Simba Yaanza Kusuka Kikosi, Saba Waonyeshwa Mlango wa Kutoka...




KLABU ya Simba imeanza mipango ya kukisuka upya kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao na mashindano ya Kimataifa huku ikielezwa tayari wachezaji saba tayari wameshaonyeshwa mlango wa kutokea.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema wachezaji ambao tayari wamepigwa panga na wataachwa ndani ya timu hiyo wameshajulikana na watawapisha wachezaji wapya wenye uwezo wa kurudishia makali yake timu hiyo.

Wachezaji ambao wanaotajwa kuachwa na timu hiyo ni Saidi Ntibazonkiza, Luis Miquissone, Jobe Pa Omar, Freddy Michael, Babacar Sarr, Henock Inonga na mzawa Aishi Manula.

Hata hivyo, chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya timu hiyo kinasema hilo ni panga la awamu ya kwanza, lakini pia kuna panga lingine ambalo litawahusisha zaidi wachezaji wazawa.

"Vikao vinaendelea kufanya tathimini lakini hao ndi wala ambao ni uhakika wataondoka ndani ya timu, uongozi unaendelea na vikao kuangalia wengine ambao mchango wao haukuwa mkubwa ndani ya timu, lengo ni kubaki na wachezaji ambao walikuwa na mchango na kuwaongeza ambao watakuja kuiinua timu na kuirudisha kwenye nafasi yake msimu ujao," kilisema chanzo hicho.

Kati ya wachezaji hao wanaotarajiwa kuachwa kwa mujibu wa chanzo chetu, Jobe, Freddy na Babacar, wote walisajiliwa kipindi cha uhamisho wa dirisha dogo msimu uliomalizika, lakini hadi sasa hawajawavutia mashabiki wa klabu hiyo.

Inonga na Miquissone wenyewe wanatarajiwa kuuzwa, huku Manula akimaliza mkataba wake msimu huu na klabu haijaonyesha nia ya kuendelea naye.

Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Murtaza Mangungu, amesema kwa sasa ni lazima wapate muda wa kufanya tathimni ya kile kilichotokea baada ya msimu wa mashindano kumalizika, lakini ni lazima yafanyike maboresho kwenye kikosi.

"Ni lazima tupate muda wa kufanya tathmini ili kubainisha mapungufu ya msimu uliomalizika, tutapokea taarifa kutoka benchi la ufundi na maeneo yote, halafu baada ya hapo ndiyo tutajua nini tunatakiwa kufanya.

Lakini kwa namna yoyote ile, tutafanya marekebisho yanayohitajika pale tutakapoona kuna mapungufu na panapohitaji kuboreshwa pataboreshwa na hili tutatoa taarifa rasmi baadaye inayohusu mwenendo wa ligi msimu huu na mashindano mengine tuliyoshiriki," alisema Mwenyekiti huyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad