Vyama vya siasa nchini Afrika Kusini, vimeanza mazungumzo ya kujaribu kutengeneza muungano utakayowezesha kuunda Serikali ya mseto. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Hatua hiyo inakuja wakati huu chama tawala cha ANC kikionekana kupoteza idadi kubwa ya viti kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30.
Licha ya kuwa chama hicho cha muasisi wa taifa hilo hayati Nelson Mandela kinatarajiwa kuwa na wabunge wengi baada ya uchaguzi wa Jumatano ya wiki hii, wapiga kura wamekiadhibu chama hicho cha harakati za ukombozi.
Wakati zaidi ya asilimia 80 ya kura zote zikiwa zimehesabiwa, katika matokeo hayo yanayoendelea kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEC), yanayonesha kuwa chama tawala cha African National Congress (ANC) kimefikia asilimia 41.37 ya kura zote kufikia jana Ijumaa jioni.
Matokeo ya awali yanaonyesha hali ya kupoteza wingi wa viti vya bunge kwa chama hicho tawala cha Rais Cyril Ramaphosa, ambacho kilipata 57.5% ya kura katika uchaguzi wa bunge uliofanyika 2019.
Chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) kinachoongozwa na John Steenhuisen, mpaka sasa kimefikia 22.16% ya kura huku chama kilichoanzishwa miezi sita tu iliyopita na rais wa zamani Jacob Zuma, uMkhonto we Sizwe (MK), kikijipatia asilimia 13.06 ya kura ilihali kile cha wapigania ukombozi wa kiuchumi, EFF, cha Julius Malema kikifikia asilimia 9.41 ya kura.
Wachambuzi wa siasa wanasema ANC pia itapoteza wingi wa kura katika jimbo lililoimarika kiuchumi la Gauteng, ambapo unapatikana mji mkuu Pretoria na kitovu cha biashara cha Johannesburg.
ANC pia inatarajiwa kupata kura ya chini ya asilimia 50 katika eneo la KwaZulu-Natal, nyumbani kwa kina Zuma.
Jimbo la Cape Magharibi, ambalo ni la pili kwa nguvu kiuchumi uliko mji wa Cape Town limetawaliwa kwa miaka mingi na chama cha DA. Matokeo ya awali yanaashiria kuwa chama hicho kitahifadhi wingi wake wa kura katika eneo hilo.
Bunge jipya litakalochaguliwa lazima liunde serikali na kumchagua rais ndani ya siku 14 baada ya tangazo la mwisho la matokeo.
Taifa hilo lenye idadi ya watu milioni 61, linakabiliwa na uchumi mbaya pamoja na kiwango kikubwa cha ukosefu ajira.