Chama cha Mapinduzi (CCM), kimemkaribisha ndani ya chama hicho, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa.
Ukaribisho huo, umetangazwa leo Jumatatu, Juni 3, 2024 katika mkutano mkubwa wa hadhara, uliofanyika Soko la Kilombero, Arusha Mjini na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla.
Mkutano huo ni wa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi wa kufuatilia utekelezaji wa Ilani, kusikiliza kero za wananchi na kuangazia maandalizi ya chaguzi zijazo za Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.
Katika mkutano huo, Makalla amesema amemwona Mchungaji Msigwa akilalamika kutokutendewa haki kwenye uchaguzi wa Kanda ya Nyasa uliofanyika Mei 29, 2024.
Mchungaji Msigwa aliyekuwa akitetea nafasi ya uenyekiti alishindwa na mshindani mwenzake, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu. Msigwa alipata kura 52 na Sugu kura 54.
Makalla amesema huko upinzani hali si shwari, wanagomgambana wao kwa wao jambo linaloashiria hakupipiki chungu kimoja.
"Pole sana Mchungaji Msigwa, njoo Chama cha Mapinduzi kuna demokrasia tele, kuna uwazi, hicho chama hakikufai tena," amesema Makalla
Mwenezi huyo amesema kwa walichokiona Arusha wamedhihirisha:"Ni ngome ya Chama cha Mapinduzi na niwaeleze Arusha sumu haionjwi, kasi za maendeleo ni kubwa na ninawaomba ikifika wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa kura zote kwa CCM na tukiwashinda kwa kishindo tutawapelekea salamu."
"Kwa sasa Arusha imetulia, hawaandamanishwi, utalii umekuwa, tusirudi nyuma, tusonge mbele," amesema.
Leo asubuhi Jumatatu, Mchungaji Msigwa amezungumza na waandishi wa habari mkoani Iringa na kueleza amekata rufaa katika chama hicho, akidai ushindi alioupata Sugu haukuwa halali.
Msigwa amedai mifumo ya chama imetumika kumhujumu ili asishinde, kitendo ambacho amesema kitaifanya Chadema kukosa uhalali wa kuikosoa CCM. Amedai kulikuwa na mbinu chafu dhidi yake.
Katika hilo, Mkurugenzi Itifaki, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema kama kweli Msigwa amekata rufaa na kufuata mfumo unaotakiwa, rufaa yake itasikilizwa na kutolewa uamuzi, kwa sababu Chadema ni chama kinachoheshimu demokrasia.