Kuhusu Kiwango cha Kelvin John Mbappe Kushuka na Kuhama Timu ya Genk

 

Kuhusu Kiwango cha Kelvin John Mbappe Kushuka na Kuhama Timu ya Genk

Baada ya dakika chache kutangaza kwamba ameachana na klabu ya Genk ya Ubelgiji, Kevin John, mchezaji aliyewahi kupachikwa jina la 'Mbappe wa Tanzania' alijitangaza kuwa mchezaji mpya wa klabu ya Aalborg ya Denmark. Jezi yao inavutia na Kelvin ni mchezaji wao mpya kuanzia sasa.


Kelvin amesogea au amerudi nyuma? Tusidanganyane. Amerudi nyuma. Nadhani hata yeye mwenyewe anafahamu na ndio maana baada ya kutangaza kuachana na Genk hapo hapo akatupoza kwa kutuwekea picha za timu yake mpya. Inaweza kuwa amewachanganya baadhi ya mashabiki wa soka nchini lakini tunaofahamu haya mambo hajatudanganya.


Tafuta orodha ya mastaa mahiri waliowahi kuibukia Aalborg na kutamba kwingineko. Nimemuona Ebba Sand. Staa wa zamani wa timu ya taifa ya Denmark. Lakini tafuta wachezaji walioibukia Genk na kwenda kwingineko. Wanajaza mabasi mengi ya Mwenge kwenda Mbagala. Wengine wameiteka dunia mpaka sasa hivi.


Aalborg inaweza kuwa kati ya timu maarufu za zamani pale Denmark, lakini Genk wanabakia kuwa Genk tu. Wamewatoa kina Kelvin De Bruyne, Kalidou Koulibaly, Leandro Trossard, Thibaut Courtois, Sander Berge, Wilfred Ndidi, Leon Bailey na zaidi ni kijana wetu mwenyewe, alama yetu ya soka, Mbwana Samatta 'Poppa'.


Genk wanawakilisha alama ya soka la Ubelgiji kama ilivyo kwa klabu nyingine kadhaa za Ubelgiji kina Royal Antwerp, Standard Liege, Gent, Anderlecht na wengine wengi. Wao ni daraja zuri la wachezaji wanaokwenda ligi kubwa zaidi. Kwanza Wabelgiji wenyewe wamepitwa na nani pale Ulaya? Wamepitwa na England, Hispania, Italia, Ujerumani na Ufaransa.


Genk wakati wanamchukua Kelvin walikuwa wanaamini kwamba wamepata bidhaa adimu ambayo ingeenda sokoni kwa bei nzuri. Labda kuanzia Pauni 15 milioni na kuendelea maana umri wa Kelvin ulikuwa unaruhusu. Na ukweli ni kwamba walikuwa wamemchukua huku akiwa moto katika soka la vijana Tanzania.


Zaidi ni kwamba wao walikuwa ni klabu pekee barani Ulaya ambayo ingemuamini kinda wa Kitanzania kwa urahisi. Sababu? Mbwana Samatta. Baada ya mambo makubwa ambayo Samatta alifanya Genk walifunguka macho na kuamini katika mchezaji anayetoka Tanzania. Taifa lisilo na jina kubwa kisoka barani Afrika.


Hata hivyo, Kelvin hakufikia matarajio yao. Na wala hakufikia matarajio yetu. Kwamba angekuwa Samatta mpya au namna mawazo yangu ya kipumbavu ambavyo yalikuwa yananiambia kwamba angeweza kuwa zaidi ya Samatta kutokana na kipaji kikubwa cha kufunga alichonacho lakini pia alikwenda Ulaya katika umri sahihi zaidi. Tulichokuwa tunakiona kwake nadhani ndicho ambacho Genk wamekiona.


Kadri siku zilivyoyoyoma ndivyo Kelvin alivyokuwa anaonekana mchezaji wa kawaida. Sisi wengine tulikuwa tunamuona zaidi wakati alipokuwa anakuja kuichezea timu ya taifa. Badala ya kuongezeka makali alikuwa anaongezeka kunawiri zaidi kwa nuru ya mwili wake. Ile kasi yake na jicho la goli hatukuviona tena.


Walio karibu yake wanadai ana mambo mengi. Walio karibu na timu ya taifa wanadai kwamba kocha Adel Amrouche alimuacha kwa sababu ya tukio kubwa la utovu wa kinidhamu alioufanya kambini. Imebakia kuwa siri ya wachache na ni jambo jema kwa sababu wakubwa hawataki kumgombanisha na mashabiki. Hata mimi naamini acha iendelee kuwa siri tu kwa sababu mashabiki wetu ni wagumu kusamehe.


Kinachouma kuhusu kuporomoka kwa Kelvin ni haya yafuatayo. Kwanza kabisa Taifa letu lina wachezaji wachache wanaocheza nje. Samatta ndiye kinara wetu. Halafu kuna kina Simon Msuva, Maurice Abraham na Novatus Dismas. Wengine wachache wanacheza ndani ya Afrika. Kina Himid Mao na wenzake.


Taifa linahitaji mafanikio ya Kelvin kama dawa adimu. Kina sisi matumaini ya mpira wetu tumeyaweka kwao. Kwanza watusaidie uzoefu wao wa soka la Ulaya walete katika timu ya taifa ambayo imesheheni wachezaji wengi wanaocheza ndani. Lakini hapo hapo tunawahitaji kwa sababu za nje ya uwanja. Ni kama vile ambavyo Samatta amefanya.


Tunahitaji wachezaji ambao wataviaminisha vizazi vijavyo kuwa mafanikio ya kucheza soka la kulipwa kwa mafanikio pale Ulaya yanawezekana. Kina Sunday Manara, Zamoyoni Mogella, Edibily Jonas Lunyamila na wengineo hawakuweza kuacha alama hii. Hawakubahatika. Hawa wa leo wana kazi hii na Samatta ameifanya vema sana kazi hii na ndio maana tunawakubalia watoto wetu wakwepe shule inapobidi wakacheze soka.


Lakini sababu nyingine ni ile ikiwemo Kelvin kuendelea kufungua njia yetu pale Genk. Rafiki zangu wa Afrika Magharibi wana tabia hii. Mchezaji mmoja akipita mahala anahakikisha anaacha jina kubwa kiasi kwamba raia wengine wa nchi yake wakifika hapo wanapata urahisi wa kuaminiwa. Hatuwezi kujidanganya ukweli kwamba kwa kiasi kikubwa Genk walimuamini Kelvin kwa sababu Samatta alikuwa amefanya mambo makubwa Genk.


Kama Kelvin angefanya mambo makubwa kwa mara nyingine tena ina maana Genk wangeendelea kuwa na jicho kali kwa wachezaji wa Kitanzania. Kwa sasa watahisi kwamba kwa Samatta ni kama Watanzania tulibahatisha tu. Kwamba labda ni kipaji kilichokuja nchini baada ya miaka mia kitu ambacho sio cha kweli. Lango letu la Genk lilipaswa kutetewa na jasho la Kelvin.


Sijui kama Kelvin alikuwa anajua kwamba yupo Ulaya na analazimika kupambana kwa sababu hizi mbili. Tunapotaka mafanikio yao taifa kama taifa huwa tunaangalia sababu hizi mbili. Suala la kufanikiwa kwa kipato huwa halituhusu. Ni suala binafsi na la familia zaidi. Noti zao huwa hazituhusu. Wala hatujawahi kumlaumu Samatta kwa kutosimama hadharani pale Mbagala na kugawa pesa. Ni jambo lake binafsi.


Kama Kelvin angejua anacheza kwa ajili yetu na sio yake binafsi nadhani angekuwa anapata msukumo mpya kila anapoamka asubuhi. Wenzetu kina Nigeria, Ghana, Morocco, Ivory Coast na kwingineko wanaweza kusababisha usiwe na msukumo huo kwa sababu wana wachezaji wengi. Ukizembea wewe bado kuna wengine tunawategemea. Sisi hatujazalisha wachezaji wengi mahiri wanaocheza Ulaya.


Haishangazi kuona taifa zima lilibaki kumtegemea Samatta peke yake. Na haishangazi pia wengi wetu tulibaki kumtegemea Kelvin kama mkombozi wetu baada ya mpira kuondoka katika miguu ya Samatta. Hata hivyo, kinachotokea kwa sasa sio kitu ambacho tulipenda kuona. Tulitaka Kelvin awashe moto pale pale na tumuone Ligi ya Mabingwa au Europa kama ambavyo Samatta alifanya.


Na sasa ameangukia Denmark. Nawafahamu wachezaji wengi ambao waliachwa na timu moja lakini wakaamka na kujipangusa vumbi kabla ya kuamkia kwingine na kuwa wachezaji hatari. Labda Kelvin angesoma vitabu vya wachezaji hao na kujaribu kujua walifanyaje. Wengine waliachwa katika umri mkubwa na wengine waliachwa katika umri mdogo.


Ajiambie wazi kwamba ameachwa kwa sababu hakuuzwa na Genk hawakuona umuhimu wa kuongeza mkataba wake. Ajiambie mwenyewe ni wapi amekosea au anakosea. Umri wa kurekebisha mambo bado anao. Umri wa kurekebisha tabia bado anao. Mpira upo katika mikono yake. Taifa linampenda na linamuamini. Akicheza kwa ajili ya taifa atafuata nyayo. Samatta alicheza kwa ajili ya taifa zaidi kwa sababu alijua kiu yetu. Alijua tulitaka siku moja Mtanzania aheshimiwe Ulaya na kweli akasababisha itokee.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad