Makada Wanne Chadema Wajitosa Nafasi ya Lema Kaskazini

Makada Wanne Chadema Wajitosa Nafasi ya Lema Kaskazini

Siku nne baada ya Mwenyekiti wa Chadema anayemaliza muda wake Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema kutangaza kutogombea tena nafasi hiyo, baadhi ya makada wamejitokeza na kutangaza nia ya kurithi mikoba yake.


Baadhi ya makada hao ambao Mwananchi iliwahi kuwatafuta Aprili mwaka huu, kujua kama wangegombea lakini wakasita kutoa jibu la moja kwa moja, leo Jumapili Juni 2, 2024 wameweka wazi nia hiyo ya kuutaka ubosi wa Kanda ya Kaskazini.


Makada ni pamoja na mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Michael Kilawila, Gervas Mgonja, mwenyekiti wa kamati ya fedha ya kanda hiyo na Grace Kiwelu, mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho na Yosepher Komba ambaye ni makamu wa mwenyekiti wa kanda hiyo kwa sasa.


Mei 30, 2024 Lema ambaye ni mjumbe wa kamati kuu aliandika kupitia akaunti yake ya mtandao wa X zamani Twitter akiweka msimamo wa kutogombea tena nafasi hiyo kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.


Hata hivyo, hatua hiyo ilipokelewa kwa hisia tofauti na makada wa Chadema, baadhi wakisema watamshawishi agombea tena nafasi hiyo kwa sababu bado anahitajika na wengine wakisema wanaheshimu uamuzi wake na wanampongeza kwa uongozi wake wa miaka mitano.


Leo Jumapili Juni 2, 2024 Mwananchi limezungumza na baadhi ya makada na wameonyesha nia ya kuunyemelea uenyekiti wa Kanda ya Kaskazini yenye mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara.


“Nimejipima, nimejiona ninatosha kuwania uenyekiti wa kanda ya kaskazini, sasa nasubiri utaratibu wa chama kuhusu kufungua pazia la kuchukua na kurejesha fomu. Muda sahihi ukifika nitatoa sababu kwa nini nagombea na vipaumbele vyangu," amesema Kiwelu, mbunge wa zamani wa viti maalumu.


Naye Komba ambaye pia ni mbunge wa zamani wa viti maalumu, amesema suala la kugombea nafasi ndani ya chama hicho, amesema "wakati ukifika nia yangu itakuwa wazi kuhusu suala hili ila nia ipo."


Alipoulizwa kwamba yeye ni makamu mwenyekiti na je, anahitaji kupanda, amejibu, "sio jambo baya, wapigakura na wanachama wa Kaskazini wakiniunga mkono na kupenda kazi nilizozifanya nipo tayari kuwasikiliza."


Kwa upande wake, Mgonja amesema anataka kuwania kiti hicho, na kwa sasa anasubiri mwongozo wa chama kuhusu taratibu za uchaguzi ikiwemo kufunguliwa kwa milango ya kuchukua fomu za mchakato huo.


"Nina uwezo na sifa, nataka kuleta mabadiliko ya umoja na mshikamano ndani ya Kaskazini hasa kuelekea chaguzi za serikali za mitaa, vijiji na vitongoji na Uchaguzi Mkuu 2025,” amesema Mgonja.


Kwa upande wake Kilawila ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa Halmashauri ya Moshi Vijijini, amesema amesikia baadhi ya makada wanataka kugombea nafasi hiyo, bado anafanya utafiti kabla ya kujitosa rasmi.


"Ndani ya siku tatu zijazo nitaweka wazi, unajua huu ni uchaguzi, sasa unaweza ukaingia kichwa kichwa ukapigwa za uso, nafanya utafiti wangu kwanza kabla sijafanya uamuzi," amesema.


Endapo wagombea hao wakichukua fomu huenda uchaguzi wa Kaskazini ukawa na ushindani kama iliyokuwa katika kanda za Nyasa, Serengeti na Magharibi ambapo wagombea walipishana kwa kura chache, kama anavyoeleza Gabriel Mwang'onda,mchambuzi wa masuala ya kisiasa.


"Hawa wote wana nguvu, ukizungumzia Kiwelu na Kilawila sio watu wadogo lakini yote haya ni ukomavu wa kisiasa unaojengeka ndani ya Chadema, lakini ni faida pia ya ndani ya chama, uzoefu unaendelea kuwa mkubwa na ushindani unakieneza chama chao," amesema.


Kwa sasa Kanda ya Kaskazini ipo katika uchaguzi kwenye ngazi ya kata, majimbo na wilaya na fomu zilianza kutolewa Juni 2 hadi 10 kwa majimbo ya Arusha Mjini na Babati Mjini mkoani Manyara.


Wakati huohuo, shughuli nyingine pevu itakuwa katika Kanda ya Pwani inayojumuisha mikoa ya Dar es Salaam (yenye mikoa ya Chadema mitano) na Pwani ambapo vigogo wawili Boniface Jacob, ambaye ni meya wa zamani wa Ubungo na Henry Kilewo, mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kinondoni wametangaza nia ya kuutaka uenyekiti wa kanda hiyo, muda ukifika.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad