Wataalamu wa afya wameishauri Serikali ipambane na kasi ya ongezeko la magonjwa ya zinaa nchini, huku kaswende ikitikisa zaidi.
Kaswende husababisha magonjwa ya moyo, upofu, ugumba, mzio wa ngozi, ganzi mwilini na athari zingine.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, kaswende inakuwa tishio zaidi kwa kuwa aliyeambukizwa anaweza kuishi na maambukizi hayo hata zaidi ya miaka 10 mpaka 15 bila kuona athari za moja kwa moja huku akiendelea kuambukiza wengine.
Kauli ya wataalamu hao, inakwenda sambamba na ripoti ya utekelezaji wa mikakati ya sekta ya afya duniani juu ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), homa ya ini na magonjwa ya ngono ya mwaka 2022–2030 ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inayoonyesha ongezeko la magonjwa ya zinaa hususan nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ripoti hiyo inaonyesha magonjwa manne ya zinaa yanayotibika yaani kaswende, kisonono, klamidia na trichomoniasis, husababisha zaidi ya maambukizi milioni moja kila siku duniani.
Akizungumza Oktoba 2023, aliyekuwa Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya, Profesa Paschal Rugajjo alisema idadi ya waliopimwa na kubainika kuwa na kaswende ilipanda kutoka 16,015 mwaka 2017 hadi 26,592 mwaka 2019.
Alisema kaswende iligundulika zaidi kwa wajawazito waliopimwa na kupata matibabu na idadi yao iliongezeka kutoka 10,049 hadi 18,298 katika kipindi hicho.
Profesa Rugajjo alisema jitihada za makusudi zitawekwa kwa kuwa takwimu za matibabu ya kaswende miongoni mwa wanawake waliogunduliwa wanaohudhuria kliniki, ilikuwa asilimia 17.3, 22.4 na 25 katika mikoa ya Tanga, Dodoma na Dar es Salaam na 100 katika mikoa ya Kagera, Geita, Mara na Simiyu.
Hali halisi nchini
Kwa mujibu wa daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake Hospitali ya Salaaman, Abdul Mkeyenge wanawake wengi wamekuwa wakijifichia katika maambukizi ya njia ya mkojo kutibu magonjwa ya zinaa.
“Akija hospitali anataja dalili za UTI na wengine wanakwenda famasi, anameza dawa akijikuta yupo sawa anahisi amepona ile hali inakuwa inajirudia rudia.
“Wengi hulalamika kutokwa na uchafu sehemu za siri au majimaji, akinywa antibaotiki siku tano zile dalili zinapotea, mdudu bado yupo anaendelea kuathiri baada ya miezi kadhaa anapata PID kwa kuwa magonjwa ya zinaa yamekaa muda mrefu,” amesema.
Dk Mkenyenge amesema wanafika kutibu kaswende kufika wakiwa katika hatua za juu za ugonjwa, kwa kuwa mdudu wa kaswende anaweza kuishi ndani ya mwili hata miaka 15.
“Unashangaa umempima mtu mzima ana kaswende na hapo tayari dalili za wazi zimeonekana wengine ugumba, magonjwa ya moyo, magonjwa ya ganzi mwili mzima, ngozi inaharibika yaani anapata magonjwa ya ngozi siyo aleji kama inavyosemekana bali mdudu wa kaswende anamsumbua,” amesema.
Amesema kaswende ina hatua zisizopungua nne na mojawapo ni kupata kuanza kupata vipele sehemu za siri na kupotea, kupata muwasho au kidonda kisichopona au majimaji sehemu za siri.
Dk Mkeyenge amesema ni vema kupima mapema, kwa kuwa mdudu huyo anaweza kutosikia dawa, “waweza kupewa dawa zote ukipima unaikuta tena haitoki, kitu kikubwa kuelimisha watu kuhusu magonjwa ya zinaa, madhara ya kuyapata na baadaye kwanini watu wanayapata tuangalie vyanzo.”
Hata hivyo, anataja sababu za kiuchumi kuwa chanzo kwa kuwa ngono imekuwa sehemu ya kupata kipato kwa baadhi, hasa kwa wasichana na kinamama wadogo.
Mtaalamu mshauri wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati amesema Serikali pamoja na wadau wamejisahau kwamba, wanapaswa kusisitiza masuala ya kupima, kujipima na kuchukua tahadhari.
“Zamani ukifungua TV au redio matangazo kila siku yanapita watu wanakumbuka kujikinga, hasa kwa vijana ili kuendelea kujua hatari ya haya magonjwa ile elimu nguvu zimepungua sana, kuhusu masuala ya HIV (Virusi vya Ukimwi) na magonjwa ya ngono,” amesema.
Dk Osati amesema ili elimu irudi kwa jamii kampeni zilizofanywa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa mwaka 2000 ziendelee kufanyika kwenye shule, vyuo, maeneo mbalimbali, kazini, hospitalini na matamasha mengi yaendelea kukumbusha watu magonjwa hayo bado yapo.
Ripoti ya WHO
Ripoti ya Mei 21 2024 iliyotolewa na WHO inaashiria ongezeko kubwa la magonjwa ya zinaa maeneo mengi, huku kukiwa na changamoto za maambukizi ya VVU na homa ya ini katika afya ya jamii na kusababisha vifo vya watu milioni 2.5 kila mwaka.
Mnamo 2022, nchi wanachama wa WHO ziliweka lengo kuu la kupunguza idadi kila mwaka ya maambukizo ya kaswende kwa watu wazima mara kumi ifikapo 2030, kutoka milioni 7.1 hadi milioni 0.71.
Hata hivyo, visa vipya vya kaswende miongoni mwa watu wazima wenye umri wa miaka 15-49 viliongezeka kwa zaidi ya milioni moja mwaka 2022 na kufikia milioni nane. Ongezeko la juu zaidi lilitokea Kanda ya Amerika na Kanda ya Afrika.
"Kuongezeka kwa maambukizi mapya ya kaswende kunazua wasiwasi mkubwa kwa afya ya jamii, ingawaje upatikanaji wa bidhaa za afya unakua na uchunguzi wa matibabu," amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus.
Ripoti hiyo inabainisha ongezeko la kaswende ya watu wazima na wajawazito milioni 1.1 na kaswende ya kuzaliwa inahusishwa watoto 523 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa hai kwa mwaka.
Mwaka 2022, kulikuwa na vifo 230,000 vinavyohusiana na kaswende. Takwimu mpya pia zinaonyesha ongezeko la kisonono sugu