Jean Baleke Afichua SIRI ya Kuwepo Tanzania....




KITENDO cha straika wa zamani wa Simba, Jean Baleke kuonekana jijini Dar es Salaam, kimeibua tetesi nyingi za kuhusishwa timu mbalimbali za hapa nchini, Mwanaspoti liliingia chimbo ili kujua ukweli wa hilo.

Jitihada za Mwanaspoti kumsaka Baleke zilifanikiwa na kufanya naye Exclusive ambapo anafafanua kuhusiana na taarifa za kuhusishwa Simba, Yanga na Azam FC.

Uwepo wake Dar es Salaam, anaeleza kuna ishu kaja kuzifanya kisha ataondoka kwenda nchini kwao Congo kwa ajili ya kuiona familia yake.

“Kwanza nipo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mambo yangu, hapa ni kama nyumbani, kwani hakuna mambo ya viza kati ya Tanzania na Congo, hivyo naweza kuja wakati wowote, vivyo hivyo Watanzania wanaweza kwenda Congo.

Anaongeza”Nilisaini Al-Ittihad kwa mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja, nimetumikia miezi sita, imesalia sita, endapo kama kuna timu ambayo inanihitaji, ije tuzungumze, kazi yangu ni mpira kikubwa ni makubaliano kwenye maslahi.”

Baleke aliondoka Simba msimu ulioisha, akiwa amefunga mabao manane kwenda kujiunga na Al-Ittihad ya Libya, anasema kila timu anayokwenda anafanikiwa kuwa mfungaji bora.

“Ukiachana na msimu wangu wa kwanza wa 2022/23 ambao nilifunga mabao manane, wakati naondoka Simba nilikuwa naongoza kwa mabao manane, ningekuwepo naamini ningefunga mengi zaidi.

“Msimu wa 2022/23 nilikuwa kati ya wachezaji ambao niliamua kuweka nguvu kwa kaka yangu Said Ntibazonkiza ‘Saido’ ili achukue kiatu cha ufungaji bora na ikawa hivyo.

Anaongeza “ Nakumbuka niulimia mechi dhidi ya Polisi Tanzania, nilivyotoka nikaanza kumuombea Saido afunge mabao mengi, akafunga matano, ikawa ndio safari yake ya kuwania kiatu, walikuwa wanashindana na Fiston Mayele ambaye alikuwa Yanga.”

BENCHIKHA ALIMKATA

Baleke anazungumzia sababu ya kuondoka Simba, kwamba ni kocha Abdelhak Benchikha, hakumhitaji katika kikosi chake, hivyo hakukuwa na namna ya kusalia ndani ya kikosi hicho.

“Sikuhitaji kuzungumza lolote kuhusiana na hilo, kwa ajili ya mashabiki, watambue kwamba nilitamani kusalia Simba, ila kocha Benchikha aliniambia anahitaji mshambuliaji mwingine na siyo mimi, hivyo viongozi hawakuwa na namna” anasema.

AMTAJA BOCCO,CHAMA

Anasema wakati anaondoka kuna mastaa wengi walioumia, walitamani angeendelea kusalia kikosini, kama John Bocco, Clatous Chama, Kibu Denis, Hussein Kazi,Fabrice Ngoma,Shomary Kapombe na wengine wengi.

“Bocco alikuwa kiongozi mzuri sana, wakati anajua naondoka alinifuata na aliumia sana, kikubwa aliniambia nikapambane nitafika mbali, pia Chama alikuwa haamini kama ningeondoka, ila maisha ya mpira ni popote.

Anaongeza”Nawaambia mashabiki wa Simba, kwamba nawapenda kijana wao nipo hapa, nashukuru kwa muda wote ambao waliniunga mkono, lakini sikuwa na budi kwenda kuanza maisha sehemu nyingine.”

ILIBAKIA KIDUCHU IHEFU

Anasema baada ya Simba kutangaza kuachana naye, alipokea simu kutoka kwa mmoja wa viongozi wa Ihefu (Singida Black Stars), akimtaka asaini miezi sita,wakati akisubiri dirisha kufunguliwa.

“Zilikuwa zimebakia dakika chache dirisha la usajili kufungwa, hivyo nisingeweza kuingizwa kwenye mfumo wa usajili wa wachezaji wa timu, ndio maana kiongozi huyo, aliniambia nisaini nitakuwa nachukua mshahara na kufanya mazoezi na timu, lakini nisubiri kucheza hadi dirisha kubwa litakapofunguliwa.

Anaongeza”Kwangu ilikuwa ngumu, kwa sababu nimezoea kucheza, halafu ingetokea nikaumia katika mazoezi ingekuaje, kutokana na malengo yangu na umri nilionao, nilijiona nahitaji kucheza zaidi.”

MTUMIKIZI KANISANI

Anasema kabla ya kuanza kucheza soka la ushindani, akiwa kijana mdogo, alikuwa mtumikizi wa kanisani, yaani wale watoto ambao wanaowasaidia mapadri wakati wa misa.

“Kabla ya soka na shule kuniweka bize nilikuwa natumika kanisani, nikajikuta imekuwa ngumu kuendelea na utumikizi kanisani, pamoja na hayo mimi napenda sana kusali, nikiwa nakwenda uwanjani ama kutoka kwenye mechi lazima nisali kumshukuru Mungu,”anasema.

ANA DIPLOMA YA UINJINIA

Ukiachana na soka, ana taaluma ya uhandisi wa masuala ya umeme, ingawa kwa sasa inakuwa vigumu kuwekeza nguvu kufanya kazi zinazohusiana na hilo.

“Naweza nikatengeneza tv, feni, redio na vifaa mbalimbali vinavyotumia umeme, ila kwa sasa soka lipo kwenye damu na ndilo ninaloona linaweza likatimiza ndoto zangu za kimaisha,”anasema Baleke ambaye akiwa nyumbani anapenda kucheza gemu.

NGUMU KURUDI LIBYA

Alipoulizwa je, upo tayari kurejea Libya. Anajibu “Nina asilimia ndogo sana, kutokana na hali ya amani kuwa ndogo, nimewahi kuvamiwa mara tatu katika nyumbani niliyokuwa naishi, hivyo naweka nguvu kwenye ofa zilizokuja mezani.

Anaulizwa kati ya ofa alizonazo mezani zipo Simba, Yanga na Azam FC? Anajibu “Hizo hazijaleta ofa rasmi, lakini kama mojawapo ikiwa tayari basi kwangu nitakachoangalia ni maslahi yanayolipa, pia zizingatie kwenda kuzungumza na viongozi wangu wa TP Mazembe.”

MFUNGAJI BORA

Baleke ndiye mfungaji bora wa Ligi ya Libya, baada ya kujiunga na AL-Ittihad alicheza mechi nane, kafunga mabao 14 ikiwemo hat-trick nne.

“Naamini ningejiunga nao mapema ningefunga mabao mengi zaidi, pamoja na hilo, nashukuru nimeibuka mfungaji bora wa ligi ya Libya, ingawa sitamani kurejea kuichezea tena,”anasema.

Anasema kila timu anayokwenda kucheza anapenda ushindani, ambao unakuwa unamfanya asijibweteke na kuona kamaliza kila kitu”Jambo ninalolizingatia ninaposaini ni uwepo wa wachezaji wenye kiwango cha juu, ili nikipata nafasi niwe naithamini na kujituma uwanjani.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad