UONGOZI wa Yanga chini ya Injinia Hersi Said umedhamiria kufanya mabalaa kwenye usajili wa dirisha hili linalokaribia ufungulia wiki ijayo June 15, ambapo majina yote wanayoyataka tayari yapo mezani na kilichobaki ni kutambulishwa tu.
Rais wa Klabu hiyo, Injinia Hersi, amesema pamoja kuwa na kikosi kizuri, bora na imara, bado wataongeza baadhi ya wachezaji wachache, lakini wenye viwango vya hali ya juu kama waliopo au zaidi kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi kuelekea kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Alisema kama kawaida yao, wapo makini katika suala ya usajili, hivyo kuwataka wanachama na mashabiki wa Yanga wasiwe na wasiwasi.
“Tumedhamiria kuwa na kikosi bora zaidi kitakachotikisa Afrika, kwa hiyo tutafanya usajili wa wachezaji watakaokuwa na faida ndani ya timu na kikubwa tunawekeza kwenye michuano ya Afrika, ili tufanye vyema huko tunalazimika kufanya usajili utakaoongeza nguvu ya kututoa hapa tulipo na kufikia kule tunapotarajia, tunataka kuwa na akina pamome au Aziz Ki wengi ndani ya kikosi” alisema Eng Hersi.
Mbali na hayo alisema kwa sasa wanaendelea kuwaongeza mikataba wachezaji ambao wanaona wanafaa kuendelea nao kwa matakwa ya benchi la ufundi, huku wale ambao wataonekana hawakidhi mahitaji ya klabu watawapisha wapya kuendelea pale walipoishia.
Alisema lengo la uongozi ni kuona timu hiyo inafanya vizuri zaidi kwenye mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo tayari wameshakata tiketi ya kushiriki baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
“msimu hyuu tumeishia robo fainali japo malengo yetu yalikuwa hatua ya makundi, msimu ujao tunataka kufika mbali zaidi, na kuw amiongoni mwa timu kubwa na tishio Afrika, hii ndio sababu tunafanya usajili wa maana na wenye tija,” alisema Hersi.
Yanga pamoja na kutwaa Ubingwa wa Tanzania Bara mara ya tatu msimu huu, lakini imekuwa na kiwango bora na msimu wenye mafanikio, ambapo mbali na ubingwa huo, imetwaa Kombe la FA, pamoja na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikitolewa kwa mbinde na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwenye hatua hiyo.