Arusha. Idadi ya waliofariki dunia katika ajali ya moto iliyoua watoto watatu wa familia moja jijini Arusha jana, imeongezeka baada ya Zuberi Msemo ambaye ni baba wa watoto hao kupoteza maisha usiku wa kuamkia leo Jumapili Juni 23, 2024.
Baba huyo alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru jijini Arusha.
Ajali hiyo iliyotokea jana Jumamosi Juni 22, 2024 katika Mtaa wa Olmatejoo jijini Arusha, ikidaiwa kusababishwa na kopyuta mpakato (laptop) iliyokuwa imechomekwa kwenye soketi ya umeme kushika moto na kuunguza kochi.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji, Jeradi Nonkwe jana amethibitisha vifo vya watoto watatu huku watu wengine akiwamo mtoto mchanga wa siku nne wakinusurika baada ya kuwahishwa hospitalini kwa matibabu.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Juni 23, 2024, mmoja wa wanafamilia, Mohamed Mussa amesema mbali na watoto hao, “baba yao Zuberi Msemo naye amefariki usiku wa kuamkia leo, nadhani ni kutokana na kumeza moshi mwingi alipokuwa akijaribu kuwaita watu waje wasaidie kuwaokoa.”
Amesema jana katika uokozi, baba huyo alizidiwa na moshi kiasi cha kupoteza fahamu.
“Baada ya kuona moshi mkubwa na milango imekaza alitoka kwenda kwenye dirisha la chooni kuita msaada ndio nikasikia na tukaanza uokozi, lakini baada ya kutoa watu wote yeye tulimkosa na katika kutafuta sana baada ya muda tulimpata huko akiwa hoi,” amesema.
Awali, akizungumza na Mwananchi Digital, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji, Nonkwe alisema watoto watatu waliofariki dunia ni Mariam Zuberi (9), Salma Zuberi (7) na Bisma Zuberi (3).
Amewataja wengine wanaoendelea na matibabu kuwa ni mama wa watoto hao, Jasmine Khatibu (33), Mariam Mussa (60), Mwanaid Aldina (50), Mussa Msemo (34), AbdulKarim Ramadhan (9) na dada wa kazi aliyefahamika kwa jina moja la Ester (20).
Mmoja wa madereva bodaboda wa eneo hilo, Ernest Swalehe amesema alikuwa anapita eneo hilo asubuhi akitokea mjini alikompeleka abiria, akaona nyumba hiyo iliyoko pembezoni mwa barabara ikitoka moshi ndio akaanza kuita watu wa ndani kabla ya kuanza kuwaamsha majirani wengine.
“Nilipoona kimya na wakati najua hii nyumba huwa ina watu wengi, nikaamua kupaki pikipiki na kuanza kugonga mageti ya jirani ambao nao waliitika kwa wingi na kuanza kuvunja geti kabla ya kuingia ndani na kung’oa madirisha, ndipo tulipofanikiwa kuwatoa watu hao,” amesema Swalehe.