Ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, katika wilaya sita za mkoa huo kwa ajili ya kukagua maendeleo na kutatua kero za wananchi, imeibua madudu ikiwamo viashiria vya upigaji fedha katika miradi.
Kutokana na kuwapo kwa madudu hayo, ameagiza kuundwa timu ya kuchunguza miradi yote iliyoko wilayani Longido, ikiwamo Shule ya Sekondari ya Wasichana Samia.
Makonda alitoa maagizo hayo juzi jioni wakati akizungumza na wananchi Namanga, mpakani mwa Tanzania na Kenya akiwa kwenye ziara yake ya wilaya sita za mkoa wa Arusha kukagua miradi na kutatua kero za wananchi.
Makonda alisema amejulishwa kupima udongo kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo kumegharimu Sh. milioni 10, deni la maji Sh. milioni tano na kuingiza umeme zimetumika Sh milioni 1.6.
“Tumepewa hela na Rais Samia Suluhu Hassan, tunataka kupata matumizi yake, yaani kupima udongo tu mnatumia Sh. milioni 10 katika ujenzi wa shule na ushuru wa gari la halmashauri walikuwa wanalipia kwa maelekezo ya mkurugenzi Sh. milioni tatu. Lilikuwa linafanya kazi gani, yaani gari lilitumika kusombea mchanga diwani naomba usogee karibu,” alisema Makonda.
Makonda alimtaka mkuu anayesimamia ujenzi wa shule hiyo, Daniel Temu, kueleza nyongeza ya fedha ambapo alisema kupima ubora wa zege Sh. 400,000 na gharama za LUKU Sh. milioni mbili
“Hiyo Sh, milioni mbili kwa muda gani? Kwa hiyo ujenzi ulivyokamilika mkaweka LUKU. Ujenzi ulianza Septemba 30, mwaka jana na kutoka Septemba hadi Machi, mwaka huu, ni miezi sita kwa hiyo mmetumia umeme wa Sh, milioni 2.5. Je, kuna watu wanaishi pale shuleni?” alihoji Makonda.
Mkuu huyo wa mkoa alimwita Diwani wa Orbomba ambaye alisema lori la halmashauri linawadai Sh, milioni 30 na fedha iliyolipwa ni Sh milioni tatu, hivyo bado wanadai Sh milioni 27.
Alisema ujenzi wa shule hiyo wananchi hawajashirikishwa hata yeye na mwenyekiti hawakuwa wanajua chochote.
“Hata mafundi wamepatikana nje ya utaratibu. Mafundi wote wa Longido hakuna hata mmoja aliyepata kazi. Sisi hawatupi taarifa hata nikidai taarifa napewa nusu nusu,” alisema diwani huyo.
Baada ya maelezo hayo, Makonda alisema: “Sasa mwalimu, diwani amesema gari la halmshauri lilitakiwa kulipwa Sh. milioni 30 lakini mkalipa Sh, milioni tatu ina maana nikipiga hesabu ongezeko la fedha ni Sh milioni 40. Hizo ndizo zinakupa uhalali wa kuomba Sh. milioni 460?” alihoji Makonda.
Awali, Temu alisema walipatiwa Sh. bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa shule ya wasichana ya mkoa wa Arusha na ilitakiwa kukamilika Machi, mwaka huu. Majengo yote yamekamilika isipokuwa bwalo la chakula ambalo zinahitajika Sh milioni 460 ili kukamilika.
Makonda alisema mradi huo wa shule una sintofahamu nyingi ikiwamo mhandisi kutaka nyongeza ya fedha zaidi ya mara mbili na kamati ilikataa kutoa fedha. Alisema nyongeza ya fedha hizo ambazo mhandisi wa ujenzi amekuwa akizitaka ni ukiukaji wa taratibu za ununuzi.
“Mkuu wa shule ametuambia hapa mara mbili kuwa mara ya kwanza walitaka nyongeza ya Sh, milioni 29 maana yake mara ya pili ikawa wanataka tena Sh. milioni 37. Ukijumlisha unapata Sh. milioni 66. Inawezekana tukawa tunaongezea hela kidogo kidogo. Ulishawahi kuona mtu mtaalamu wa kuua chura huwezi kuua chura ukimwekea maji ya moto kwa mpigo anaruka?
“Wataalamu waliona wakiongeza zaidi ya asilimia 15 watabanwa na sheria ya ununuzi inayokataa inataka utangaze tenda upya. Wakagundua hii staili ya kumwekea chura maji ya moto wataruka kwa wakati mmoja wakaona wapige Sh, milioni 27, Sh. milioni 29 na Sh. milioni 37 ukijumlisha bado kuna changamoto,” alisema. .
Makonda alimwagiza Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) kuunda timu ya uchunguzi kwenye miradi yote ya Longido ili apate majibu sahihi.
“Sitaki aje kiongozi wangu nikose majibu. Hivi ninavyowabana na mimi nina mabosi wangu wa kunibana, wacha niwapelekee moto kabla sijapigwa moto. Naomba nisaidiwe kuundwa kwa timu na ndugu zetu wa TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) ili tupate picha kamili ya nani wa kwenda naye,” alisema.
Alisema anashindwa kumhukumu mtu kwa sababu namba zinatofautiana huku akimpongeza mkuu wa shule kuwekewa Sh. bilioni tatu za ujenzi wa shule.
Makonda alimuuliza mkuu wa shule mara yake ya mwisho kuwekewa fedha nyingi ni Sh. ngapi akasema ilikuwa Sh. Sh. milioni 50.
“Mwalimu kazi yake ni kufundisha lakini alipatiwa jukumu lingine. Haikuwa kazi rahisi sasa tukipita kwenye nyaraka tuone kila fedha iliyotoka shilingi kwa shilingi uwe na maelezo. Timu inayokuja mwalimu naomba usiniangushe,”alisema