Rais Samia Anaupiga Mwingi, Sababu Zilizopelekea Kutunukiwa Shahada ya Udaktari Hizi Hapa

 

Rais Samia Anaupiga Mwingi, Sababu Zilizopelekea Kutunukiwa Shahada ya Udaktari Hizi Hapa

Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga Korea (KAU), kimeeleza sababu za kumtunuku Rais Samia Suluhu Hassan Shahada ya Udaktari wa Heshima (Honoris Causa) kuwa ni kazi kubwa iliyofanyika katika kuimarisha usafiri wa anga nchini na uongozi wenye mabadiliko ya sera na kimantiki.


Kimesema R nne anazozisimamia ambazo ni Reconciliation (Maridhiano), Resiliency (Ustahamilivu), Reforms (Mabadiliko) and Rebuilding (Kujenga Upya), zimeiwezesha Tanzania kupiga hatua katika njanja mbalimbali.


Rais wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Korea, Dk. Hee Young Hurr, akizungumza jana kabla ya Samia kutunukiwa shahada hiyo, alisema ni Rais pekee mwanamke Afrika na mwanamke wa kwanza kwa nafasi hiyo Tanzania katika historia ya miaka 60 ya Tanzania ambaye alileta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii kwa kuwa na uongozi wa ushirikiano kipindi cha UVIKO- 19.


Alisema kupitia R nne, amelileta taifa pamoja na kuchangia mabadiliko na ustawi wa kijamii, huku akiwa kiongozi mashuhuri kwenye mabadiliko ya tabianchi na nishati safi ya kupikia kwa Afrika ambayo ni mafanikio makubwa kwenye sekta za afya, elimu, TEHAMA, usafiri wa anga, viwanda na miundombinu.


"Mafanikio haya ni kutokana na uongozi bora na kumfanya kujulikana kimataifa licha ya kuongoza kwa kipindi kifupi. Katika sekta ya anga kuna mabadiliko makubwa kwa vitendo hatua inayodhihirisha uongozi bora ambao umeibadili sekta ya anga kwa sasa,” alisema.


Pia alisema hatua kubwa alizochukua kiongozi na uongozi wenye kujali wengine, kurekodi filamu ya The Royal Tour ambayo vimesaidia kukuza utalii duniani, kuendeleza miundombinu ya viwanja vya ndege kwa kujenga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, Dodoma, utakaozinduliwa Desemba, mwakani.


Eneo lingine ni uwekezaji kwenye kujenga mifumo na nguvu kazi katika kuongeza idadi ya abiria na ndege za mizigo hatua zilizosaidia nchi kuwa na ndege 14 za abiria na moja ya mizigo, hivyo kufanya ongezeko la safari za ndani na nje ya nchi kama Dubai na China.


"Kwa kutambua uongozi wake, ari ya kipekee ya Rais Samia yenye mafanikio makubwa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga kimeamua kumtunukia shahada ya udaktari wa heshima,” alisema.


Akizungumza baada ya kutunukiwa shahada hiyo, Rais Samia alisema amepokea kwa hisia kubwa ya uwajibikaji na kujitolea kwa Watanzania na kwamba kwa msaada wao na watangulizi wake, hasa Hayati Dk. John Magufuli ambaye aliweka misingi ya ukuaji wa sekta ya usafiri wa anga, mafanikio yanaonekana sasa.


Alisema msingi uliowekwa na Magufuli umewezesha kuendelea na kufanya mabadiliko makubwa katika kuhakikisha Tanzania inasonga mbele na kwamba amejitolea kuhakikisha sekta ya anga inabaki kuwa chachu ya maendeleo na ustawi wa nchi.


Pia alikiomba chuo hicho kushirikiana na Tanzania katika kufundisha na kubadilishana maarifa na wataalamu wa sekta ya anga Tanzania.


Rais Samia alisema kwa sasa Tanzania inaunganika na viwanja 38 duniani na kwamba kuna nafasi kubwa ya muunganisho na maeneo mengi lakini kuna changamoto mbalimbali zinazozuia kuwa wa haraka wa sekta hiyo.


Kwa mujibu wa Rais Samia, sekta ya anga ya Tanzania kati mwaka 2021 hadi 2023 imekua kwa kuwa abiria wameongezeka kila mwaka kwa takriban asilimia 28 na idadi ya ndege zinazofanya safari za kimataifa zimeongezeka kutoka 26 hadi 33.


"Idadi ya wasafiri wa ndani imeongezeka kwa asilimia 26.5 baada ya UVIKO-19 kutoka abiria milioni tatu hadi milioni 3.8 kwa mwaka 2023. Nia ilikuwa kuwekeza kimkakati hasa katika kufufua Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na kuendeleza miundombinu, ikiwamo mfumo wa kujenga rada, kukarabati na kupanua viwanja vya ndege nchini kote,” alisema.


Alisema kabla mwaka 2016, ATCL ilikuwa na ndege moja inayofanya kazi na hadi Machi 2024, zimeongezeka ndege 14 za abiria na moja ya mizigo na kwamba ndege sita kati ya hizo, zimenunuliwa katika kipindi cha miaka mitatu ikiwamo ndege ya mizigo.


Aidha, alisema mtandao wake umepanuliwa kutoka maeneo 4 tu nchini hadi 24, ikiwamo safari katika miji minane Afrika na mitatu ya kimataifa (Guangzhou, Dubai na Mumbai).


Rais Samia alisema kufufua shirika hilo kumesaidia kuongeza mapato kutoka Sh. bilioni 23 mwaka 2016/17 hadi bilioni 380.4 mwaka 2022/23 huku soko la ATCL la safari za ndani likifika asilimia 53 kutoka asilimia 2.4 tu mwaka 2022/23. Pia idadi ya abiria imeongezeka kwa asilimia 42 kutoka milioni 4.8 mwaka 2015 hadi milioni 6.8 mwaka huu.


"Idadi ya marubani waliosajiliwa na wahandisi wa ndege imeongezeka kufikia 604 ikiwa ni ongezeko la asilimia 21 na wahandisi kufikia 76 ambao ni ongezeko la asilimia 181 mpaka mwisho wa mwaka 2023,” alisema.


Rais Samia alisema mchango katika sekta ya anga kwenye pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 0.9 mwaka 2018 hadi asilimia 2.5 mwaka 2023.


Tayari kiongozi huyo ana shahada tano za udaktari wa heshima baada ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha Jawaharial Nehru cha India na Chuo Kikuu cha Ankara, Uturuki, wote wakitambua mchango wake kwenye nyanja mbalimbali.


Rais Samia amehitimisha ziara rasmi ya siku mbili na leo anaanza ziara ya kikazi na atahudhuria mkutano wa wakuu wa nchi na serikali kati ya Korea na Afrika. Katika mkutano huo, atatoa maoni katika jopo la Kuimarisha Usalama wa Chakula na Madini.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad