Watu 14 wamefariki na wengine 18 kujeruhiwa kufuatia kutokea kwa ajali iliyohusisha magari matatu katika Mlima wa Simike uliopo eneo la Mbembela, jijini Mbeya.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema ajali hiyo imetokea majira ya saa saba mchana kwa kuhusisha Lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 979 CVV likiwa na tela namba T 758 BEU.
Amesema Lori hilo lilikuwa likiendeshwa na Dereva Ross Mwaikambo (40), likitokea Shamwengo likiwa limepakia kokoto ambapo liligonga gari nyingine aina ya Toyota Coaster namba T 167 DLF na Toyota Harrier yenye namba za usajili T 120 DER.
“Lori hilo liliendelea kugonga guta namba MC 660 BCR na kisha kugonga pikipiki namba MC 889 CKX, chanzo cha ajali ni uzembe wa Dereva wa lori namba T 979 CVV kushindwa kulimudu gari kwenye mteremko,” amesema Kamanda Kuzaga.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Dereva wa gari hilo ambaye anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.