Upendo Peneza Arusha Kombora Chadema, Wenyewe wajibu

 

Upendo Peneza Arusha Kombora Chadema, Wenyewe wajibu

Aliyewahi kuwa Mbunge wa Viti Maalumu wa Chadema, Upendo Peneza amekishutumu chama chake cha zamani, akidai kilikuwa kikiwachangisha fedha wabunge, lakini matumizi yake hayakuwahi kuwekwa wazi.


Peneza ambaye Januari 22 mwaka huu alijiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyesema hayo jana katika mahojiano maalumu na Radio ya Clouds FM. Alisema Chadema imekuwa ikiwadanganya wananchi.


Hata hivyo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema ameyapuuza madai hayo akisema ni propaganda za CCM.


“Kwanza Upendo Peneza ameshaondoka Chadema, ni kada wa CCM ajikite kujenga chama chake kipya.”


“Pili yeye ndiye anapaswa kuishukuru Chadema, kwa sababu alitoka shuleni, hakuwahi kuwa na ajira yoyote, chama kikampa fursa ya kuwa mbunge, kwa hiyo anapaswa kukishukuru chama,” alisema Mrema.


Peneza alikuwa mbunge wa viti maalumu kupitia Chadema, mwaka 2015-2020.


Madai ya fedha za wabunge


Akizungumzia madai ya wabunge kuchangishwa fedha, Peneza amedai Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli alianzisha uchunguzi wa fedha walichokuwa wakichangishwa wabunge kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.


“Sisi tulivyokuwa bungeni, unajua Magufuli alianzisha uchunguzi kwa Chadema, Tulikuwa tunakatwa Sh1.6 milioni kila mwezi wabunge wa viti maalumu, wabunge wa majimbo walikuwa wanakatwa Sh500,000.


“Maana yake ni kwamba hizo hela tulivyokuwa tunaambiwa kwamba zitasaidia kipindi cha uchaguzi mwaka 2020, watu wawe na uwezo wa kufanya kampeni,” amesema.


Upendo Peneza alipokuwa mbunge viti maalumu kupitia Chadema.


Amesema waliitwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kuhojiwa kuhusu hizo fedha na yeye alisema wanakatwa kwa mujibu wa katiba ya chama chao.


“Nikasema hizo hela walishatutangazia zitatumika wakati wa uchaguzi wa 2020 kusaidia wagombea,” amesema.


Hata hivyo, alisema kinyume na matarajio hawakusaidiwa katika uchaguzi huo.


“Kamuulize mwana Chadema yoyote ni nani aliyesaidiwa? Binafsi mimi sikusaidiwa na watu katika mkoa wetu hawakusaidiwa. Sasa tumemaliza uchaguzi tukasema tumekataa ruzuku, maisha tuliyoishi tangu tulivyokataa ruzuku mpaka ilipokubaliwa Mungu mwenyewe anajua.”


“Kwa hiyo hela ingekuwepo mahali fulani labda ingetusaidia kipindi hicho kwenye kesi na kumalizia, hakuna tunarudi tena kwa wananchi watuchangie,” amesema.


Hata hivyo, akijibu suala hilo, Mrema alikiri wabunge na madiwani wa chama hicho wamekuwa wakichangishwa kwa mujibu wa Katiba na kanuni za chama hicho.


“Suala la wabunge kuchangishwa liko kwenye kanuni zinazosimamia wabunge na madiwani nao wanachama kwa mujibu wa kanuni zetu na katiba yetu.


“Ni fedha kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli mbalimbali za chama, sio kibubu cha kuwawekeza fedha wabunge kwa ajili ya uchaguzi.


“Ni kama wanavyochangia wanachama wengine wa kawaida, lakini wao kwa sababu wana fursa chama kimewapa ubunge, wanachangia kwa ajili ya kuendesha chama na iko kwenye kanuni.


“Wanaopata fursa kuwa kwenye vikao wanasomewa mapato na matumizi na taarifa hizo zinakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa sababu zinakuwa sehemu ya mapato ya chama,” amesema.


Kuhusu uchunguzi uliofanywa na Takukuru, Mrema amesema kuna taarifa zilizushwa na baadhi ya waliokuwa wabunge walisema fedha zinatumika vibaya.


“Takukuru ikachunguza ikaona ni uongo ikaachana na huo uchunguzi na taarifa ikawekwa hadharani. Hata mimi Takukuru iliniita nikawapa maelezo, kwamba hiyo michango ni kwa mujibu wa kanuni za chama na nikawapa Katiba ya chama,” alisema.


Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamudi alipoulizwa juu ya kinachoendelea kuhusu uchunguzi huo amesema: “2020 ni almost miaka minne iliyopita, lazima niangalie kumbukumbu za ofisi."


Kwa mujibu wa katiba ya Chadema mbunge wa jimbo ana majukumu matatu; kuwatumikia wapiga kura wake, kujenga na kuimarisha mtandao wa chama katika jimbo lake na kusaidia chama kukua na kuimarika nchi nzima.


“Kwa sababu ya majukumu hayo, Mbunge wa Jimbo atachangia Chama kila mwezi asilimia 10 ya posho za kibunge,” inaeleza katiba.


Kwa mbunge wa viti maalum inaeleza: “Jimbo la wabunge hawa ni chama, na jukumu lao la msingi ni kusaidia chama ili kikue na kuimarika. Wabunge wa Viti Maalum watachangia chama kila mwezi asilimia 30 ya posho za kibunge.”


Wabunge 19


Kuhusu wabunge 19 waliofukuzwa Chadema akiwemo Halima Mdee, Peneza amesema bado hakubaliani na uhalali wao, lakini anashangaa bado Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anakuwa na ukaribu nao.


Alitoa mfano wa baadhi ya wabunge hao akiwamo Mdee na Esther Bulaya kuhudhuria harambee ya uchangiaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), usharika wa Nshara Machame mkoani Kilimanjaro Desemba 31, 2023.


“Halafu baada ya muda unasikia mwenyekiti wako wa chama anakula na kugonga cheers na aliyefukuzwa uanachama na kamati kuu.


“Mwenyekiti anagonga naye cheers kwa sababu zozote zingine ambazo zipo, halafu unataka watu waamini kwamba kwa kweli mambo yanavyoenda ndivyo yalivyo,” amehoji Peneza.


“Kuna kukutana kwa sababu tumekutana na kukutana na kusherehekea kwa sababu mimi nimepanga tusherehekee kwa sababu mimi nimepanga tusherehekee pamoja. Hawa watu, taasisi unayoiongoza ambayo wewe ni mwenyekiti wa chama wameita ni haramu,” amesema.


Hata hivyo, akijibhu hoja hiyo, Mrema amesema Halima na Esther walihudhuria kama washarika wenginje.


“Kama Rais Samia Suluhu Hassan alichangia ujenzi wa kanisa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alichangia kwa sababu ni ujenzi wa kanisa, hivi wao wakichangia kunatia doa gani chama?


“Tusiwafanye watu wengine wana dhambi kuliko wengine, hatujui waliendaje kuchangia, walikuwa Watanzania kama wengine waliokuja kuchangia. Mbona tunakutana nao kwenye misiba, mbona haileti doa? Mnataka tuzuie watu hata kutoa sadaka kujenga nyumba za kumwabudia Mungu,” amehoji Mrema.


Peneza aliendelea kunyooshea kidole kuhusu mwenendo wa kesi ya wabunge hao ambao walishinda akidai chama hakikutoa taarifa za kutosha.


“Hatujui kinachoendelea mahakamani na nguvu ambayo Chadema ilikuwa imewekwa mahakamani na hata wanasheria wenyewe leo yupo huyo kesho huyu.


“Nakumbuka niliwahi kumwambia katibu mkuu kwamba hii kesi tunaweza tukashindwa, lakini kuonyesha seriousness na wanachama wetu ni muhimu, kwa hiyo kuwe utaratibu wa namna hii kesi inavyoendeshwa,” amesema.


Hata hivyo, kwa nyakati tofauti viongozi wa Chadema akiwemo Katibu Mkuu, John Mnyika walikwisha kueleza wamemalizana na kesi hiyo, wakiwataka wanachama wao kumpigia simu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson na kumweleza kuwa wabunge hao sio halali.


Uchaguzi Bavicha


Akieleza jinsi alivyojiunga na Chadema mwaka 2009 na hatimaye kugombea uenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) mwaka 2014, Peneza amedai hakutendewa haki katika uchaguzi huo.


Amesema katika uchaguzi huo uliokuwa na wagombea 13 wa uenyekiti ulikuwa mgumu na alijiandaa vya kutosha.


“Wakati uchaguzi unaendelea, mwenyekiti wa chama mheshimiwa Mbowe akaja kutoa hotuba katikati ya uchaguzi, yaani wagombea wameshajieleza. Nikaomba Yesu wangu nisaidie.


“Niliongoza kwenye uchaguzi na nilipata kura zaidi ya 60 na aliyenifuata alikuwa na 61 na mwingine kidogo kidogo. Sikufikisha asilimia 50, ikabidi turudie uchaguzi watu wawili, ni katiba ya chama,” amesema. Walirudia yeye (Peneza) na Patrobas Katambi.


Amesema baada ya kutangazwa kurudiwa kwa uchaguzi, utaratibu haukuzingatiwa,


“Uchaguzi umerudia, wajumbe wengine wameondoka, msimamizi hataki kuhesabu idadi ya wapiga kura, kwa hiyo inabidi uhesabu waliobaki.


“Kingine, ni karatasi za kupigia kura, wa sababu ilikuwa mara ya kwanza kupiga kura, hapakuwa na karatasi za kupiga kura kama zilizotumika mwanzo.


“Karatasi zilizokuwepo nimeandikwa Patrobas na Upendo na zinavyogawanywa. Halafu watu wangu wakizunguka, wanaambiwa kaa chini, wengine wakizunguka, sawa,” amesema.


Hata hivyo, amesema hakukata rufaa bali alitoa malalamiko yake kwa mdomo.


Hata hivyo, Novemba 21, 217 Katambi alitimka Chadema na kujiunga na CCM katika moja ya vikao vya chama hicho vilivyofanyikia Ikulu ya Dar es Salaam na kuongozwa na mwenyekiti wake, Magufuli.


Akijibu suala hilo, Mrema amesema, Peneza alitakiwa kukata rufaa.


“Sasa mambo ya 2014 leo miaka 10 baadaye anakuja kulalamika? Amekosa hoja. Hakuwahi kulalamika, hakuwahi kukata rufaa popote, sasa leo anapokuja kuyazungumza ni mambo ya kuchekesha,” amesema.


Katika hatua nyingine, Peneza amewashukuru baadhi ya viongozi akiwamo Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akisema ni miongoni mwa viongozi waliomjenga, huku pia akimtaja marehemu Alphonce Mawazo aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, akisema alimjenga kisiasa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad