Hizi ndizo mashine 11 zinaotajwa kutua Simba

Hizi ndizo mashine 11 zinaotajwa kutua Simba


Tangu dirisha kubwa la uhamisho wa wachezaji kufunguliwa Juni 15, mwaka huu, Klabu ya Simba ndiyo imeongoza kuwa na tetesi nyingi za usajili kuliko zingine zote hapa nchini.


Inawezekana ni kwa sababu ya mahitaji, kwani hata viongozi wake kwa nyakati tofauti wamesema wanataka kufanya usajili mkubwa kwa kuondoka wachezaji wengi, ambao baadhi umri umekwenda, wengine wamelewa mafanikio, na wapo wanaotajwa kuwa na nidhamu isiyoridhisha na walioshuka viwango pia.


Kutokana na hilo, inawezekana kabisa msimu ujao, Simba ikawa moja kati ya timu zitakazosajili wachezaji wengi ili kuunda kikosi kipya chenye uchu wa mafanikio. Katika makala haya tunakuleta tetesi za wachezaji 11 ambao wanatajwa kuwa huenda wakavaa uzi mwekundu na timu zao walizotoka, ukimwondoa Lameck Lawi kutoka Coastal Union ambaye klabu imeshathibitisha. 


1# Omari Omari- Mashujaa FC Hadi kufikia jana, klabu hiyo ilikuwa katika hatua za mwisho kumsajili straika Omari Omari  kutoka Mashujaa FC. Habari zinasema kuwa kuna vitu vichache tu vimebaki kabla ya nyota huyo wa zamani wa Prisons kutambulishwa katika dirisha hili kubwa la usajili. 


2# Rahim Shomari- KMC Taarifa zinaeleza kuwa Simba inapigana huku na huko kuhakikisha inapata saini ya beki wa kushoto wa KMC, Rahim Shomari, ili kusaidiana na Mohamed Hussein 'Tshabalala.'


Chanzo hicho kimesema kuwa KMC ambayo makuzi yake yalianzia kwenye kikosi cha vijana cha Simba, anatajwa kwenda Msimbazi, huku klabu yake ikihitaji kiasi cha Sh. milioni 100 ili kumwachia. 


3# Anthony Tra Bi Tra- Asec Mimosas Inatajwa pia kuwa Simba iko kwenye mazungumzo na beki wa kati wa Asec Mimosas ya Ivory Coast, Anthony Tra Bi Tra ili kuziba pengo la beki Henock Inonga ambaye kwa siku za karibuni amepoteza mapenzi kwa wanachama na mashabiki wa Simba.


Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema baada ya kupata saini ya Lameck Lawi, sasa wanasaka beki mmoja kutoka nje ya nchi ambaye atakuja kusaidiana na waliopo. 


4# Derrick Fordjour- Medeama Katika kusaka mastraika watakaoiwezesha timu kurudi kwenye makali yake, imeelezwa kuwa ipo mbioni kukamilisha dili la kumsajili straika wa Medeama ya Ghana, Derrick Fordjour. Watanzania walimshuhudia msimu uliopita, akiwa kwenye kiwango cha juu, katika Ligi ya Mabingwa Afrika, timu yake ikiwa kundi moja na Yanga. 


5# Pedro Miguel- Petro de Luanda Katika kuhangaikia kusaka kiungo mkabaji, taarifa zinaeleza klabu hiyo imetua nchini Angola kusaka saini ya Pedro Miguel wa Petro de Luanda ambaye alikichafua msimu uliopita katika klabu yake hiyo na kuifanya kuongoza Kundi C, kabla ya kutolewa na TP Mazembe katika hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.  6# Ricky Banda- Red Arrows


Taarifa zinasema Simba imeanzisha mazungumzo na straika Ricky Banda anayekipiga katika Klabu ya Red Arrows ya Zambia.


Straika huyo amemaliza Ligi Kuu ya Zambia akiwa na mabao 10 na kuwa kinara wa ufungaji, akifungana na wachezaji wengine wawili waliofunga idadi kama hiyo ya mabao, Enock Sakala wa Zesco United na Prince Mumba wa Kabwe Warriors. 


7# Agostinho Mabululu- Al Ittihad Alitamba sana kwenye fainali za AFCON zilizofanyika mapema mwaka huu nchini Ivory Coast akiwa na timu yake ya Taifa ya Angola. Straika huyu anayeichezea Al Ittihad ya Misri naye anatajwa kuwa mmoja wa wachezaji ambao Simba wanachangamka ili atue Msimbazi. 


8# Jean-Marc Makusu- Hajer FC Mwanzoni kabisa wakati dirisha la usajili linafunguliwa, zilikuja taarifa zinazohusu klabu hiyo kuwa na mazungumza na straika wa zamani wa AS Vita, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Jean-Marc Makusu Mundele ili kusaidia eneo la ushambuliaji.


Kwa sasa anaichezea Klabu ya Hejer FC ya Saudi Arabia na amekuwa akihusishwa na Simba kwa misimu kadhaa ya hivi karibuni. 


9# Augustine Okejepha- Rivers United Taarifa hizi zimetoka juzi kuwa Simba iko mbioni kukamilisha dili ya kusajili kiungo mkabaji, Augustine Okejepha kwa mkataba wa miaka mitatu.


Mchezaji huyo aliyeonyesha kiwango kikubwa katika mechi za Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita akiwa na River United ya Nigeria, ameonyesha kukubaliana kila kitu na klabu hiyo na sasa kinachosubiriwa ni utekelezaji.   10# Kelvin Kapumbu- Zesco United Simba pia inadaiwa kuwa na mazungumzo na kiungo huyu wa Zesco ya Zambia, kuja kuimarisha eneo hilo ambalo limeonekana kwa miaka ya hivi karibuni linasuasua kitu ambacho si utamaduni wa klabu hiyo. 


11# Joshua Mutale- Power Dynamos Inaelezwa kuwa winga huyu machachari wameshasainiana mkataba wa miaka mitatu kuitumikia klabu hiyo kutoka Power Dyanamos ya Zambia, kinachosubiriwa ni utambulisho tu.


Winga huyo aliyemaliza ligi na mabao manane, anakumbukwa na mashabiki wa Simba, kwani aliwachachafya mabeki wa timu hiyo, hasa Shomari Kapombe katika mechi tatu ambazo timu hizo zimekutana, moja ya Simba Day na zilizobaki ni za Ligi ya Mabingwa Afrika katika hatua za awali msimu uliopita.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad