Mwekezaji wa klabu ya Simba Mohammed Dewji, amezuia uwezekano wa beki Joyce Lomalisa kutua Msimbazi lakini amemuita kipa Ayoub Lakred kwa ajili ya mazungumzo nyumbani kwake nchini Dubai.
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba Ayoub ambaye mkataba wake na Simba imemalizika amewaambia viongozi wa Simba kwamba ana ofa mbili kutoka klabu ya Pyramids na Zamalek zote za Misri.
Lakini Mo akawaambia kwamba atapambana mpaka dakika ya mwisho kuhakikisha kwamba kipa huyo raia wa Morocco anaongeza mkataba klabuni hapo kwani tayari gari lilishawaka na ni ngumu kupata kipa wa aina yake sokoni kirahisi.
Mo anaamini kwamba ni ngumu kupata mbadala wa Lakred kwa haraka haswa ukizingatia kwamba kipa mzoefu, Aishi Manula bado hajakaa sawa kutokana na majeraha yanayomkabili ambayo yamemweka nje karibu msimu mzima.
Ayoub ambaye ni raia wa Morocco amekuwa na msimu mzuri ndani ya Simba ingawa katika siku za hivi karibuni ilielezwa kwamba anataka kuondoka hata kama hajapata ofa hizo za Misri.
Lakini habari za ndani zinasema kwamba Mo atakutana naye wiki hii na kumaliza dili lake juu kwa juu kwamba uwezekano wa kusalia Msimbazi ni mkubwa kwani ndiye aliyehusika kumleta hapo awali.
“Ayoub alishasema anataka kuondoka, lakini hajaanga rasmi, baada ya yeye kusema hivyo, Mohammed Dewji amepewa taarifa na kugomea kipa huyo kuondoka ambapo amemwita Dubai ili azungumze naye na ikiwezekana asalie ingawa lazima kifanyike kitu cha ziada,” kilisema chanzo hicho.
Habari zinasema pia tajiri huyo amefuta uwezekano wa Lomalisa wa Yanga kusajiliwa Simba baada ya kutilia shaka kiwango cha staa huyo mwenye sintofahamu ya kuondoka Jangwani.
Lakini ikadaiwa pia kuwa hataki kufanya kazi na wachezaji wa DR Congo kwa vile wana usumbufu mwingi nje ya uwanja.
Habari za ndani ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba Lomalisa kuna uwezekano asiongezewa mkataba Yanga baada ya kutokea mzozo wa kimasilahi kwani anataka aongezewe mshahara kutoka Sh10Milioni mpaka Sh18Milioni.
Habari zinasema Yanga bado wanajadiliana kuhusu Lomalisa ambaye juzi alikwenda kambini kubeba vitu vyake vyote huku akisikilizia hatma yake endapo simu ya kiongozi wa Simba ikimrudia atakuwa ametimiza malengo yake.
Ingawa kuna mawasiliano yanaendelea baina ya wasimamizi wake na watu wa Simba, lakini huenda msimamo wa Mo juu ya wachezaji wa DR Congo huenda ukatibua dili hilo kwani inadaiwa ameweka msimamo mkali ambao ni ngumu kuubadili haswa kutokana na mwenendo wa timu na kile kinachoendelea klabuni hapo.
Simba imepania kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake cha msimu huu na kuibuka na sura nyingi mpya kwani mwenendo umekuwa mbovu na wanaona kwamba unazidi kuwashushia thamani yao.
Tayari vigogo kadhaa wameshajiuzulu na bado fukuto linaendelea ndani kwa ndani huku ikielezwa kuwa hata mchakato wa kupata kocha mpya umesimama kwa kuwa hakuna anayefahamu hatima yake klabuni hapo.
Kwenye ujumbe wake kwa mashabiki na wanachama wa Simba, Mo aliahidi kufanya mabadiliko makubwa kuanzia kwenye benchi la ufundi mpaka uwanjani ili kurejesha pira biriani ambalo limepotea Msimbazi katika misimu ya hivikaribuni.
Ingawa awali Mwanaspoti liliambiwa kwamba msimamo wake ulikuwa ni kuhakikisha anafagia bodi yote ukiwemo upande wa wanachama lakini sasa amepiga moyo konde na kusema kwamba atafanya kazi na viongozi waliopo klabuni baada ya wale wa upande wake kujiuzulu akiwemo Mwenyekiti wa Bodi, Salim Abdallah.
Tayari Mwanaspoti linajua kwamba MO amefumua jopo la usajili na kuongeza vichwa vinne ambavyo anaamini vitaivusha Simba. Hao ni Mulamu Ng’ambi, Kassim Dewji na Cresentius Magori ambao wanaaminika na wanasimba kwamba uzoefu wao ndani ya klabu na mapambano ya soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla.
DJUMA SHABAAN NA BALEKE
Mwanaspoti limejiridhisha kwamba aliyekuwa beki wa Yanga, Mkongomani Djuma Shabaan ‘Soja ya Bemba’ yupo jijini Dar es Salaam akihusishwa na Coastal Union ya Tanga.
Siyo huyo tu, Jean Baleke anayecheza Libya yupo pia Dar es Salaam akiangalia uwezekano wa kupata dili la haraka kwani hataki kuendelea kucheza aliko kutokana na sababu za kiusalama lakini amewaambia marafiki zake pia kwamba ligi ya kule ‘haina vaibu’ alilozowea.
Wanaomsimamia wanamhusisha na Yanga na Azam ingawa habari za ndani kabisa ambazo Mwanaspoti imejiridhisha nazo ni kwamba hakuna klabu yoyote kati ya hizo iliyokuwa na mpango na staa huyo wa zamani wa Simba.