“Huko nyuma, Mimi hela nilikuwa naipata ila muongozo nilikuwa sina, yaani mtu wa kunishika mkono na kunipa ushauri, hii hela ifanyi hiki na kile maana kuna kesho na kesho kutwa, hicho kitu ndicho nilikuwa sina, nilikikosa kabisa,” Karoli alisema.
Muhtasari
• Baadae alipata wazo la kuamua kujitosa katika kutumbuiza kwenye hafla ndogo ndogo ili kupata pesa na akajichanga hadi pale alipojenga miaka si mingi iliyopita.
SAIDA KAROLI.
Saida Karoli, mtunzi na muimbaji wa nyimbo za kiasili kutoka Tanzania ambaye alivuma kwa muda mrefu miaka ya nyuma amefunguka kuhusu baadhi ya mambo ambayo anayajutia katika maisha yake ya awali kimuziki.
Msanii huyo ambaye katika miaka ya hivi karibuni hasikiki tena alitafutwa na Global TV ya nchini humo na katika mahojiano ya kipekee, alieleza sababu zimemfanya kutosikika tena kwa nyimbo kama miaka ya nyuma.
Karoli alikiri kwamba alilazimika kuhama kutoka jiji kuu la kibiashara la Dar es Salaam na kurejea kwao Bukoba mkoani Kagera ambako amelazimika kujisatiti kwa maisha ya uhayawinde mradi siku zisonge.
Karoli alieleza kwamba licha ya kufanya vizuri kwa muda mrefu kimuziki akiwa jijini Dar es Salaam, hakuweza kujenga nyumba na baadae aliporudi Mwanza, alilazimika kukaa na wanawe kwenye vyumba vya kulala akilipia kwa siku.
Baadae alipata wazo la kuamua kujitosa katika kutumbuiza kwenye hafla ndogo ndogo ili kupata pesa na akajichanga hadi pale alipojenga miaka si mingi iliyopita.
“Dar nilikata tamaa nikarudi Mwanza na nilikuwa nafanya kazi na Wasukuma. Ilikuwa ni kazi ngumu sana ambapo hakuna hata nyumba ya kulala, ni pori hadi pori. Ile kazi mimi niliamua kujikaza ili nipate nyumba, nipate kiwanja na nijenge.”
“Nilijiuliza ninawezaje pata kiwanja nijenge nyumba ya kwangu, maana nimeenda Dar es Salaam miaka 9 na sijafanya kitu, ulipofika mwaka wa 10 nikaamua kufunganya na kurudi Mwanza. Hapa niliingia kwa gesti bubu nalipa 4k kila siku. Nikajiuliza nawezaje pata sehemu ya watoto wangu kutulia. Ilibidi nizame, nikajifunga kweli mkanda tumboni, sikujali hela yoyote, gemu nikapiga msimu mmoja nikajenga nyumba,” alieleza.
Karoli alifichua baada ya kujenga, hatimaye aliachana na kazi hizo za pesa ndogo kwa sababu aliona zinamshusha hadhi na kwa sasa amerejea tena jijini Dar es Salaam ambako watu wanathamini Sanaa ya mtu.
Akiulizwa kwa nini hakuweza kujenga siku za nyumba akiwa staa mkubwa na kusubiri mpaka kuja kufanya kazi za kushusha hadhi ili kujenga, Karoli alisema kwamba ni kutokuwa na usimamizi mzuri wa hela zake kulimpelekea kutowajibika kifedha.
“Huko nyuma, unajua kipato si tatizo, tatizo mtu wa kukushika mkono akakuongoza. Mimi hela nilikuwa naipata ila muongozo nilikuwa sina, yaani mtu wa kunishika mkono, ushauri, akaniongoza fanya hiki, fanya kile, usile hela hii, hii hela naishikilia sikupi ili tufanye hiki maana kuna kesho na kesho kutwa, hicho kitu ndicho nilikuwa sina, nilikikosa kabisa,” Karoli alisema.
Alisema alikuja kupata muongozo baada ya kufika Mwanza na kufunguka macho kwamba pesa sharti zifanyiwe mambo.
Alisema kwamba alipata kiwanja akapewa na mtu bila pesa, akajikusanya na kujenga kisha baadae akaja kumlipa pole pole yule mzee aliyempa nyumba.