Changamoto 10 Kubwa Atakazo Kabiliana Nazo Mo Dewji Kuirudisha Simba Njia Kuu


Baada ya Mohamed Dewji Mo kukubali kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, kutokana na Salim Abdallah 'Try Again' kujiuzulu sasa inaonekana kuwa ana mitahani kumi ambayo ina mkabili ili timu hiyo irudi kwenye mstari.

Try Again juzi alitangaza kujiuzulu nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba ikiwa ni siku chache baada ya wajumbe watano wa bodi hiyo upande wa mwekezaji kujiuzulu kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo.

Wakati Try Again akitangaza kujiuzulu nafasi hiyo, alimuomba Mo Dewji kuchukua kiti hicho. Ikumbukwe kwamba, hapo awali Mo Dewji alikuwa Mwenyekiti wa Bodi kabla ya kujiuzulu Septemba 2021, akikaa kwa miaka minne na kumuachia kijiti Try Again. Mo Dewji akatangazwa kuwa Rais wa Heshima Simba.

Kurejea kwa Mo Dewji katika nafasi hiyo ambayo kiutaratibu itabidi aigombee upya, kuna mengi yameibuka. Miongoni mwa hilo ni namna mitihani kumi anavyokwenda kukutana nayo huku mashabiki na wanachama wa klabu hiyo wakiwa na hamu kubwa ya kuona matokeo chanya.

Usajili

Kilio kikubwa cha Wanasimba ni sehemu ya usajili wa kikosi chao ambapo inatajwa kwamba ndiyo imewafelisha zaidi kipindi hiki ambacho wanajitafuta kurudi kwenye njia yao ya utawala. Msimu uliomalizika, Simba imeshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, kitu ambacho kimewaumiza zaidi Wanasimba kwani msimu ujao wanakwenda kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika na siyo Ligi ya Mabingwa.

Timu hiyo sio kwamba haikufanya usajili msimu uliomalizika, bali wachezaji wengi walioingia kikosini hapo wameshindwa kutoa matokeo chanya akiwemo Aubin Kramo ambaye msimu mzima alikuwa majeruhi, Pa Omar Jobe na Babacar Sarr walioingia dirisha dogo wameshindwa kukata kiu ya mashabiki. Wapo waliofanya vizuri akiwemo Ayoub Lakred na Freddy Michael licha ya kuanza taratibu.

Hao ni kwa upande wa wachezaji wa kimataifa ambao ndiyo wanatolewa macho zaidi na Wanasimba kwani wanaamini kutokana na kushiriki kwao michuano ya kimataifa basi wanapaswa kusajili majembe ya maana kutoka nje.

Mo Dewji ana jukumu kubwa la kuhakikisha Simba inafanya usajili mzuri na wenye tija kwa timu jambo ambalo litarudisha ushindani wao katika michuano wanayokwenda kushiriki.

Kuhusu usajili, Mo Dewji amesema: "Tumekuwa tukisajili wachezaji wengi ambao wameshindwa kukidhi kiu ya Wanasimba, nataka niwaambie Wanasimba tutakwenda kufanya usajili mzuri utakaorudisha ubora wa kikosi chetu."

Safu ya uongozi

Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba upande wa Mwekezaji, wote wameachia ngazi akiwemo mwenyekiti wao, Try Again, hivyo lazima iundwe safu mpya ya uongozi kuja kuungana na wajumbe upande wa wanachama wanaoendelea kudunda wakitangaza kwamba hawana mpango wa kujiuzulu kama wenzao.

Imani kwa mashabiki

Simba kufanya vibaya kwao imepelekea mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuondoa imani na timu yao na wengi hawaendi uwanjani. Katika kipindi cha misimu mitatu sasa, Yanga imeendelea kutawala huku Simba ikisuasua na yote hayo lawama zinakwenda kwa viongozi.

Mo ametangaza kurejea, anapaswa kurudisha imani ya mashabiki na hilo haliwezi kufanikiwa kama itashindikana kuwa na timu nzuri. Simba ilikuwa ikisifika kwa kucheza soka la kuvutia, lakini hapo kati hali imebadilika, ikawa ni muhimu kupata ushindi tu, mengine ziada.

"Kiukweli tumepoteza falsafa yetu ya kucheza soka biriani, lazima turudi kwenye falsafa yetu," anasema Mo.

Kuifunga Yanga Ngao ya Jamii

Watani wa jadi wa Simba ni Yanga, timu hizo zinapokutana hakuna ambaye anapenda kuona mwenzake ameshinda. Hilo linaufanya mchezo wao kuwa na hisia kali sana ndani na nje ya uwanja kwa kuwa Simba iliteseka msimu mzima uliopita ilipofungwa jumla ya mabao 7-2 kwenye mechi za ligi.

Simba na Yanga zinakwenda kukutana tena katika mechi ya ufunguzi wa msimu ujao ambapo michuano hiyo inahusisha timu nne ikianzia nusu fainali. Zingine ni Azam na Coastal Union.

Nusu fainali itakuwa Yanga vs Simba na Azam vs Coastal Union, washindi wanakwenda fainali kuwania taji ambalo linashikiliwa na Simba. Hapa ni kipimo kingine cha Simba kuonyesha ubabe wao mbele ya Yanga na kutetea taji lao ambalo walilitwaa kwa kuichapa Yanga kwa penalti msimu uliopita.

Benchi imara la ufundi

Msimu uliomalizika, Simba imefundishwa na makocha watatu tofauti. Alianza Roberto Oliveira 'Robertinho', akaondoka Novemba 2023, akaja Abdelhak Benchikha ambaye naye safari iliishia Aprili 2024. Makocha wote hao ni wa kigeni, mzawa Juma Mgunda akamalizia.

Kitendo cha kubadilisha makocha ndani ya kipindi cha muda mfupi kimetajwa kuwa ni sehemu ya kufeli kwa Simba, hivyo Mo Dewji anapaswa kuliangalia hili.

"Tumeshindwa kutengeneza timu bora ya ushindani, eneo la benchi la ufundi halikuwa zuri hali ambayo imepelekea hata kupotea kwa falsafa yetu ya pira biriani. Hili ni eneo muhimu la kufanyia kazi. Nawaahidi nitashirikiana na viongozi wenzangu kusuka upya benchi la Ufundi," amesema Mo.

Utawala Simba

Simba na Yanga ndiyo timu kongwe katika Ligi Kuu Bara na zimeweka utawala wao kwani katika kipindi cha misimu 20 iliyopita, zimekuwa zikibadilishana ubingwa wa ligi hiyo, mara moja tu Azam imeingilia kati.

Misimu mitatu mfululizo sasa, Yanga imeweka utawala wake kwa kubeba ubingwa wa ligi mfululizo, kabla ya hapo, Simba ilifanya hivyo kwa misimu minne nyuma.

Wakati Simba ikishinda ubingwa wa ligi mara nne mfululizo 2017/2018, 2018/19, 2019/20 na 2020/21, Mo Dewji alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, hivyo kuondoka kwake ni kama aliondoka na makombe yake.

Sasa anarejea, matumaini makubwa ni kurudisha ule utawala uliopotea wakati yeye amekaa pembeni kidogo.

Kucheza nusu fainali

Malengo ya Simba muda mrefu yalikuwa ni kucheza hatua ya nusu fainali katika michuano ya CAF, hiyo ni baada ya kucheza robo fainali mara tano kuanzia 2018. Misimu ya karibuni, timu hiyo katika kuishia kwao robo fainali ilionekana ni kitu kidogo tu kinawafelisha, hivyo kuelekea msimu ujao ambapo watashiriki Kombe la Shirikisho, wana kazi ya kufanya kufikia malengo.

Umoja

Kauli mbiu ya Simba ni Nguvu Moja, lakini Mo Dewji anaamini kwamba umoja huo haupo kwa sasa, hivyo anaporejea katika kiti chake cha awali, anapaswa kulisimamia hilo ili kuonyesha kuna mabadiliko.

Mwenyewe amesema: "Tumekuwa hatupo wamoja hasa baada ya msuguano wa uchaguzi, malumbano na mgawanyiko umeendelea kutafuna timu yetu, hili jambo halina afya, naomba niwaombe Wanachama, Wanasimba na mashabiki tumalize tofauti zetu za uchaguzi na kuzizika kabisa kwa kauli yetu ya Simba ya Nguvu Moja."

Mchakato wa mabadiliko

Hapa ndiyo kuna kazi kubwa ya kufanya kwani tangu uanze mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa Klabu ya Simba mwaka 2018, hadi leo kuna mvutano wa hapa na pale kiasi cha kufanya jambo hilo kuchelewa kukamilika.

Yamekuwa yakisemwa mengi juu ya mchakato huo wa mabadiliko, lakini jambo linalosubiriwa ni kuona kila kitu kikikamilika haraka kwani Wanachama wameridhia mabadiliko japo wanahitaji utaratibu ufuatwe.
Kuhusu mabadiliko, Mo anasema: "Nitahakikisha tunakwenda kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji ili wanachama waweze pia kupata hisa zao stahiki na kuwa wamiliki wa Simba SC."

Soka la vijana

Msingi wa timu nyingi zinazofanya vizuri kwa muda mrefu ni soka la vijana. Unaweza kuwa na timu bora kwa kununua wachezaji kila kipindi cha usajili lakini inaweza kufika wakati bajeti yenu inawabana hivyo wachezaji vijana mnaowakuza wanakuja kuwabeba.

Simba ni miongoni mwa timu ambazo huko nyuma zilikuwa na msingi mzuri wa soka la vijana. Tulishuhudia vijana wao wengi wakija kuwabeba mbele. Hiyo ilitokea miaka ya 2012 hadi 2015, lakini baada ya hapo, ni kama wamejisahau, vijana wanaopandishwa timu ya wakubwa hawapewi ile nafasi ya kukua zaidi.

Hivi sasa kipa Ally Salim unaweza kusema ni mmoja kati ya vijana wao wanaopata hiyo nafasi, lakini ilipaswa wawepo vijana wengine wengi wanapewa nafasi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma tuliposhuhudia Ramadhan Singano, Jonas Mkude, Said Ndemla na wengineo wakikiwasha.

MO amesema eneo hilo la uwekezaji kwa soka la vijana anakwenda kulisimamia kwa kuweka nguvu kubwa itakayozalisha vipaji kuanzia chini.

Mwananchi 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad