Kuna kipindi kizito cha takribani siku 14 walichonacho Simba SC chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ambaye pia ni Rais wa Heshima wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’.
Simba SC ambayo hivi karibuni ilipata mtikisiko kidogo wa baadhi ya viongozi wake wa Bodi ya Wakurugenzi upande wa Mwekezaji kujiuzulu wote akiwemo Salim Abdallah ‘Tyr Again’ aliyekuwa mwenyekiti wa Bodi hiyo, imeanza kujengwa upya kutokana na Mo Dewji kurejea katika kiti hicho na kuwachagua wajumbe wake.
Ishu nzima ya kujiuzulu kwa wajumbe hao na mwenyekiti wao Try Again ilianzia pale Mo Dewji alipowataka kufanya hivyo kwa kile kilichoelezwa kushindwa kuiongoza vyema Simba ambayo kwa kipindi cha misimu mitatu mfululizo imelikosa taji la Ligi Kuu Bara lililokwenda kwa watani zao wa jadi, Yanga SC.
Baada ya wajumbe hao ambao ni Dk Raphael Chageni, Hamza Johari, Zulfikar Chandoo na Rashid Shangazi kujiuzulu, Jumapili iliyopita Mo Dewji alitengeneza safu mpya ya uongozi ambao wanaingia kwenye Bodi ya Wakurugenzi upande wa Mwekezaji. Walioteuliwa na Mo Dewji ambaye ndiye mwenyekiti wa bodi hiyo ni Salim Abdallah ‘Try Again’, Mohamed Nassoro, Crescentius Magori, Hussein Kita, Zulfikar Chandoo na Rashid Shangazi.
Wajumbe hao upande wa Mwekezaji wanakwenda kuungana na wale wa upande wa Wanachama wakiongozwa na Mwenyekiti wa Klabu, Murtaza Mangungu ambao ni Seif Ramadhan Muba, Asha Baraka, CPA Issa Masoud Iddi, Rodney Chiduo na Seleman Harubu.
Tangu Mo Dewji aunde safu hiyo mpya ya uongozi Juni 16, 2024, Simba ina takribani siku 14 ambazo ni sawa na wiki mbili kumaliza kila kitu kabla ya kuanza kwa maandalizi ya msimu mpya wa 2024-2025. Siku hizo 14 zinafikia tamati Juni 30 na mipango ya Simba kuanza maandalizi yao ya msimu ni Julai mwaka huu.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema hivi sasa wachezaji wapo kwenye mapumziko baada ya kumalizika kwa msimu wa 2023-2024 na wanatarajia kurejea Julai kuanza maandalizi ya msimu mpya.
“Wachezaji wetu wapo mapumziko na wanatarajia kurejea Julai na tunataka tukianza pre-season basi kila kitu kiwe kimekamilika kwa maana ya kukamilisha usajili, benchi la ufundi na kupata sehemu ya kwenda kuweka kambi ya pre season.
“Kitu ambacho tunakihitaji katika pre-season ya safari hii ni siku ya kwanza tunayoingia kambini tuwe tumekamilika wachezaji wote.
“Moja ya changamoto iliyokuwepo kwa siku za hivi karibuni na kutokana na ratiba na mipango ya usajili unajikuta unakwenda kwenye pre-season kuna mchezaji mwingine bado mpo katika kumalizana naye hivyo anajikuta amechelewa programu za mazoezi.
“Lakini moja ya mipango ambayo tumeimarisha safari hii siku ya kwanza tunaingia kambini basi wachezaji wote 30 wamekamilika, benchi la ufundi limekamilika, kisha tunafanya pre season iliyokamilika,” alisema Ally.
Hiyo inamaanisha, Simba inatarajia kuanza pre season wiki ya kwanza ya mwezi Julai na ni siku chache baada ya wachezaji wao kurejea kambini baada ya kumaliza mapumziko.
Timu hiyo yenye jumla ya mataji 22 ya Ligi Kuu Bara, ratiba yao inaonyesha kwamba pre season hiyo itakuwa ya takribani mwezi mmoja kwani mwanzoni mwa mwezi Agosti watakuwa na tamasha lao la Simba Day ambalo hufanyika kila mwaka tangu lilipoasisiwa mwaka 2009. Kisha watacheza mechi za Ngao ya Jamii kuanzia Agosti 8 hadi 11, kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Agosti 17.
USAJILI
Juni 15 mwaka huu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza kufunguliwa kwa dirisha kubwa la usajili ambalo litakwenda hadi Agosti 15, 2024 likidumu kwa miezi miwili.
Kufunguliwa kwa dirisha hilo la usajili kunatoa mwanya kwa timu za Ligi Kuu Bara, Championship, First League na Ligi Kuu Wanawake kuimarisha vikosi vyao kuelekea msimu wa 2024-2025.
Simba yenye mipango ya kuanza pre season wiki ya kwanza ya Julai mwaka huu, wana takribani siku 14 kukamilisha zoezi hilo ambapo taarifa zinabainisha kwamba, tayari imefikia pazuri katika kumsajili winga wa Power Dynamos ya Zambia, Joshua Mutale, huku ikimbakisha kipa wao, Ayoub Lakred ambaye msimu uliopita alifanya kazi kubwa ya kuziba pengo la Aishi Manula aliyekuwa majeruhi wa muda mrefu.
Katika usajili, taarifa kutoka ndani ya Simba zinabainisha kwamba Mo Dewji ameingia mwenyewe sokoni kuhakikisha wachezaji wanaohitajika wanatua ndani ya kikosi hicho lengo likiwa ni kutotoa mwanya tena kwa wapinzani wao kuendelea kutawala ndani ya Ligi Kuu Bara.
VIONGOZI
Siku chache baada ya Mo Dewji kutangaza safu mpya ya uongozi wa Bodi ya Wakurugenzi upande wa mwekezaji, yameibuka maswali mengi ya kwa nini waliojiuzulu wamerudishwa huku sintofahamu ikiibuka ya uhalali wa Mo Dewji kurejea kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi baada ya kujiuzulu.
Mengi yalizungumzwa ikiwemo kauli ya Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu kubainisha kwamba watakaa kama bodi kumchagua mwenyekiti wa. Kabla ya hayo hayajafanyika, Mo Dewji ameendelea kufanya majukumu ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba.
Ili kuondoa sintofahamu hizi zote, viongozi wa Simba kwanza wanapaswa kuwa wamoja kwa maana ya wale Wajumbe wa Bodi upande wa Mwekezaji na Wanachama ili kuijenga Simba moja, lakini pia wanachama na mashabiki wa timu hiyo kukubaliana na kauli za viongozi wao.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, ametuliza upepo huo kwa kusema: “Tuachane na mambo yote na badala yake tujikite kuisaidia Simba SC, hapa tulipofikia tunahitaji kusimama imara na Simba yetu, kusimama pamoja na Simba yetu, tunapaswa kuwa ushirikiano wa asilimia 100 na viongozi wetu, wana kazi kubwa viongozi wetu ya kuandaa pre season, kufanya usajili na kuboresha benchi la ufundi, hawataweza kuifanya kazi hiyo kama tunaendelea kuwapigia kelele muda wote.
“Tuwape muda na utulivu waweze kuitengeneza Simba yetu kwani ukiwa na utulivu unapata nafasi ya kufanya vitu bora na sahihi kabisa lakini ukiwa kwenye presha unakuwa katika nafasi ya kukosea. Wakikosea viongozi wetu ndiyo imekosea Simba SC na msiba unarudi kwetu sisi Wanasimba.
“Tumeshakosa ubingwa mara tatu, hivyo kama tusipotuliza akili Wanasimba tunaweza kukosa mara ya nne lakini tuna uwezo wa kufanya msimu uliomalizika ndiyo mwisho wa mateso na msimu ujao ukawa wa mafanikio na tunawezaje kufanya hivyo muda ni huu wa pre season kuijenga Simba yetu,” alisema Ally.
KOCHA
Jambo muhimu zaidi ambalo Simba wanapaswa kulifanya ndani ya siku hizo 14 kabla hata ya kutangaza wachezaji wapya waliowasajili ni kumtambulisha kocha mkuu anayekuja kuchukua nafasi ya Abdelhak Benchikha ambaye aliachana na timu hiyo Aprili mwaka huu akiiongoza kwa takribani miezi mitano kuanzia Novemba 2023.
Benchikha alichukua mikoba ya Roberto Oliveira ‘Robertinho’ lakini alishindwa kuifanya Simba kupata mafanikio yaliyotarajiwa, mapema akatupa taulo. Kikosi hicho kikawa chini ya makocha wazawa Juma Mgunda akiwa Kaimu Kocha Mkuu akisaidiana na Seleman Matola, wakamaliza ligi nafasi ya tatu na kupata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.
Mwanaspoti linafahamu kwamba Simba limezungumza na Kocha Steve Komphela (56) kutoka Afrika Kusini ambaye anasubiri muda ufike atambulishwe kama mambo hayatabadilika kwani tangu taarifa zake zivuje, kumekuwa na ukimya hapo kati.
Ikiwa kocha huyo ndiye mrithi wa Benchikha, anapaswa kutangazwa ndani ya siku hizi 14 kabla ya kikosi hicho hakijaanza kambi yao ya pre season.
PRE-SEASON
Hapa ndipo kuna jambo lingine muhimu kufanyika kwani Simba katika misimu mitatu iliyokosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, kambi yao ya maandalizi ya msimu ilikuwa nje ya nchi na zote hazikuwa na matunda mazuri.
Wakati Simba ikienda nje ya nchi, watani zao wa jadi Yanga walibaki hapa nchini na kujificha Avic Town pale Kigamboni jijini Dar es Salaam na kusuka mabomu ambayo yamewapa mafanikio makubwa kipindi hicho chote kwa kubeba mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA), huku timu hiyo ikicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023 ikiwa ni mara yao ya kwanza kufanya hivyo na kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2023-2024 ikiwa ni mara ya kwanza pia.
Hilo la pre season ya Simba kuelekea msimu ujao, majadiliano yamekuwa makubwa sana lakini kwa taarifa zilizopo ni kwamba timu hiyo safari hii imeamua kubaki hapa nchini kutokana na muda uliopo kuwabana zaidi.
“Majadiliano yamekuwa makubwa ndani ya Simba SC kuanisha na kuangalia wapi twende tukaweke kambi yetu, tumeangalia kwa ufinyu wa muda uliopo ni sehemu gani sahihi twende tukaweke kambi.
“Mapendekezo yamekuwa mengi nje ya nchi na ndani ya nchi, imetajwa Afrika Kusini, Morocco, Uturuki na sehemu nyingine nyingi sana ambazo Simba SC inaweza kwenda kuweka kambi, lakini hapa ndani ya Tanzania kuna Morogoro maeneo ya Bigwa pale ni sehemu nzuri ya kuweka kambi, Lushoto milimani kule ndanindani, kuna Arusha, hivyo majadiliano yanaendelea na muda si mrefu tutakuja kuwaambia Wanasimba wapi timu yao inaweka kambi lakini itakuwa kambi nzuri na yenye matunda makubwa,” alisema Ahmed Ally ambaye ni Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba.