Mkazi wa Kijiji cha Nyamburi Kata ya Sedeco, wilayani Serengeti mkoani Mara, Nyaikongoro Mwita (34), amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na kulipa faini ya Sh 2,000,000 kosa la shambulio la kudhuru mwili akidaiwa kumpiga mke wake Elizabeth Wambura(21) na kumlisha kinyesi.
Katika hukumu ya rufaa namba 4270/2024 imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Serengeti, Jacob Ndira baada ya upande wa Jamhuri kupitia Ofisi ya mashtaka Wilaya ya Serengeti uliowakilishwa Thryphone Makosa kupinga uamuzi uliotolewa Februari 5, 2024 na mahakama ya mwanzo Mugumu ya kumwachia huru mtuhumiwa.
Hakimu Ndira aliiambia mahakama kuwa wamepitia maelezo na ushahidi wote ambao ulitolewa katika kesi ya msingi namba 13/2024 iliyosikilizwa na kuamriwa katika mahakama ya Mwanzo Mugumu na kubaini kuwa uamuzi katika kesi hiyo haukuwa sahihi.
Amesema mshtakiwa atatumikia kifungo hicho cha mwaka mmoja na kulipa faini ya shilingi milioni 2 kwa kumsababishia madhara kutokana na kipigo hicho, huku milango ya Rufaa ikiwa wazi.
Mshtakiwa Nyaikongoro Mwita alipopewa nafasi ya kujitetea aliomba mahakama impunguzue adhabu kwa vile ana mke mwingine na watoto wote wanamtegemea .
Jamhuri ilikata rufaa kupinga hukumu ya kumwachia huru Mwita katika kesi ya jinai namba 13/2024 iliyosomwa Februari 5, mwaka huu na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Mugumu, Lordon Nanyaro, kufuatia upande wa mashtaka kushindwa kuwasilisha vielelezo ikiwamo PF.3, daktari aliyemtibu na Polisi waliofanya upelelezi.
Ilidaiwa mshtakiwa Mwita alitenda kosa hilo Novemba 21, 2023 usiku na Novemba 23, 2023 mlalamikaji alifika polisi na kupewa PF.3 na kwenda kutibiwa hospitali ya Wilaya Kibeyo, Desemba 30 mwaka jana na Mwita alikamatwa na polisi na kufikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Januari 3,2024.