Mechi mbili za hatua ya robo fainali kati ya Yanga na Mamelodi zimetosha kumpa mkataba wa mwaka mmoja kiungo Jonas Mkude kuendelea kusalia Jangwani.
Mkude alisajiliwa na Yanga kama mchezaji huru mwanzoni mwa msimu huu baada ya mkongwe huyo kutemwa na Simba aliyokuwa ameitumikia kwa takribani miaka 13.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kimeliambia Mwanaspoti kuwa Mkude na Abubakar Salum 'Sure Boy' wataendelea kubaki Jangwani huku Zawadi Mauya akitajwa kumpisha Yusuf Kagoma endapo dili lake litakwenda sawa.
Mkude ambaye alikuwa akishirikiana na Mudathir Yahya, kwenye mechi hizo aliifanya Yanga kuwa na utulivu huku akirahisha mashambulizi kutokana na kuachia kwake mpira kwa haraka kwa pasi fupifupi na ndefu ilipohitajika.
Yanga walimpa Mkude mkataba wa mwaka mmoja kwa kuwa hawakuwa na uhakika kama angeweza kuwa na kiwango bora hasa ikikumbukwa kuwa hakuwa akipata nafasi ndani ya Simba kwa muda mrefu katika kipindi cha mwaka wake wa mwisho ndani ya timu hiyo.
Uwezo alionesha katika mechi dhidi ya Mamelodi Sundowns ya nchini Afrika Kusini, nyumbani na ugenini viongozi wa Yanga wameamua kumuongezea kandarasi nyingine, Mwanaspoti limezinasa habari hizo.
"Ni kweli Mkude kaongezwa mkataba ataendelea kubaki Jangwani kwa mwaka mmoja hii ni baada ya benchi la ufundi kupitisha jina lake kutokana na kuridhishwa na uwezo wake kila anapopata nafasi ya kucheza," kilisema chanzo hicho.
Wakati Mkude akiwa na uhakika wa kusalia ndani ya timu hiyo inaelezwa kiungo Zawadi Mauya ambaye mkataba wake pia umamalizika mwisho wa msimu mabosi wa timu hiyo bado hawajafan]yanae mazungumzo ya kumuongeza mkataba msimu ukiisha anasepa.
Endapo Yanga itakamilisha dili la kiungo wa Ihefu FC, Yusuf Kagoma, basi Mauya atatakiwa kumpisha mchezaji huyo ambaye anatajwa kuungana na timu hiyo msimu ujao ili kuongeza nguvu katika eneo hilo ambalo kwa sasa Khalid Aucho amekuwa akifanya vizuri.