Ni suala la muda tu, Prince Dube 'Mwana wa Mfalme' atatambulishwa kuwa mchezaji wa Yanga baada ya kuachana na Azam Fc
Jana Azam Fc walimkabidhi Dube 'release letter' baada ya kutimiza masharti aliyowekewa ambayo ni kurudisha fedha aliyokuwa amelipwa na Azam Fc kwa ajili ya kuongeza mkataba
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ndio iliyomaliza utata wa sakata la mkataba wa Dube ambapo awali Azam Fc walikuwa wakidai ana mkataba na klabu hiyo mpaka mwaka 2026
Kamati ilibaini mkataba ambao Azam Fc wanadai Dube alisaini ambao ungemfanya adumu katika klabu hiyo mpaka 2026, haukuwa umesajiliwa katika mfumo wa usajili FIFA Connect na hivyo Dube kutakiwa arudishe fedha alizopewa na Azam Fc ili awe huru
Hicho ndicho kiilichotokea na sasa Dube ni mchezaji huru na anakwenda kujiunga na timu ya ndoto zake, Yanga
Safari ya Dube kun'goka Azam Fc ilianza mwezi March 2024 pale alipotangaza kuachana na timu hiyo kwa kile alichoeleza hafurahishwi vile timu hiyo inaendeshwa
Kuondoka kwa Dube katikati ya msimu hakutofautiani na tukio ambalo aliyekuwa kiungo wa Yanga Feisal Salum alifanya Disemba 2023
Unaweza kusema Wananchi wamejibu mapigo kwa kutumia njia ileile ambayo Azam Fc waliitumia kumn'goa Fei Toto Yanga
Wakati Fei Toto ametoroka Yanga, uongozi wa mabingwa hao wa nchi uliweka msimamo kwa kutaka taratibu zifuatwe ikiwa ni pamoja na kuitaka timu iliyokuwa ikimuhitaji Feisal ijitokeze lakini Azam Fc hawakufanya hivyo
Busara ikatumika kumruhusu Fei Toto kujiunga na Azam Fc baada ya ushauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Dk Samia Suluhu Hassan ambaye aliwataka viongozi wa Yanga kumaliza sakata la mchezaji huyo