Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameendelea kutoa msimamo na kusisitiza suala la oparesheni ya kuwakamata Madada Poa lililoanzishwa na DC wa Ubungo, Hassan Bomboko ni zoezi endelevu na kusema litaendelea kufanywa na Wakuu wote wa Wilaya za Dar es salaam ili kukomesha vitendo vya uvunjifu wa maadili Mitaani.
Akiongea leo June 23,2024 Jijini Dar es salaam, Chalamila amesema “Suala la oparesheni za Madada Poa huo ni mwanzo tu litaendelea sana, tumeshapokea malalamiko kutoka kwa Wazazi kwamba Watoto wao wanapokwenda Shuleni wanashuhudia vitu ambavyo ni kinyume na maadili”
“Nimeona baadhi ya Waandishi mnawahoji baadhi ya Watu akiwemo Mjamzito aliyeonesha alikamatwa ghafla akiwa anaingia dukani Sinza Mori akaendelea kumlalamikia DC wa Ubungo, Ndugu zangu Waandishi Sinza Mori ni Kinondoni wala sio Ubungo maana yake unaweza kuona Mwandishi ukipata habari kabla haujazirusha ebu balance story ili usikie upande mwingine, ni muhimu kumuuliza ulikamatiwa duka gani?, ulipelekwa kituo kipi cha Polisi”
“Katika oparesheni hii wapo baadhi ya Watu wanajaribu kulichukulia kimizaha, Mimi kama RC nitakanyaga clutch kuhakikisha jambo hili halikomi leo wala halikomi kesho, masuala yote ya kisheria niliyoyaona mitandaoni, wapeleke popote pale wanapodhani, na sisi tunaiheshimu Mahakama tutasimama imara”
“Ndugu yetu Bomboko kamwe hayuko peke yake, Mimi ndiye Kaka yake mkubwa wa Mkoa huu niko hatua tano mbele, yuko hatua chache nyuma, yuko kulia kwangu yuko kushoto kwangu na Wakuu wa Wilaya wote wa mkoa wa Dar es salaam wataendelea kufanya shughuli hizo”