Naamini sasa watu wataiheshimu Ligi ya Tanzania [NBC Premier League] pamoja na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars.’
Kuna ambao walidhani ile sare ya Tanzania vs Zambia kwenye michuano ya AFCON ilikuwa ni kama bahati ‘fluke’ kwa Taifa Stars.
Ukiangalia kikosi cha Taifa Stars kilichoanza kwenye mchezo dhidi ya Zambia [kufuzu Kombe la Dunia 2026], wachezaji tisa [9] wanacheza Ligi ya nyumbani.
Ni wachezaji wawili tu kati ya 16 waliocheza mechi dhidi ya Zambia ndio wanacheza soka nje ya nchi. Wengine wote wakiwa wanacheza Ligi ya ndani huku mchezaji mwandamizi Mbwana Samatta akiwa nje ya kikosi.
Stars ikamudu kuizima Zambia vizuri tu ambayo kwenye kikosi chake walianza wachezaji nane [8] wanaocheza Ligi tofauti huko Ulaya.
Miaka saba [7] nyuma Ligi ya Tanzania haikuwepo hata katika Ligi bora 40 za Afrika! Lakini leo Ligi ya Tanzania ni miongoni mwa Ligi 10 bora za Afrika ikiwa nafasi ya sita [6].
Hivi karibuni wachezaji wao wengi wamepata fursa ya kucheza mashindano ya CAF mara kwa mara kutokana na ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye mashindano hayo kuanzia hatua ya makundi hadi hatua za mtoano.
Uzoefu wanaoupata wa kucheza dhidi ya klabu bora za Afrika kama Al Ahly, Wydad Casablanca, TP Mazembe, Mamelodi Sundowns sio tu umewafanya waboreshe viwango vyao lakini hawana tena presha ya kucheza mbele ya mashabiki 50,000.
Kumbuka Stars ilianza na golikipa namba tatu [3] wa Simba [Ally Salim] lakini timu ilicheza kwa utulivu na kwa kujiamini dhidi ya Zambia.
Umefika wakati ambao mataifa ambayo yalikuwa yamepiga hatua kadhaa mbele kwenye mchezo wa soka, yataanza kujifunza nini kinafanywa kwenye Ligi ya Tanzania na kuzalisha wachezaji wazuri kwa ajili ya timu ya taifa.
Amesema Kocha wa zamani wa Lesotho Bw. Thabo Senong.