Simba, Mo Dewji wayamalize kiungwana

 

Simba, Mo Dewji wayamalize kiungwana

Simba na Mohammed Dewji hakuna anayepaswa kumnyooshea kidole mwenzake katika hili linaloendelea hivyo jambo la msingi lazima wakae chini wayamalize.


Kila upande umefanya makosa ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangia kuvuruga hali ya mambo ndani ya klabu hiyo leo hii hadi kufikia hatua ya watu kusutana hadharani.


Klabu kwa upande wake imeshindwa kukamilisha mambo muhimu yanayohitajika na ya msingi katika kufanya mchakato wa uwekezaji upitishwe kama vile kufanya tathmini ya mali na madeni ya klabu na mwisho wa siku jambo linashindwa kukamilika.


Laiti kama klabu ingekuwa imekamilisha masuala muhimu maana yake ingekuwa rahisi kwa mamlaka za kiserikali ambazo zinahusika na ufanyaji tathmini na upembuzi wa masuala ya uwekezaji na michezo kupitisha mfumo huo ndani ya Simba.


Lakini kosa jingine la upande wa klabu ni kutokuwa na uwazi na ukweli katika uwasilishaji taarifa kwa wapenzi, mashabiki na wanachama ambapo mara kwa mara imekuwa ikitoa taarifa zisizo sahihi mbele za umma ili tu kutuliza watu.


Mfano klabu mara kadhaa imekuwa ikijinasibu mbele ya kadamnasi kuwa tajiri ameweka Sh20 bilioni kwenye akaunti na kila mwaka inajizalisha na ile faida inarudishwa katika shughuli za kawaida za uendeshaji wa timu lakini leo hii inamgeuka mwekezaji wao kuwa hajatoa hiyo fedha kwa klabu na kile anachotoa kusaidia uendeshaji amekuwa anakidai.


Kwa upande wa tajiri nako kuna matatizo na kubwa zaidi ni kutokuwa tayari kufuata utaratibu rasmi wa uendeshaji wa timu na kufanya mambo kienyeji jambo ambalo limesababisha mchakato kukwama kwama mara kadhaa.


Klabu bado haijaingia kwenye uwekezaji lakini Dewji anatangazwa kuwa yeye ndio muwekezaji na analifurahia hilo huku akifahamu kinachofanyika sio sahihi hadi pale mamlaka za serikali zitakapolipitisha jambo hilo.


Mwenyewe Dewji pia aliwahi kufanya mahojiano na kudai kwamba aliinunua klabu hiyo miaka kadhaa iliyopita, kauli hii pia imekuwa ikimsababishia kusakamwa sana watu wakihoji aliinunua lini na aliinunua kutoka kwa nani na katika utaratibu upi, vitu ambavyo Mo mwenyewe hakurudi tena kuvitolea ufafanuzi.


Ishu hapa iko hivi, kama klabu haijaingia katika uwekezaji, Dewji alipaswa kutotoa fedha zake za mfukoni na kuipa Simba bila utaratibu maalum kwani kunakuwa hakuna kinga na ulinzi kwa upande wake siku za usoni iwapo mchakato utakwama.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad