula inapungua au inaisha kabisa.
Akizungumzia pombe kali, Dk Gambo anasema zinaathiri vimeng’enya chakula ‘enzymes’ na ikiathiri utengenezaji wa vimeng’enya chakula inaua wale wadudu waliopo kwenye utumbo.
“Pombe kali huingilia utengenezaji wa vitamin B zilizo muhimu kwa ajili ya wadudu wa tumboni na wale wanaohusika katika kumeng’enya chakula, hivyo kwa sababu ule mmeng’enyo wa utumbo unakuwa umepungua, ndiyo maana wanaotumia pombe kali wanapata shida ikiwamo ya ugonjwa wa utapiamlo.
“Endapo amezidisha pombe, wale wadudu rafiki wanaosaidia mmeng’enyo wa chakula wanaotakiwa kutengeneza vitamin B kwenye utumbo mdogo, wanapotea na ile simenti ya kwenye utumbo nayo inapata shida,” anasema.
Akizungumza na Mwananchi, Mtaalamu mwingine wa afya ya jamii na aliyekuwa Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya, Dk Ali Mzige anasema ili watu waendelee kuwa na afya bora, ni vizuri wale chakula saa mbili hadi tatu kabla ya kulala ili kutoa nafasi ya umeng’enyaji, pia uzungukaji wa damu mwilini, hususan kwenye ubongo, figo na moyo.
“Mtu anapokula chakula baada ya saa mbili usiku ni rahisi kurundika chakula katika eneo lake na kushindwa kutoa nafasi kwa mzunguko wa damu kwenda taratibu na wakati mwingine kusinzia,” anasema Dk Mzige.
Akitoa mfano, anasema kuna mtu mmoja alipoandaa sherehe ya binti yake, walipotoka kanisani walifikia kula muda huo ilikuwa Saa 12 jioni na baada ya hapo utaratibu mwingine uliendelea.
“Inawezekana tamaduni za nje zilikuwa zimemkaa, hivyo alipofika huku akaamua kuendelea nazo na watu walimsifu kwa sababu baada ya sherehe, waalikwa walikuwa na nafasi ya kufanya vitu vingine bila kuathiri afya zao ambazo zingesababishwa na chakula,” anasema.
Dk Mzige anasema haipaswi mtu kunywa pombe kabla ya kula kwenye sherehe na kula chakula kingi kupita kiasi kwa usiku, kwa sababu unywaji wa pombe unakwenda kuchukua nafasi ya chakula na kusababisha kuwa cha ziada.
Anasema inapotokea kwenye sherehe wameanza kula, haitakiwi kula kila chakula kilichopo, bali inatakiwa kuchagua vyakula vichache ambavyo uwezekano wa kumaliza upo na si kula ili mradu mtu avimbiwe.
“Katika masuala ya ulaji mtu anatakiwa kula kidogo, siyo mtu anachanganya kipande cha kuku na samaki, wali, ndizi, pilau na vingine kwa wakati mmoja, kinachotakiwa ni kuchagua kimojawapo,” anasema Dk Mzige.
Hata hivyo, anasema cha kuzingatiwa kwenye sherehe wakati wa ulaji ni kutumia mboga za majani na matunda, kwa sababu inasaidia kupunguza saratani na tafiti zimefanyika takribani watu milioni 2 wanakufa kila mwaka kwa kutokula matunda na mboga za majani.
Mhudumu wa chakula katika sherehe, Mwatanga Madoda anasema ulaji wa chakula unacheleweshwa na wenye shughuli kwa kuingia ukumbini saa tatu tofauti na muda uliopangwa kwenye ratiba.
Utamaduni ukoje?
Kuna utamaduni uliokaririwa na wengi kuwa chakula cha kwenye sherehe kinaliwa kuanzia saa tatu usiku. Jambo hilo linahatarisha afya kwa kupata magonjwa yasiyoambukiza na kuleta usingizi, huku kula na kulala haishauriwi kiafya.
Kwa mujibu wa wataalamu, utaratibu wa chakula kinapaswa kiliwe mwisho saa mbili usiku ili kuruhusu umeng’enywaji wake ufanyike kwa wepesi hadi itakapofika muda wa kulala.