Kuna lingine huko... ni swali lililokuwa likiulizwa kwa furaha na mashabiki wa Yanga baada ya timu hiyo kutetea taji la Kombe la Shirikisho kwa msimu wa tatu mfululizo baada ya kuichapa Azam kwa penalti 6-5 katika fainali kali iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan, mjini hapa.
Katika fainali hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi Ahmed Aragija lililolazimika kwenda hadi dakika 120 baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu, mashabiki walipata burudani kwa namna nyota wa timu zote walivyotembeza boli uwanjani.
Hiyo ilikuwa ni fainali ya tisa tangu kurejeshwa kwa michuano hiyo msimu wa 2015-2016 na hilo ni taji la kwa mara ya tatu mfululizo, huku hicho kikiwa ni kipigo cha tatu cha fainali kwa Azam mbele ya Yanga.
Pia lilikuwa pambano la pili la fainali za michuano hiyo kuamuliwa kwa penalti baada ya ile ya msimu wa 2021-2022 ambapo Yanga iliifunga Coastal Union kwa penalti 3-2 baada ya dakika 120 kuisha kwa sare ya 3-3.
Jana dakika 120 ziliisha kwa suluhu ndipo zikafuata penalti na Yanga kumaliza ubishi baada ya Idd Seleman ‘Nado’ kupaisha penalti baada ya awali Kennedy Musonda kuitanguliza kwa kufunga iliyokuwa penalti ya tisa kwa Yanga.
Katika penalti tano za awali, Yanga ilipata kupitia kwa Pacome Zouzoua, Yao Kouassi na nahodha Bakar Mwamnyeto, huku Stephane Aziz KI na Joseph Guede, huku kwa Azam waliofunga walikuwa ni Cheikh Sidibe, Adolph Mtasingwa na Kipre Junior, huku Yeison Fuentes na Gjibril Sillah wakikosa.
Kisha zikaja moja moja ambapo Ibrahim Bacca alikosa wakati Mwamnyeto na Musonda kufungwa, huku Lusajo Mwaikenda na Nado wakikosa zao, ilihali Charles Manyama na Feisal Salum wakifunga.
Ibrahim Bacca alichaguliwa mchezaji bora wa fainali hiyo na kuvuna Sh 1 milioni, huku Clement Mzize akitangazwa Mfungaji Bora akifunga matano sawa na aliyomalizana nayo Edward Songo wa JKT Tanzania.
Katika dakika 90 zilikuwa na kosa kosa nyingi, hasa kwa Yanga waliotengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini umahiri wa kipa Mohamed Mustafa uliwanyima mabao katika dakika 45 za kwanza na zile za kipindi cha pili.
Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko na kuongeza utamu wa fainali hiyo huku bato ikiwa eneo la kiungo lililokuwa na Khalid Aucho na Mudathir Yahya wa Yanga na Adolf Mtasingwa na Yahya Zayd. Fei Toto alikuwa akija kuwasaidia.
Mara kadhaa, Fei Toto alionekana kukamiwa zaidi na viungo wa Yanga ambapo mara mbili tofauti Mudathir alizama uvunguni kuwania mpira na kufanikiwa.
Makocha wa timu zote mbili, waliingia uwanjani na mbinu ya kuuchezea zaidi mpira kati kitu ambacho watazamaji walienjoi.
MUDATHIR AISHIA NJIANI
Dakika 88 zilitosha kwa Mudathir Yahya kucheza mchezo huo kwani alitolewa na nafasi yake ikachukuliwa na Kennedy Musonda.
Kabla ya hapo, yalifanyika mabadiliko mengine ambapo dakika ya 75, Clement Mzize alimpisha Joseph Guede. Baadaye dakika ya 90, Jonas Mkude akaingia kuchukua nafasi ya Maxi Nzengeli, huku Yahya Zayd akimpisha James Akaminko kwa upande wa Azam.
Wakati Mudathir akiishia njiani, Fei Toto alimaliza dakika zote 120.
MZIZE ASHINDA VITA
Katika fainali hii, Clement Mzize wa Yanga na Abdul Seleman Sopu, waliingia uwanjani wakiwa na vita yao ya kuwania ufungaji bora, lakini vita hiyo haikudumu hadi mwisho wa mchezo, ikamaliza dakika ya 100 baada ya kutangazwa Mfungaji Bora, huku Sopu ambaye hakumaliza mchezo huo kwa kuumia alimaliza na mabao manne.
Mzize alitolewa dakika ya 75, kisha Sopu alifuata dakika 10 baada ya kuongezwa zile 30.
MSAUZI WA YANGA
Mpho Maruping ambaye ni mtaalamu wa kusoma mchezo ndani ya Yanga, alikuwa mchora ramani wa mechi hii akitoa maelekezo kutokea jukwaani.
Msauzi huyo alikuwa amevaa kifaa maalum cha kuwasiliana na Meneja wa Yanga, Walter Harrison ambaye aliwasilisha ujumbe kwa Miguel Gamondi, kisha yanafanyika mabadiliko.
DABO, GAMONDI
Makocha wa timu hizo, Youssouf Dabo wa Azam na Miguel Gamondi hawakukaa vitini kutokana na mcghezo ulivyokuwa mkali na kuishia kutoa maeleko na wakati mwingine kulaumua waamuzi, kiasi Gamondi alipewa kadi ya njano.
Katika fainali hiyo viongozi mbalimbali wa Yanga, serikali na wale wa TFF na ZFF waliohudhuria kupata burudani, huku Uwanja wa Amaan ukijaa na kutapika kutokana na mashabiki waliojitokeza.
Mara ya pambano hilo makocha wote walikiri pambano lilikuwa gumu na Gamondi aliwapongeza wachezaji kwa namna walivyopambana na kuiwezesha timu ibebe medali na taji hilo walilokabidhiwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro akisaidiana na Rais wa TFF, Wallace Karia.
Hilo ni taji la nne kwa Yanga tangu michuano iliporudishwa, lakini ni la nane kwa jumla tangu michuano ilipoasisiwa ikiwa na jinan la Kombe la FAT mwaka 1967 kisha kuwa Kombe la FA lililozimika rasmi mwaka 2002.
Vikosi vilivyoanza jana;
AZAM FC: Mustafa, Lusajo, Msindo/Sidibe, Fuentes, Bangala/Manyama, Zayd/Akaminko, Adolph, Sopu/ Idd Nado, Kipre Jr, Fei Toto na Sillah.
YANGA: Diarra, Yao, Lomalisa./Mwamnyeto, Bacca, Job, Aucho, Maxi/Mkude, Mudathir/Musonda, Mzize/Guede, Pacome na Aziz KI.