Mzimu wa Baleke, Saido Unavyoipa Presha Simba

 

Mzimu wa Baleke, Saido Unavyoipa Presha Simba

Sima iko kwenye mchakato wa kutengeneza upya kikosi chake bora kitakachobeba matumaini ya kurudisha heshima ya klabu iliyolega kwa miaka mitatu sasa lakini ndani ya hilo itapambana kuzima presha ya mastaa wao wawili wa zamani walioacha rekodi ngumu.


Hesabu za Simba ni kama itatema mastaa wengi wa kigeni wasiopungua saba lakini eneo ambalo litawapa presha mabosi wa klabu hiyo wanaosimamia usajili ni safu ya ushambuliaji.


Mapema kupitia dirisha la usajili mdogo la msimu uliopita, Simba ilifanya uamuzi mgumu wa kumtema aliyekuwa mshambuliaji wake Jean Otto Baleke aliyekuwa kinara wa ufungaji kwa timu yao akifunga mara nane.


Wakati Simba ikiwa chini ya aliyekuwa kocha Abdelhak Benchikha aliyekuwa anataka mshambuliaji bora zaidi ya Baleke, mabosi wa wekundu hao wakasajili washambuliaji wawili Pa Omar Jobe na Freddy Kouablan.


Hata hivyo, washambuliaji hao wawili walishindwa kuzima rekodi hiyo ya Baleke wote wakifunga jumla ya mabao saba ambapo Jobe alifunga bao moja pekee huku Kouablan akifunga mabao sita.


Ujio wa washambuliaji hao bado haujaweza kukata kiu ya mashabiki wa Simba wakiona wawili hao walishindwa kuvaa viatu vya Baleke sawasawa kwa mabao yao wote wawili kwa pamoja ukiyajumlisha wakishindwa hata kumfikia Mkongomani huyo.


Kabla ya hilo halijatulia Simba imefanya uamuzi mwingine mgumu kwa kumuacha Said Ntibazonkiza 'Saido' ambaye baada ya kuondoka Baleke akaibuka kuwa kinara wa mabao ndani ya wekundu hao akifunga jumla ya mabao 10.


Ndani ya misimu miwili Saido aliibeba Simba akitangulia kuwa mfungaji bora wa ligi msimu wa juzi akifunga mabao 17 sawa na aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele.


Msimu ulipita ingawa mkongwe huyo alishindwa kuwa mfungaji bora wa ligi lakini akaibuka kinara wa mabao ndani ya timu yake huku akiwa na tofauti ya bao mawili dhidi ya Baleke.


Kwenye mabao 10 aliyofunga Saido amefunga mabao saba ya mpira iliyokufa ambapo sita ni penalti na moja na la frii-kiki, huku mabao ya mashambulizi ya wazi yakiwa matatu pekee tofauti na Baleke akifunga mabao tisa yote ya kumalizia kupitia mashambulizi ya wazi ya timu hiyo.


Simba iko mezani ikitaka kuachana na Jobe kwa kumtoa kwa mkopo au kumsitishia mkataba wa mshambuliaji huyo ambaye mashabiki wengi wa Simba hawajaonyesha kuridhishwa na kile anachokifanya uwanjani tangu asajiliwe.


Mtihani wa mabosi wa Simba unabaki kuwa nani atakuja kuwasahaulisha mashabiki wa Simba juu ya ubutu wa washambuliaji hao kupitia dirisha hili la usajili mkubwa lililofunguliwa kuanzia Juni 15,2024.


Uchunguzi wa Mwanaspoti unaonyesha kuwa wala tatizo la Simba sio utengenezwaji wa nafasi, shida kubwa ni ubora wa wamaliziaji ambao wameifanya timu hiyo kuwa na utumiaji mdogo wa nafasi inazotengeneza.


Simba ilitawala mechi dhidi ya mabingwa wa Afrika, Al Ahly kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na ikapiga mashuti 19 huku saba yakilenga lango, lakini ililala 1-0 kwa shuti pekee la Ahly lililolenga lango. Simba ilitawala mechi kwa asilimia 62 dhidi ya 38 za Al Ahly. Simba ilipiga kona 11 dhidi ya kona 4 tu za Al Ahly.


Dhidi ya Ahly, moja ya mifano mingi ambayo Simba ilitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini haikushinda mechi hizo.


Huu ni uthibitisho kwamba, Simba inahitaji kuboresha eneo la umaliziaji ili kurejea katika makali yake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad