WANAFUNZI watatu wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya John Paul II, Kahama mkoani Shinyanga, wamepoteza maisha kwa kukosa hewa baada ya kuingia kwenye ghala la mahindi shuleni hapo.
Vifo hivyo vimeripotiwa ikiwa ni mwaka mmoja tangu kutokea kwa tukio la aina hiyo Mei 12, 2023 katika Shule ya Sekondari Kisomachi iliyoko Kata ya Vunjo Mashariki, Moshi mkoani Kilimanjaro.
Kutokana na vifo hivyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknlolojia, Prof. Adolf Mkenda, ametoa angalizo mahususi kwa walimu kuhusu usalama wa wanafunzi shuleni.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi (ACP) Kenedy Mgani, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo katika shule hiyo iliyoko Mtaa wa Mbulu, Kata ya Mhongolo wilayani Kahama, alipozungumza na waandishi wa habari jana.
Alisema vifo hivyo vilitokea Mei Mosi, mwaka huu, saa 5:00 asubuhi shuleni hapo walipoingia ndani ya ghala na baadaye kuzirai na kufariki dunia hatimaye kupelekwa katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama.
Kamanda Mgani aliwataja wanafunzi hao kuwa ni Abdul Ibrahim (17) mkazi wa Mwanza, Jonathan Mdabila (17) mkazi wa Nzega mkoani Tabora na Paul Emmanuel (18) mkazi wa Kahama.
Alisema siku ya tukio, wanafunzi hao waliingizwa kwenye ghala, maarufu kama ‘vihenge’, lililojenga na mabati magumu kwa lengo la kutoa mahindi ya chakula cha siku hiyo.
Kamanda Mgani alisema walikuwa wanafunzi sita ambao waliongozana na mwalimu wa zamu, Moris Leo (54) kwenda kwenye ghala hilo na baada ya mahindi kushindwa kutoka kupitia tundu la chini ya tangi hilo, mwalimu huyo aliwataka wanafunzi kupanda juu na kuingia ndani kuyasukuma.
Alisema baada ya kutoa agizo hilo, mwalimu huyo aliondoka eneo hilo na kwenda ofisini kupata chai, huku wanafunzi watatu kati ya sita, wakiingia ndani ya tangi hilo kwa kutumia ngazi.
Baada ya dakika kati ya 15 hadi 30, waliokuwa nje hawakuona mahindi yakitoka huku waliokuwa ndani wakiwa kimya, ndipo walipotoa taarifa kwa uongozi wa shule.
Alisema walimu walifika na kuangalia kinachoendelea na haraka wakachukua uamuzi wa kuvunja tangi hilo kwa shoka na kupata mpenyo wa kuwatoa na kuwapeleka katika zahanati ya jirani na shule na baadaye Hospitali ya Manispaa ya Kahama, ambako walipoteza maisha.
Mpaka sasa, alisema wanamshikilia mwalimu Leo kwa mahojiano zaidi na upelelezi unaendelea kuhusu tukio hilo.
MKASA ULE ULE
Mei, mwaka jana, kulitokea tukio kama hilo katika Shule ya Sekondari Kisomachi ambako wanafunzi wawili wa kidato cha mne walipoteza maisha katika mkasa unaofanana na huo. Nao walipanda katika tangi la kuhifadhia maharage.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, siku hiyo ilisema tukio hilo lilitokea saa 10:00 jioni wakati wanafunzi hao walipoingia ndani ya tangi linalotumika kuhifadhia maharage kwa lengo la kuyatoa baada ya sehemu ya chini inayotumika kuziba.
Kamanda maigwa aliwataja wanafunzi waliofariki dunia ni Edson Mosha (17) na Godwin John (17).
MKENDA ATOA ANGALIZO
Baada ya kuripotiwa kwa tukio la Kahama, Nipashe ilimtafuta Waziri Mkenda ambaye alisema usalama wa watoto wote ni jambo moja la msingi na muhimu shuleni.
“Hatua zozote zinazochukuliwa hazina maana kama zitahatarisha usalama wao. Tuna jukumu la kuhakikisha tunaendesha shughuli na kulinda watoto tunaokabidhiwa shuleni. Tunafuatilia matukio yote mawili,” alisema Prof. Mkenda.
Kimsingi wanafunzi waliofariki dunia ni watoto. Sheria ya Ulinzi wa Mtoto ya mwaka 2009, mbali na mambo mengine, inaelekeza watoto kupewa haki ikiwamo ulinzi wa usalama wao.
IMEANDALIWA na Shaban Njia (KAHAMA) na Romana Mallya (DAR)