Vanessa Mdee, moja kati ya wasanii wakubwa wa Tanzania waliobobea kwa miziki yao ya Bongo Fleva miaka ya nyuma amefunguka makubwa aliyowahi kuyapitia enzi anahangaika kutafuta riziki kupitia muziki.
Mdee ambaye alikuwa anazungumza kwenye podkasti ya pamoja na mumwe, Rotimi nchini Marekani alisimulia jinsi alikuja kufahamu upande mweusi wa tasnia ya Bongo Fleva kwamba kuna baadhi ya wasanii wanatoboa kwa kutumia uchawi na ushirikina.
Alisimulia kisa chake ambapo wakati mmoja aliwahi kumfuata meneja mmoja mkubwa na kutaka kufanya kazi chini yake lakini meneja huyo bila kuficha alimuelezea wazi kwamba ili kufanya kazi naye, sharti ajue kwamba katika kampuni yake wanatumia ushirikina ili mambo ya wasanii wao yatiki.
“Niliwahi kumfikia mmoja kati ya meneja maarufu sana Tanzania kipindi hicho, nikamwambia ningependa kuwa chini ya uongozi wake na aliniambia bila kupepesa jicho kwamba kana unakuja chini ya uongozi wetu, inakupasa kuelewa kwamba sisi tunatumia ushirikina, uchawi,” Vanessa Mdee alisimulia.
Msanii huyo alisema kwamba meneja huyo alimwambia kila kabla msanii wao hajaachia muziki, ni sharti waupitishe kwa taratibu za kishirikina.
Kwa kustaajabu, Mdee alisema kwamba alijivuta nyuma na kujikunyata akimtaka meneja huyo kufahamu kuwa yeye alikuwa anamuogopa Mungu.
“Nilimuuliza, ‘unajua ninaamini katika Mungu?’ akanijibu kwamba anafahamu hivyo lakini akasema kuwa hiyo ilikuwa ni kati ya vitu ambavyo wanafanya. Nilikataa matakwa yao na nikaondoka kutoka kwa mkutano wao na sikuwai kurudi kufuatilia mazungumzo hayo tena,” alisema.