Vuta picha hapa kuna Clatous Chama kule Prince Dube katika kikosi cha Yanga chenye nyota wengine kama vile, Stephane Aziz KI, Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na Mudathir Yahya ambao waliwafanya Wananchi kutembea kifua mbele msimu uliopita na kusherehekea ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA).
Chama ambaye mkataba wake umemalizika Msimbazi inadaiwa amemalizana na Yanga huku Dube naye akitajwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya mabingwa hao wa kihistoria baada ya sakata lake na waajiri wake wa zamani Azam kutajwa kufikia tamati kwa mujibu wa vyanzo vya ndani.
Ishu iliyopo kwa sasa ni kama wachezaji hao watasajiliwa Jangwani na namna ambavyo watatumiwa na kocha, Miguel Gamondi ili kupata kilicho bora kutoka kwao kwenye kikosi ambacho msimu uliopita kilifanya vizuri kuanzia kwenye ligi hadi Ligi ya Mabingwa.
Yanga ya msimu uliopita, ikiongozwa na Aziz KI kwenye safu ya ushambuliaji ndio timu iliyofunga mabao mengi zaidi ligi kuu (71), ilikuwa na wastani wa kufunga zaidi ya mabao mawili (2.3) katika kila mchezo na hapo waliuanza msimu huo bila ya kuwa na mshambuliaji hatari wa kati kiasili.
Nyuma yake Yanga waliondokewa na aliyekuwa mshambuliaji wao kinara Fiston Mayele, hivyo Kennedy Musonda na Clement Mzize walishindwa kuvaa viatu vya Mkongomani huyo aliyetimkia Misri, ndipo wakati wa dirisha dogo alipotua Joseph Guede.
Kutua kwa Guede kulikuwa na maana kwamba Gamondi alihitaji nguvu zaidi eneo hilo na je kuongezeka kwa Dube kuna maana gani? Na vipi kuhusu Chama? Hii ni mifumo tofauti ambavyo Yanga inaweza kucheza ikiwa na wachezaji hao.
4-3-3
Huu ni miongoni mwa mifumo maarufu na wa kisasa, ambao unatoa uwiano mzuri wakati wa kushambulia na kuzuia. Unaundwa na mabeki wanne, viungo watatu na washambuliaji watatu.
Katika mfumo huo Dube ambaye msimu uliopita alifunga mabao saba katika ligi akiwa na Azam FC, anaweza kuwa mshambuliaji kiongozi kati ya nyota watatu wa mwisho kwa kushirikiana na Pacome, Nzengeli/ Mzize au Mudathir ambaye hivi karibuni amekuwa akitumika katika eneo hilo ndio maana msimu uliopita alimaliza akiwa na mabao tisa katika ligi.
Nani wa kuanza kati ya hao wa kusaidiana na Dube, itategemea na Gamondi atakavyoamka siku hiyo na aina ya mpinzani ambaye wanakabiliana naye lakini kati ya watatu wa nyuma ya Mzimbabwe huyo, anaweza kuanza Khalid Aucho kama kiungo pekee mwenye jukumu la kukaba huku kushoto akicheza Chama na kulia Aziz KI.
Nyota hao watakuwa huru katika eneo hilo kuchezesha timu, hivyo Yanga inaweza kuwa moja ya timu yenye safu bora zaidi ya viungo wachezeshaji kutokana na rekodi za wachezaji hao, wote ni wazuri katika upishi wa mabao kutokana na ufundi walionao.
4-4-2
Miongoni mwa mechi ambazo Yanga ya Gamondi iliutumia mfumo huo ni pamoja na ile ya hatua ya robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns, Gamondi aliwavuruga matajiri hao wa Afrika Kusini kwa kuanza na washambuliaji wawili kiasili, Mzize na Guede japo walikuwa na majukumu tofauti.
Katika mfumo huo, Dube anaweza kuanza sambamba na Mzize au Musonda kama atahitaji kuanza na washambuliaji wawili wa kati kiasili au anaweza kuanza na mshambuliaji mmoja wa kati kiasili ambaye ni Dube huku akicheza sambamba na kiungo mwenye uwezo wa kusimama eneo hilo ambaye ni Aziz KI ameonyesha msimu uliopita.
Kati ya viungo wanne, kama Gamondi atataka kuanza na wawili wenye uwezo wa kukaba zaidi basi nafasi inaweza kuwa kwa Aucho na Mudathir huku jukumu la kuchezesha timu likiwa mikononi mwa Chama na Aziz KI watakaokuwa na jukumu la kushambulia kutokea pembeni, watakuwa mabeki wa kushoto na kulia ambao ni Kouassi Attohoula Yao na Nickson Kibabage au Chadrack Issaka Boka.
Ikiwa Gamondi atataka kuanza na kiungo mmoja tu mwenye sifa nzuri za kuzuia zaidi basi Aucho au Mudathir mmoja atasubiri benchi hivyo itakuwa ni nafasi ya Pacome au Nzengeli kuungana na Chama pamoja na Aziz KI kunogesha eneo hilo.
4-2-3-1
Muundo huu unatoa nafasi ya kucheza na mabeki wanne, viungo wawili wa ukabaji, na watatu wanaoshambulia huku mshambuliaji wa kati akiwa mmoja.
Dube anasimama kama mshambuliaji kiongozi huku nyuma yake kukiwa na viungo watatu washambuliaji ambao wanaweza kuwa Chama, Aziz KI na Pacome au Nzengeli.
Uwepo wa Dube unaweza kumfanya Gamondi amrudishe Mudathir katika eneo la ukabaji hivyo katika mfumo huo anaweza kushirikiana na Aucho huku Jonas Mkude akiwa na kibarua cha kupambana kupenya eneo hilo sambamba na Salum Abubakar 'Sureboy'.
3-5-2 Uwepo wa Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Hamad 'Bacca' na hata Gift Fred ambaye hazungumzwi sana unatoa nafasi kwa Gamondi kutumia mfumo huu ambao huwa na mabeki watatu wa kati, idadi ya viungo huwa watano wapo ambao huwa na jukumu la kusaidia kulinda.
Yanga ilicheza hivyo wakati ambao ilimkosa Yao kutokana na majeraha huku Nzengeli akifanya vizuri upande wa kulia kati ya viungo watano huku akiwa na jukumu la kushuka chini ya kusaidia kuzuia, katika mfumo huo tunaweza kuona Chama, Aziz KI, Pacome, Aucho na Mkongomani huyo wakicheza kwa pamoja.
Huku Dube akiendelea kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo sambamba na Mzize au Musonda.
Guede njia panda
Nani atampisha Prince Dube katika safu ya ushambuliaji ya Yanga ndio mtihani ambao inaelezwa unawapasua kichwa vigogo wa timu hiyo baada ya kudaiwa kukamilisha dili la straika huyo Mzimbabwe na msala umewaangukia Kennedy Musonda na Joseph Guede ambaye alikiwasha mwishoni mwa msimu uliopita.
Awali ilikuwa ikielezwa huenda Musonda ndiye atakayeondoka Jangwani baada ya mkataba wake kumalizika lakini ni kama kibao kimegeuka na huenda akashuhudiwa akisalia kutokana na kipengele cha mkataba wake aliosaini miaka miwili iliyopita wakati akitua nchini akitokea Power Dynamo ya Zambia.
Ipo hivi, Yanga inafikiria kutumia kipengele hicho (alisaini miaka miwili huku watatu akitakiwa kuongeza ikiwa atafanya vizuri) kwa kumuongeza mwaka mwingine mshambuliaji huyo huku ikitajwa kuwa na mpango wa kumuonyeshea mlango wa kutokea Guede ambaye licha ya kuingia wakati wa dirisha dogo msimu uliopita alifunga mabao sita katika Ligi Kuu Bara.
Kabla ya kufanya maamuzi hayo, inaelezwa kwamba vigogo hao wanataka kuhakikisha Yanga inakuwa na safu kali zaidi ya ushambuliaji na ndio maana wapo pia katika mazungumzo kwa karibu na mshambuliaji wa zamani wa Geita Gold, George Mpole.
Mpole ambaye kwa sasa yupo nchini kwa mapumziko akitokea DR Congo ambako alikuwa akiichezea FC Saint Eloi, anatazamwa kama chaguo sahihi la kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho cha Miguel Gamondi ambacho kinajukumu zito msimu ujao kutetea ubingwa wa ligi na Kombe la Shirikisho (FA) huku wakiwa na jukumu la kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka Yanga inaelezwa ishu ya Mpole inaweza kukamilika ndani ya siku chache zikazo kabla ya kuanza kwa maandalizi ya msimu ujao, ikumbukwe mabingwa hao wa Kihistoria wanamualiko wa kwenda Ulaya ambao wamepewa na miamba ya soka la Urusi, CSKA Moscow.
Msikie Musonda
"Nimeitumikia Yanga kwa misimu miwili nimebakiza mwaka mmoja ambao ni wa uamuzi wa viongozi wa timu kuamua mimi kuendelea kucheza au kuondoka," alisema na kuongeza; "Mimi ni mchezaji kama sitaweza kucheza tena Yanga au nikaendelea ni suala la muda tu na mimi ni mchezaji nipo tayari kwa lolote maisha ya mpira yapo hivyo leo unaweza ukacheza timu hii na kesho unacheza nyingine."