Serikali imesema ujenzi wa viwanja vipya vya michezo kwa ajili ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), unatarajiwa kukamilika mwakani ili kupisha ukaguzi wa kikanuni.
Tanzania, Kenya na Uganda zitaandaa Fainali za Mataifa Afrika mwaka 2027 ikiwa ni mara ya kwanza nchi hizo zinafanya hivyo.
Hayo yamesemwa leo Jumanne (Mei 21) na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Chakechake, Ramadhan Suleiman Ramadhan.
Mbunge huyo amehoji ni lini viwanja vipya ambavyo Serikali inatarajia kujenga kwa ajili ya matayarisho ya Afcon vitakamilika.
Akijibu swali hilo, Mwijuma amesema kwa mujibu wa ratiba na mahitaji ya viwanja hivyo vinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka ujao.
Amesema wanafanya hivyo ikiwa ni tayari kwa ajili ya ukaguzi wa kikanuni wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ambao utafanyika mwaka 2025 kwa ajili ya mashindano ya AFCON 2027.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest amesema michezo mara nyingi huendana na mazoezi na wakati mwingine hupelekea majeruhi na kutaka kufahamu serikali imejiandaa vipi.
“Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha watu wote wanaofanya mazoezi wanaweze kupata bima ya afya,” amesema Anatropia.
Akijibu swali hilo, Mwijuma amesema Serikali imekuwa ikitilia mkazo mashindano yote ya kitaalamu kwa kuwawekea bima za afya wachezaji.
Amesema kuwa hata kwa wachezaji wa timu ya Taifa, wamekuwa wakiwawekea bima ya afya ili wakipata madhara ya kudumu Serikali iweze kuwatibia kwa kutumia bima hizo.
Baada ya majibu hayo, Naibu Spika wa Bunge Mussa Zungu alisema wachezaji wote wa Simba wanabima ya afya na kuwataka klabu nyingine kuiga.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Chumbuni Ussi Salum Pendeza, amehoji ni lini Serikali itaamua kuwekeza kwa nguvu zote katika viwanja, walimu na mawakala wa michezo mbalimbali inayoonekana kuleta tija kwa Taifa.
Akijibu swali hilo, Mwijuma amesema Serikali inatekeleza ujenzi wa viwanja vya mpira wa miguu Arusha, Dodoma, Zanzibar (Fumba), Ilemela Jijini Mwanza pamoja na akademia na hosteli katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.
“Vilevile, Serikali ipo katika ukarabati wa viwanja vya Benjamin Mkapa, Uhuru, Amaan na Gombani vya Zanzibar kwa ajili ya maandalizi ya CHAN 2023 na AFCON 2027,”amesema.
Amesema katika kuhakikisha kuwa kuna walimu wa kutosha wa michezo, Serikali imekuwa ikiongeza udahili katika vyuo vinavyotoa mafunzo ya walimu wa michezo hususani Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Amesema hadi kufikia mwaka 2023/24, jumla ya wanafunzi 812 wamehitimu katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.
Amesema Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa imeendelea kusajili mawakala wa michezo mbalimbali ambapo jumla ya mawakala 233, walisajiliwa kuanzia mwaka 2018 hadi Desemba, 2023.