Mahakama Yaionya Serikali Kesi ya Makahaba


Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive imeionya Jamhuri (upande wa mashtaka) katika kesi ya ukahaba inayowakabili washtakiwa watano mahakamani hapo, kwa kushindwa kutekeleza amri yake ya kuwapeleka mahakamani mashahidi wengi baada ya shahidi aliyetarajiwa kudaiwa kuwa mgonjwa.

Hata hivyo, shahidi huyo alifika mahakamani akisaidiwa kutembea kwa kushikiliwa, akitembea kwa kujikokota huku akionesha kusikia maumivu, uliibuka mvutano mkali baada ya mawakili wa utetezi katika kesi hiyo kupinga taarifa za ugonjwa wake, wakidai kuwa huyo si mgonjwa, huku wakitaka uthibitisho.

Mahakama katika uamuzi wake pia imewataka waendesha mashtaka wa kesi hiyo kuwasilisha mahakamani ushahidi unaothibitisha ugonjwa wa shahidi huyo pamoja na wa mashahidi wengine ambao walidai kuwa wamepata dharura na kwamba wana kazi maalum, ambayo hata hivyo hawakuitaja.

Onyo hilo kwa upande wa mashtaka limetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo anayesikiliza kesi hiyo, Rachael Kasebele, leo Ijumaa Juni 28, 2024.

"Jana walitwambia shahidi ni mgonjwa, tulitarajia leo atoe ushahidi au aseme kwa nini ameshindwa. Kwa hiyo huyu anayetumwa atuletee vyeti vya matibabu, kwa kumwangalia tu haitoshelezi, sasa waende hospitali watuletee vyeti,” amesema hakimu Kasebele akiuelekeza upande wa mashtaka na kuongeza:

“Kuhusu hao mnaosema wamekwenda kwenye kazi maalumu mtu akienda kwenye kazi lazima kuna notification (taarifa), kwa hiyo lazima ushahidi upo, tunauhitaji huo ushahidi na hilo mlifanye leo, ikishindika leo wanapokuja waje na uthibitisho siyo maneno matupu tu.

Amesema kuwa kama maelekezo hayo hayatatekelezwa mahakama itaona kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kutimiza wajibu wake na itaweza kutoa uamuzi.

Kuhusiana waendesha mashtaka hao kuwa na kesi kwenye mahakama nyingine amewataka pia kuwasilisha uthibitisho huo na kwamba kama hakuna uthibitisho huo Mahakama inapanga tarehe yake yenyewe.


“Kwa hiyo tunapanga kuendelea Jumanne Julai 2, 2024 kuanzia saa 3. Upande wa mashtaka kama mnapata changamoto ya mashahidi bado mna mashahidi 8 labda ukitoa huyu mgonjwa mnao saba hawawezi kuwa wamesafiri wote. Kwa hiyo tarehe hiyo leteni mashahidi hatutasikiliza excuse (udhuru) yeyote. mzingatie wajibu wenu.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya jinai namba 17277/2024 ni Mariam Yusufu Mkinde (25) mkazi wa Magomeni, Mwazani Nassoro (25) mkazi wa Kigogo, Mwanaidi Salum (25) mkazi wa Mabibo, Faudhia Hassan (35) mkazi wa Ubungo na Tatu Omary (40) mkazi wa Ubungo.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka moja la kufanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa ajili ya kufanya umalaya kinyume na kifungu cha 176 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 Marejeo ya mwaka 2022.


Wanadaiwa kuwa Juni 17, eneo la Manzese Tiptop, wilayani Ubungo, Dar es Salaam, walikutwa wakifanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa kusimama hadharani, wakiwa wamevaa mavazi yasiyo ya heshima kwa lengo la kufanya umalaya.

Kesi hiyo ambayo iko katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka ilipangwa kuendelea leo kwa shahidi wa tatu, kati ya mashahidi 10 wanaotarajiwa kuitwa mahakamani kutoa ushahidi.

Hata hivyo, mahakama haikuweza kuendelea na usikilizwaji huo kutokana na upande wa mashtaka kukosa shahidi na hivyo kuilazimu kuiahirisha, huku ikitoa maelekezo yenye onyo ndani yake kwa upande wa mashtaka.

Kabla ya maelekezo hayo ya mahakama kuliibuka malumbano ya hoja za kisheria baina ya mawakili wa pande zote, waendesha mashtaka ambao ni mawakili wa Serikali na mawakili wa utetezi, Peter Madeleka, Jebra Kambole na Maria Mushi, kuhusu mashahidi hao wa Jamhuri.

Leo kesi hiyo ilipoitwa, Wakili Mafuru ameieleza mahakama kuwa walikuwa na shahidi mmoja lakini bado hali yake ya kiafya haijawa nzuri kiasi cha kuweza kuendelea na jukumu hilo.

Amesema kuwa baada ya kuwasiliana naye asubuhi imeonekana kuwa bado hali yake si nzuri na kwamba alitaka kwenda hospitali lakini wakamtaka afike mahakama kwanza ili mahakama imuone.

Shahidi huyo ambaye ni mwanamke amefika mbele ya mahakama akiwa anatembea kwa kujikokota, akisaidiwa na wakili mmoja wa Serikali, huku akionesha hali ya kuugulia maumivu na kuketi kwenye benchi ambako aliendelea kujikunjakunja na kuinama kuashiria kuugulia maumivu.

Kutokana na hali hiyo, wakili Mafuru ameioma mahakama hiyo iahirishe kesi hiyo mpaka Jumatano, Julai 3, 2024 akidai kuwa Jumatatu atakuwa kwenye kesi nyingine ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu na kwamba Jumanne atakuwa na kesi nyingine Mahakama ya Rufani.

Wakili Mafuru amesema kuwa mashahidi wengine wako kwenye kazi maalumu na mpaka sasa bado hawajarejwa kwa hiyo, kisha akaomba mahakama itoe hati za wito wa kufika mahakamani kutoa ushahidi.

Akijibu hoja hizo za upande wa mashtaka, wakili Madeleka amepinga taarifa za ugonjwa wa shahidi huyo akisema kuwa mahakama haina uwezo wa kubaini ugonjwa kwa macho badala yake akata upande wa mashtaka uwasilishe ushahidi wa vyeti vya matibabu.

“Mheshimiwa jana tuliambiwa kuwa kulikuwa na mashahidi wawili tukaambiwa shahidi mwingine amepata shida ya kiafya. Lakini mahakama yako haina uwezo wa kubaini mgonjwa kwa macho,” amesema wakili Madeleka na kuongeza:

“Huyu shahidi alianza kuumwa jana na akaenda hospitalini, kwa hiyo tulitegemea leo angeleta vyeti vya ugonjwa. Kwa hiyo shahidi waliyemleta leo siyo mgonjwa kwa maoni yetu isipokuwa kama tutapata uthibitisho kutoka kwenye taasisi yenye mamlaka," amesisitiza wakili Madeleka.

Amesema kuwa hata hivyo upande wa mashtaka hauna shahidi huyo mmoja tu na kwamba mahakama iklishatoa amri kuwa wapeleke shahidi zaidi ya mmoja.

Wakili Madeleka amesema kuwa mahakama haifanyi kazi kwa kwa kuwasikiliza mashahidi kwamba wana kazi maalumu ambayo ni taarifa za siri na kwamba inachotakiwa kuona ni mashahidi mahakamani.

Kuhusu maelezo ya wakili Mafuru kuwa watakuwa na kesi nyingine amesema kuwa washtakiwa hao wameshtakiwa na Jamhuri na si wakili wa Serikali na kwamba Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambaye ndiye ana dhamana ya kuwashtaki watu ofisi yake ina waendesha mashtaka wengi.

“Kwa hiyo tunaomba mahakama yako ione kwamba upande wa mashtaka hawana mashahidi wafunge kesi yao na mahakama itoe uamuzi kama wana kesi ya kujibu au la maana hata dharura na sisi tunazo.

Hata hivyo wakili Mafuru amesema kuwa wao Jamhuri hawajashindwa kupeleka mashahidi na kwamba mashahidi wapo na watawapeleka.

“Ni kweli niliieleza Mahakama yako jana kwamba shahidi ameugua na amekwenda kupatiwa matibabu. Amefika hapa nimemuomba vyeti akasema alikuwa na dawa nyumbani ndizo alizotumia na leo ndo alipanga kwenda hospitali lakini tuliheshimu amri yako tumemuita aje hapa imuone”, amesema wakili Mafuru.

Kuhusu ofisi ya DPP kuwa na mawakili wengi, amesema kuwa ni kweli wapo wengi lakini akasema kuwa si kwamba wanakuwa wamekaat tu bali nao wana majukumu mengine.

Wakili Mafuru amesema kuwa kwa sasa ambapo kuna vikao maalumu vya mahakama kwa lengo la kupunguza mrundikano wa mashauri ya muda mrefu, hata wao mawakili wa Serikali ni wachache.

Hivyo ameiomba mahakama itumie busara yake iwape nafasi shahidi aende hospitali.

Kuhusu hoja ya mahakama kuamuru wafunge kesi, amesema kuwa hata wakili mwenzake huyo wa utetezi anajua kuwa mahakama haina mamlaka hayo kwamba ni upande wa mshatka wenyewe ndio unaweza kufunga kesi yake yenyewe.

Hata hivyo wakili Madeleka amepinga hoja ya shahidi huyo mgonjwa kumeza dawa tu nyumbani akisema kuwa upande wa mashtaka wanataka kuitumia kama kichaka tu wasiwasilishe uthibitisho mahakamani.

“Katika common sense (ufahamu wa kawaida) mgonjwa anakwenda hospitali ndo anaandikiwa dawa, kwa hiyo huyo mgonjwa haumwi na hata leo haumwi,” amesisitiza wakili Madeleka.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad