KUMEKUCHA: DC Ubungo Kuwalipa Makahaba Bilioni 36



Dar es Salaam. Sakata la ukamataji wanawake 36, wanaodaiwa kujihusisha na biashara ya ukahaba limechukua sura mpya, baada ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo (DC), Hassan Bomboko kupewa notisi ya kuwalipa Sh36 bilioni.

Notisi hiyo ya siku 14 inayoanza leo Alhamisi, Juni 20, 2024, ambayo Mwananchi Digital imeiona, inalenga kuwalipa watuhumiwa hao 36 wanaodai wamedhalilishwa kwa kuwaita ‘Dada Poa’ na kuwaweka rumande kwa zaidi ya siku tano kinyume na sheria.

Notisi hiyo imeandikwa na wakili wao kutoka tasisi ya Stalwart, Peter Madeleka ambaye amethibitisha kwamba tayari wameshaiwasilisha kwa kiongozi huyo.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi, DC Bomboko amesema hadi saa 5:48 asubuhi leo alikuwa hajapokea notisi hiyo inayoelezwa amepelekewa.“Sijapokea hiyo notisi. Muulizeni vizuri.” Alipotafutwa tena jioni hakupatikana.

Operesheni hiyo iliyoendeshwa na mkuu huyo wa wilaya, hivi karibuni, iliwakamata ‘makahaba’ hao katika maeneo ya Ubungo, River Side na Sinza, bado inavuta hisia za wengi mitandaoni wakieleza inaingilia faragha za watu na inakiuka haki za binadamu.

Baadhi ya wanaharakati za haki za wanawake wamekosoa operesheni hiyo wakisema inakiuka haki za binadamu.

“Ni kweli nimemuandikia notisi ya siku 14, kwa sababu katika kesi ya madai hatua ya kwanza ni kumuandikia nia ya kushtaki mtu unayemdai. Siku hizo 14 zinaanzia leo baada ya kupokea na kutakiwa kuwalipa wateja wangu Sh36 bilioni kwa kuwadhalilisha,” amesema.

Katika maelezo yake, Wakili Madeleka amesema baada ya kupokewa notisi hiyo, kisheria anapaswa aijibu na asipokubali kuwalipa wateja wake kiasi hicho ndani ya muda huo wanakusudia kwenda mahakamani kufungua kesi.


“Wateja wangu wamekamatwa na mkuu wa wilaya kinyume na sheria na wamekaa mahabusu ya polisi Mburahati kwa zaidi ya siku tano wakituhumiwa kufanya ukahaba, lakini hawajafikishwa mahakamani kuthibitishwa kama wanafanya ukahaba, ila ni uonevu uliofanyika,” alisema.

Amesema wateja wake hao, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) alishindwa kuwafikisha mahakamani na kuishia kuwapeleka ofisini kwake na baadaye walichukuliwa na Polisi kabla ya kuachiwa.

Baada ya Bomboko kukataa kuwa hajapoteka notisi hiyo, Mwananchi ilimrejea tena Wakili Madeleka saa 6 mchana ambaye katika majibu yake amesema “Ndiyo maoni yake.”


Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akiwa kwenye maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, amemkingia kifua Bomboko juu ya mijadala inayoendelea katika mitandao ya kijamii ya kuikosoa operesheni aliyoifanya ya ukamataji huo.

Chalamila amesema amepita katika mitandao ya kijamii na kuona lawama zikitolewa kwa kitendo kilichifanywa na mkuu wa wilaya ya Ubungo ya ukamataji dada poa na kaka poa.

“Sasa kupitia siku hii ya mtoto wa Afrika naomba kwa uchache wa meneno na ukali mkubwa sana nifafanue yafuatayo. Katika mijadala ya watoto wameonyesha ni muhimu kupata malezi ya wazazi, ila ni fedheha kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika kutafsiri maisha ya kawaida kwa mama au baba kujiuza muda mwingi wa maisha na kusahau malezi ya watoto,” amesema Chalamila.

Amesema kilichofanyika kwa sasa ni kuanza kubadilisha mitazamo ya watu, huku ndani ya halmashauri tayari zikianza kuandaa mpango maalumu wa kutoa mikopo itakayowasaidia wenye mawazo ya kuuza miili na kufanya vitendo ambavyo haviendani na tamaduni kuanza biashara ambazo zina mwangwi wa watoto kuiga kutoka kwa wazazi.

Alionya vitendo vya kushabikia alichokiita ujinga ambao hayupo tayari kuuchekea, huku akizitaka taasisi zisizokuwa za kiserikali kutambua kuwa watoto waliopo hawana baba mwingine, bali baba yao ni Afrika itakayowalea kuwa viongozi bora.

Amesema wanaohisi kinamama hao wamedhalilishwa, amesema hawakudhalilishwa, kwani hakuna aliyevuliwa nguo bali walijivua wenyewe.

“Hakuna hata mama mmoja aliyefanyiwa vitendo hivyo, bali wakichukuliwa kama walivyovaa wenyewe, wakiwa wamekaa hadharani kwa watu wenyewe na kupelekwa mahali ambapo ili isiwe aibu kwa watoto wanaokwenda shuleni alfajiri,” amesema Chalamila.

Amesema siku ya mkesha wa sikukuu ya Idd, mtoto wa miaka minne alilawitiwa nyumbani kwao akiwa peke yake baada ya wazazi kutoka, huku mwingine wa miaka tisa akibakwa.

Amesema vyombo vya dola vinawafuatilia waliofanya vitendo hivyo, huku watoto wakifuatiliwa afya zao ili wawe sawa licha ya kuwa tayari wameathiriwa kisaikolojia.

“Stori hizi ukizisikiliza vizuri inatuamsha ari ya baba na mama kuwa wapenzi wakubwa wa melezi kwa watoto wetu na kamwe tusiwe mashabiki wa vitendo vinavyodhalilisha utu wa mwanamke, utu wa mtoto, au utu wa raia,” amesema Chalamila.

Amesema mtoto ni mtaji wa makuzi ya Taifa la baadaye, huku akisema kama katika biashara mtu anawekeza kwa ajili ya fahari ya uzee, ni wakati wa kuwekeza kwa watoto kama fahari ya Taifa la baadaye.

Amesema hilo limfanye kila mtu kutokubali mtoto aharibiwe, atengwe, akosewe heshima, avunjiwe utu bali kufanya matendo mema na mazuri ambayo kila mtu atatamani kuiga matendo ya baba na mama.

“Baadhi ya watoto wa kidato cha kwanza na pili waliokamatwa katika maeneo wakiwa wanajiuza walisema wameiga tabia za mama na baba zao,” amesema Chalamila.

Hata hivyo, mwanaharakati wa haki za binadamu, Dk Hellen Kijo Bisimba amesema kinachofanyika ni kuingilia faragha za watu kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

“Kama lengo ni kulinda maadili, hata kuingilia faragha ya watu ni kosa kisheria,” amesema Dk Bisimba alipozungumza na Mwananchi.

Akifafanua zaidi, Dk Bisimba amesema sheria zina utata katika kudhibiti biashara ya ukahaba.

“Sheria ya Kanuni ya Adhabu inasema mtu anayetumia mapato yatokanayo na ukahaba ndiye anayefanya kosa. Kwa nini wanaonunua madada poa wasiwe na kosa? Kama mwanamke anauza mwili, maana yake yupo mnunuzi. Unajuaje kwamba huyu anajiuza? Maana wengine ni wapita njia tu?” amehoji.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad